30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KITWANA KONDO AFARIKI DUNIA DAR

 

 

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

MWANASIASA mkongwe na Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Kitwana Kondo (88), amefariki dunia.

 Mtoto mkubwa wa kiume wa mwanasiasa huyo, Adinan Kondo  alisema kuwa baba yake alifariki dunia jana    saa 11 jioni katika Hospitali ya Hindu Mandal,   Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo ambaye alikuwa maarufu kwa jina la ‘KK’, awali alikuwa akisumbuliwa na kiharusi kilichompata tangu mwaka 2013.

Adinan alisema  baba yake  walimkimbiza hospitalini hapo kwa matibabu na kulazwa baada ya kuzidiwa.

Viongozi mbalimbali walifika hospitalini hapo kumjulia hali akiwamo Rais mstaafu  Jakaya Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Wengine ni  Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa   na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye   alikuwa akienda hospitalini hapo mara kwa mara.

Kitwana Kondo ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini ambaye ambaye pia aliwahi kuwa mbunge wa Kigamboni kuanzia mwaka 1995 hadi 2000 kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, alishindwa kutetea nafasi yake kwa kubwagwa na Frank Magoba wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye kwa sasa amejiunga na CCM.

Februari 2, 1999 Kitwana Kondo akiwa Mbunge wa Kigamboni, alisimama ndani ya Bunge na kutoa hoja ya kuitaka Serikali iondoe kero zinazowasibu Waislamu na makundi yote ya wanaharakati ya Kiislamu.

Vilevile kwenye miaka ya 1990 alikuwa  mmoja wa viongozi waliozima hatua ya kuvunjwa mabucha ya nguruwe katika eneo la Kigogo kwa   kufanya mazungumzo na viongozi wa dini ya Kiislamu akiwamo marehemu Sheikh Kassim Bin Jumaa, aliyekuwa imamu wa Msikiti wa Mtoro.

Akizungumzia msiba huo jana, Mbunge wa Kigamboni Dk.Faustine Ndugulile (CCM), alisema amepokea kwa masikitiko taarifa za  msiba huo ambao kwake ni mkubwa.

Alisema Kondo alikuwa mtangulizi wake na hata katika harakati za kugombea ubunge aliwahi kupata ushauri kwake.

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo kwa sababu  siyo tu kwa kuwa aliwahi kuwa meya lakini pia alikuwa mtangulizi wangu katika jimbo la Kigamboni.

“Nawapa pole wafiwa wote na pia wana CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam,’’alisema Dk. Ndugulile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles