Na Mwandishi wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amezindua kituo cha kisasa cha kujazia gesi asilia chenye uwezo wa kuhudumia magari zaidi ya 800 ikiwa ni utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kuchochea matumizi nishati safi.
Uzinduzi wa kituo hicho kilichojengwa na kampuni ya TAQA Arabia na washirika wao JCG Oil & Gas, umefanyika jana Novemba 11, 2023 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na mabalozi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk. Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uwekezaji wa sekta ya Nishati.
“Serikali inaweka msukumo mkubwa kwenye matumizi ya gesi ya asilia yakiwemo magari, mitambo ya viwandani, hivyo kuzinduliwa kwa kituo hicho ni kuonesha azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa gesi inayopatikana Tanzania inatumika ndani ya nchi kwanza,”amesema .
Amesema kituo hicho kitajaza gesi kwenye gari moja kwa dakika tatu, hivyo kitasaidia kubadilisha magari ya mafuta ili yatumie gesi.
Amesema kampuni hiyo inatarajia kujenga vituo 12 vingine jijini ili kuwa navyo vingi zaidi vya kujazia gesi kwenye magari.
Ameongeza kuwa, kampuni hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wapo kwenye majadiliano ili kujenga vituo vidogo vya Gesi ya Kusindika (LNG) ili kuweza kutoa gesi Dar es Salaam na kupeleka kwenye mikoa mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kutekeleza maono ya Rais Samia ya usambazaji wa nishati katika maeneo yote ikiwamo gesi asilia.
Amesema wilaya yake inaona fahari kufunguliwa kwa kituo hicho kutokana na kuwa kitovu cha Mkoa wa Dar es Salaam kwani, ina wananchi wasiopungua milioni 1.6 ukilinganisha na idadi yote ya wakazi wa mkoa huo ambao jumla yao ni milioni 5.3.