25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kitakacho ikwamisha Man City ni safu ya ulinzi

BADI MCHOMOLO

KWA sasa Manchester City ni moja kati ya timu zinazotajwa kuwa bora duniani kutokana na aina ya wachezaji walionao pamoja na kocha mwenye uwezo wa hali ya juu wa kufundisha soka, Pep Guardiola.

Ilikuwa Jumatatu ya Februari 1, 2016, uongozi wa Manchester City ulipotangaza kuinasa saini ya kocha Guardiola kutoka Bayern Munich, walitangaza mkataba wa miaka mitatu huku wakiamini ndani ya kipindi hicho timu yao itakuwa na mabadiliko makubwa hasa kwenye mafanikio ya soka.

Mbali Guardiola kuwa na uwezo wa kufundisha, lakini ana ushawishi wa kusajili wachezaji wazuri ambao wanaweza kumsaidia kwenye kikosi chake popote anapokwenda, amefanya hivyo akiwa na Barcelona na Bayern Munich kabla ya kutua Manchester City.

Msimu wa kwanza ndani ya Man City haukuwa bora kwake kwa kuwa alihitaji kuitengeneza timu hiyo kwenye mifumo yake, hivyo baada ya msimu kumalizika hakuweza kwenda likizo aliamua kukaa na kusuka mipango mipya.

Msimu wake wa pili 2017/2018 alifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu England na msimu uliofuata 2018/2019 akaweza kulitetea taji hilo akichukua kwa mara ya pili mfululizo, lakini msimu huu ana kazi kubwa ya kufanya ili kuweza kuchukua kwa mara ya tatu kutokana na upinzani pamoja na majeruhi waliyonayo wachezaji wake.

Ubora wa timu unatokana na uimara wa safu ya ulinzi pamoja na washambuliaji, kwa upande wa ushambuliaji kwa Man City hakuna shida, juzi wametoka kuichapa Watford mabao 8-0, ila kwa walinzi shida ipo tena kubwa.

Hii ni mara baada ya kutangaza kuondoka kwa beki wao wa kati Vincent Kompany aliyemaliza mkataba wake na kuamua kurudi katika klabu yake ya utotoni R.S.C. Anderlecht akiwa kama kocha mchezaji.

Manchester City ikawa inabakiwa na mabeki wake Aymeric Laporte, John Stones na Nicholas Otamendi, lakini mapema mwanzoni mwa msimu huu Laporte na Stones wameingia kwenye orodha ya wachezaji majeruhi na kuifanya timu hiyo ianze kwa kusua sua katika baadhi ya michezo yao.

Laporte ambaye alikuwa kwenye muhimili mkubwa wa timu hiyo kuumia kwake kutamfanya awe nje ya uwanja kwa miezi sita, wakati huo Stone anaweza kuwa nje kwa wiki nne hadi tano jambo ambalo litamfanya Guardiola abadilishe mifumo yake.

Kwa hali hiyo Guardiola amebakiwa na beki mmoja ambaye mwenye uzoefu, Nicholas Otamendi. Lakini mchezaji huyo hakuonesha kiwango kizuri wakati wa mchezo wa wiki moja iliopita dhidi ya Norwich ambapo City ilikubali kichapo cha mabao 3-2, huku beki huyo akisababisha kufungwa moja ya bao katika kipigo hicho.

Kutokana na aina ya wachezaji alionao Guardiola kwenye kikosi hicho anaweza kuliziba tatizo hilo kwa muda endapo ataamua kufanya yafuatayo.

Kumrudisha nyuma Fernandinho

Huyu ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, amekuwa akitoa mchango wa hali ya juu katika kuwalinda mabeki wake, hivyo ana uwezo huo wa kucheza nafasi za ulinzi.

Msimu uliopita mchezaji huyo aliwahi kuchezeshwa kama beki wa kati na aliweza kufanya yale ambayo aliagizwa na kocha huyo. Kutokana na tatizo walilonalo sasa Fernandinho anaweza kusaidiana na Otamendi kuimarisha ulinzi.

Kumpa nafasi Rodri

Julai 3 mwaka huu Manchester City walitangaza kumsajili Rodrigo Cascante maarufu kwa jina la Rodri akitokea klabu ya Atletico Madrid. Mchezaji huyo alisajiliwa kwa ajili ya kuja kuwa msaidizi wa Fernandinho hapo baadae na ndio maana alisaini mkataba wa miaka mitano.

Hivyo huu ni wakati sasa wa Guardiola kuamua kumtumia mchezaji huyo kwenye safu ya ulinzi pamoja na Otamendi ili kumuacha Fernandinho akiwa huru kwenye safu ya kiungo mkabaji. Ila kutokana na kukosa uzoefu wa kucheza michezo mingi anaweza kucheza nafasi ya kiungo na kumuacha Fernandinho akirudi nyuma.

Kuwaamini chipukizi

Eric Garcia ni jina la mchezaji chipukizi wa timu hiyo mwenye umri wa miaka 18, tangu amekuwa kwenye kikosi hicho cha wakubwa amecheza michezo mitatu tu tangu 2018, akicheza mchezo mmoja kwenye michuano ya Ligi msimu uliopita ambapo uwezo wake ni kucheza beki wa kati, lakini hajawahi kupata nafasi kwenye Ligi Kuu.

Kinda mwingine ni Taylor Harwood-Bellis mwenye umri wa miaka 17, hana uzoefu kutokana na kukosa namba, lakini wachezaji hao wana uwezo wa kucheza nafasi za ulinzi.

Kumtumia Kyle Walker

Walker ni chaguo la Guardiola katika nafasi ya beki wa kulia. Mchezaji huyo wa timu ya taifa England alilifikisha taifa hilo nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. Guardiola anamuamini mchezaji huyo tangu alipomsajili mwaka 2017 akitokea Tottenham, hivyo anaweza kumtumia katika nafasi ya ulinzi pale inapobidi.

Ufundi

Guardiola anajulikana kwa ufundi, anaweza kumtengeneza mchezaji na akawa bora zaidi kama ilivyo kwa mshambuliaji wake wa pembeni Raheem Sterling alivyo kwenye kiwango cha juu.

Anaweza kuwatumia wachezaji wake kwa ufundi akiwaweka walinzi watatu Oleksandr Zinchenko akikaba kushoto, Otamendi katikati huku Walker akiwa kulia au kati ya Fernandinho na Rodri akicheza kati.

Kusajili beki

Njia nyingine ambayo inaweza kumsaidia kocha huyo ni kuingia sokoni kutafuta beki mpya wakati huu wa kiangazi. Japokuwa usajili umefungwa lakini wanaweza kusajili wachezaji ambao hawana timu kwa sasa kama vile aliyekuwa beki wa Watford, Younes Kaboul na beki wa Aston Vila, Chris Samba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles