ILIPOISHIA…
Nilijitutumua kisha kuketi upande upande. Niliunyanyua mkono wangu kuzitazama pingu zilizokuwa zimeung’angania mkono wangu kama ruba. Nilijaribu kuing’ata kwa meno yangu ili itanuke.
La hasha!
Ilizidi kukaza na kuusaga mkono wangu. Sikuwa nazijua pingu kwa hakika. Nilikuwa nikizisikia tu kwa mazungumzo ya vijiweni pia kupitia runinga mbalimbali za mapigano na uhalifu ambazo askari walikuwa wakiwatia nazo watuhumiwa wenye hila.
SASA ENDELEA…
MUDA ule zilikuwa mkononi kwangu. Sikuwa na haja ya kuuliza juu yake. Nikiwa bado nafurukuta, ghafla askari aliingia. Alikuwa na chupa ya chai mkononi, mfuko wa nailoni mweusi ambao baada ya kuivuta harufu kulikuwemo vitumbua.
Aliniletea chai.
Nilimtazama usoni, hakutabasamu wala kuonesha hisia za kutaka kuzungumza nami. Nilimtazama kwa kumkazia macho, niliukagua mwili wake haraka. Juu kisha chini.
Salale!
Alikuwa amebeba bunduki yake kama begi. Ilitanda mgongoni na kujishikiza ubavuni. Matumaini yalinihama.
Nia yangu ya kutaka kupata upenyo wa kutoroka yalikuwa sawa na mtu atakaye kushindana kwa mbio za miguu angali kiwete asiye baiskeli. Nilibaki kimya.
Askari aliimimina chai kwenye kikombe kilichokuwa pale pembeni kwenye kijimeza kidogo cha duara. Alikisukuma kikanisogelea. Alinitazama kisha kutingisha kichwa kabla ya maneno kumtoka.
“Muuaji umeamka. Bila shaka upo tayari kuyakabili mashitaka yanayokukabili leo mahakamani,” alisema askari yule kisha kusogea pembeni akinitazama wakati nikiwa najaribu kunywa chai.
Sikuhisi njaa bali tumbo la hofu liliniparamia. Sijawahi kufika mahakamani tangu kuzaliwa kwangu. Si kwa shauri hata kutembea ama kujifunza lolote kuhusu mahakama.
Mahakama na jeshi la polisi pamoja na mahakimu kwangu ilikuwa nadra kuwawaza bali niliwahofu kwa maamuzi yao makubwa. Nilipiga funda tatu za chai na kukimeza kitumbua kimoja kisha kutoa ishara ya kushukuru.
Yote sababu ya hofu pia sauti iliyopotea.
***
Baada ya kumaliza kunywa chai niliyofadhiliwa na kituo cha polisi, sikuwa na utambuzi wa kile ambacho kingefuata baadaye.
Sawa, akilini niliwaza kuwa ilikuwa wasaa wa kupelekwa mahamani. Sikuwa nafahamu hatua ambazo zilipaswa kufuatwa kuliendesha shitaka lile.
Nililokuwa najua na kuhisi akilini ilikuwa ni kuwaona hakimu na waendesha mashitaka wakinitia hatiani kisha kunihukumu kwa kifungo cha maisha jela au kifo cha kunyongwa.
Sikuwaza lolote zaidi. Nilikata tamaa na kuamini siku ilikuwa ikienda kutimia. Nikiwa bado katika tafakari ya kile ambacho sikuwa na uzoefu nacho, ghafla mlangoni niliwaona askari wawili wakinijia.
Walikuwa tofauti na yule ambaye aliniletea chai. Walikuja moja kwa moja hadi kitandani nilipokuwa nimejilaza. Hawakusema neno bali mmoja alinifungua pingu za mguuni na mwingine alinifungua mkononi kisha kunifunga tena mikono yangu yote kwa kuikusanya.
Mmoja alisimama kushoto na mwingine kulia kwangu kisha kuninyanyua. Walinitua chini ya sakafu. Walinitazama kwa jicho la muuaji aliyeogopeka. Askari mmoja katika wima ule alinitamkia nisimame kisha tuondoke.
Nilisimama wima kisha tulianza kuondoka. Nilikuwa katikati yao, mmoja kulia mwingine kushoto. Tulipotoka kwenye mlango wa chumba nilimokuwa nimelazwa, kwa nje tuliwakuta askari wengine watatu wenye silaha, jumla walikuwa watano.
Tayari nilianza kusukumwa kama gari bovu lililozima kilimani. Nilipoyaangaza macho yangu, moja kwa moja yalienda hadi kwenye gari lililokuwa pembeni ya hospitali. Nako kulikuwa na askari watatu wenye silaha wakiningoja. Walipoiona sura ayangu nao walikaa kwa hadhari.
Nilipelekwa hobelahobela kisha kulipanda gari lile. Kwa kuwa tulipanda nyuma ya gari lile la wazi, nililazimika kuketi chini kwa mamlaka ya askari. Walisimama wima kunizunguka nami kuwatazama kwa hofu kwani sikuwa naamini kama nilikuwa mtu mwenye kulindwa kama dungu la fedha za umma zilizookolewa.
Nilikuwa dhaifu hata unyasi ungeweza kuniua. Katika safari ya kutoka hospitali, askari wale walipiga soga za hapa na pale. Wakati waliniteta pia kunitolea maneno machafu ambayo yaliukera moyo wangu.
Lakini sikuwa na namna. Kweli niliua. Niliua kwa makusudi au kwa kukusudia hilo lilikuwa juu ya uamuzi wa walionitwaa. Nilikuwa zumbukuku wa sheria wala sikufahamu jambo lolote. Zaidi nilikuwa nafahamu adhabu ya kosa nililokuwa nimelifanya. Nilikuwa tayari kuhukumiwa.
Ilichukua dakika chache sana, hatimaye tulifika eneo la mahakama. Kulikuwa na watu wengi waliojazana. Wengi walitaka kujua kisa kile na wengine walitaka kuandika habari kuujuza ulimwengu.
Wengine walitaka kuishuhudia sura yangu kwa tukio ambalo lilikuwa limetawala kote duniani. Kila jicho lilikuwa na hamu ya kumjua muuaji Mbununu alifafanaje.
Baada ya kushuka toka ndani ya gari lile, gari rafiki kwa wahalifu na watuhumiwa, niliongozwa hadi ndani ya ukumbi wa mahakama.
Nilifikishwa hadi sehemu ambayo nilipaswa kuketi ningali katika shinikizo la pingu. Nikiwa nangoja mahakama kuanza, sauti ya kujitetea ilianza kunivaa akilini mwangu. Niliwaza kisha kupata suluhu lakini haikuwa suluhu ya kina.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia Jumamosi ijayo.