Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imezuia wafanyabiashara wa nguruwe kuuza nyama na mazao yake baada ya kuwapo kwa mlipuko wa homa ya nguruwe.
Hata hivyo, halmashauri hiyo imesema wanyama hao na mazao yake wataingia kwa kibali maalumu cha barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Ramadhani Juma, imeeleza kuwa zuio hilo limetolewa kupitia Sheria ya Magonjwa ya Mifugo namba 17 ya mwaka 2003, kifungu cha 15.
“Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kwa mamlaka waliyonayo kupitia sheria ya magonjwa ya mifugo namba 17 ya 2003 kifungu cha 15, inatangaza rasmi kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe wilayani Dodoma,” alisema.
Juma alisema kutokana na hali hiyo manispaa hiyo imeweka zuio la kufanya biashara ya nguruwe na mazao yake hadi itakapotangazwa.
Alisema kwa sasa manispaa hiyo haitaruhusu mnyama yoyote jamii ya nguruwe wakiwamo ngiri, nguruwe pori na wa kufugwa kuingia katika eneo hilo bila kibali maalumu kutoka katika ofisi ya manispaa.
Pia alisema zuio hilo limejumuisha bidhaa zote zitokanazo na nguruwe, ikiwamo mbolea, kinyesi, mkojo na damu ambazo kwa pamoja hazitaruhusiwa kusafirishwa, kuingizwa ama kutolewa nje ya Wilaya ya Dodoma bila kibali hicho.