Na Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM
KUTOKANA na kasi ya ujenzi wa Barabara ya Juu Ubungo (Fly Over), serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendeyo Haraka (DART) imepanga kuhamisha matumizi ya Kituo cha Ubungo Maji kupisha ujenzi huo.
Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki, Mtendaji Mkuu wa DART, Ronald Lwakatare, alisema changamoto ya ujenzi huo sasa unalazimu kufanya mabadiliko kwenye kituo hicho.
“Ujenzi was Fly Over ya Ubungo, hasa katika eneo letu la Ubungo Maji sasa tunajitahidi kuhakikisha tunabadili kituo ili watu wawe salama.
“Tunaelewa ni kituo kinachopendwa na watu wengi nasi kama Dart siku zote tunajali usalama wa watu,” alisema Lwakatare.
MBIA WA PILI
Alipoulizwa mchakato wa kumpa mbia wa pili kwa ajili ya kuendesha mradi huo wa mabasi ya mwendokasi, Lwakatare, alisema bado mchakato huo unaendelea.
“Masuala ya ununuzi kwa hiyo tupo mbioni kutafuta mtu atakayeleta huduma ya mabasi na tunaendelea na juhudi za kumpata.
“Tunaamini tutafika mwisho tunajitahidi kuhakikisha kuna mabasi ya kutosha kwa sababu mwitikio umekuwa mkubwa sana,” alisema.
UJENZI NJIA YA MBAGALA
Mtendaji Mkuu huyo wa DART, alisema kwa sasa taratibu ziko mbioni kukamilika kuhusu mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa Mbagala ambaye ataanza kazi mwishoni mwa mwaka huu.
“Mungu akipenda mwishoni mwa mwaka huu mkandarasi huenda akawa site (eneo la ujenzi) kwa njia ya Mbagala. Tunawaomba na tunawashukuru wananchi kwa kuupokea vizuri mradi huu,” alisema.