Kituo cha demokrasia chatoa mapendekezo

0
496

LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM

KITUO cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimetoa mapendekezo  yanayopaswa kufanywa na vyama vya siasa ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa, hasa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Mapendekezo hayo yametolewa Dar es Salaam jana na mhadhiri kutoka Ndaki ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Consolata Sulley, alipokuwa akiwasilisha mada katika warsha ya viongozi wa ngazi ya juu wa vyama vya siasa iliyolenga kujadili na kuridhia mapendekezo ya taratibu za uteuzi wa wagombea iliyoandaliwa na TCD.

Kuhusu kupata watu wanaostahili kugombea kuwa watia nia, walipendekeza kubuni kampeni za kujenga ufahamu ndani ya vyama kuhusu uhalisia wa utengwaji wanawake kisiasa ndani ya vyama na katika vyombo vya maamuzi serikalini.

Dk. Consolata alisema hatua hiyo itawafanya viongozi wa vyama na wanachama kufahamu kuwapo kwa tatizo la ushiriki mdogo wa wanawake na itahamasisha na kuhimiza wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama na Serikali.

Pendekezo jingine ni kuanziasha sheria au kanuni za vyama kudhibiti vurugu dhidi ya wanawake katika mchakato wa kura za maoni ili kuhakikisha usalama binafsi kwao na kupunguza matukio ya vurugu za uchaguzi jambo ambalo linaweza kuhakikisha fursa sawa ya ushindani kwa wanawake na wanaume katika siasa.

“Pia ni vyama kuanzisha programu za kujenga uwezo wa kiongozi na kujiamini kwa wanawake kwa kuwalenga wanawake wanaowania uongozi kwa sasa na wale ambao wanaweza kufanya hivyo katika siku za usoni.

“Kuanzisha mpango mkakati wa kuwafikia na kuwatambua wanawake ambao wanaweza kuwa wagombea bora na kuhimiza wanawake kuwania nafasi za uongozi,” alisema.

Kuhusu kuwezesha watia nia kuwa wagombea, walipendekeza kuwa na makubaliano na utashi wa kisiasa ndani ya uongozi wa chama husika ili kukuza ushiriki wa wanawake kikamilifu katika uchaguzi, kuweka na kurasimisha mfumo wa uwiano wa uteuzi wagombea aidha kisheria au uwiano wa hiari.

Mwakilishi wa Mtandao wa Wanawake, Katiba na Uongozi, Victoria Mandari, alishauri ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha kuwa chama chochote kinachoomba kusajiliwa kizingatie kifungu cha 6 A cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinachotaka kuwapo uwiano wa kijinsia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here