27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kitabu cha Mkapa kizito

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

KITABU cha maisha binafsi ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kiitwacho ‘My Life, My Purpose’ (Maisha Yangu, Kusudio Langu), kimezinduliwa ambapo pamoja na mambo mengine kimeeleza aliyokumbana nayo wakati wa utawala wake.

Kilizinduliwa jana Dar es Salaam na Rais Dk. John Magufuli, katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na marais wastaafu; Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete na viongozi wengine wastaafu.

Kitabu hicho kilichoandaliwa na Taasisi ya Uongozi Institute kikiwa na kurasa 316 na sura 16, kilianza kuandaliwa tangu mwaka 2016 na kimegharimu Sh milioni 230.

Akichambua kitabu hicho, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, alisema Mkapa katika kitabu hicho amefichua kuwa mauaji ya watu 21 visiwani Pemba ni kati ya tukio lililotia doa katika uongozi wake.

“Vifo vya watu 21 mwaka 2001 kule Zanzibar vilimhuzunisha sana, hili litaendelea kuwa doa katika utawala wake ingawa anasema hakuwepo vilipotokea,” alisema.

Mauaji hayo ya Januari 27 mwaka 2001 yalitokana na mgogoro wa kisiasa wakati polisi wakizima maandamano ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2000.

Walikuwa wakipinga matokeo ambayo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimtangaza aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Amani Abeid Karume kuwa Rais wa Zanzibar kwa kumshinda aliyekuwa mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

CUF walikuwa wanapinga matokeo hayo wakidai ‘yamepikwa’ na mgombea wao ndiye aliyekuwa ameshinda katika uchaguzi huo uliokuwa umeshirikisha vyama vingi vya siasa viwasini humo uliofanyika kwa mara ya pili tangu ule wa mwaka 1995.

Vilevile Profesa Mukandala alisema kuwa Mkapa anakiri katika kitabu hicho kuwa kati ya mageuzi aliyoyafanya wakati wa utawala wake yaliyokuwa na utata, ni pamoja na kubinafsishwa kwa mashirika ya umma.

“Rais Mkapa anasimulia pia mageuzi au maboresho ya utumishi na uuzaji wa nyumba za Serikali. Pia anasema mashirika ya umma yalikuwa yakiendeshwa kwa hasara.

“Kuna wanaodai kuwa Mwalimu Nyerere hakupenda ubinafsishwaji, lakini yeye Mkapa anasema Mwalimu Nyerere hakulisema, lakini aliona hali halisi na anasema kwa bahati mbaya hakufuatilia utendaji wa mashirika yaliyobinafsishwa,” alisema Profesa Mukandala.

Katika kitabu hicho, Mkapa anasimulia kuwa maono yake yalikuwa ni maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa kipato. 

 “Anasimulia kuwa kwenye Baraza la Mawaziri hawakumuunga mkono kuhusu uanzishwaji wa Tasaf, lakini sasa anaiona Tasaf kama High Point ya urais wake.

“Anasema alianzisha bima ya taifa, uhusiano wa ndani na Zanzibar ulikuwa mgumu, lakini alifanikiwa kutatua matatizo.

“Pamoja na ugumu na utata wa baadhi ya mageuzi, alisema kura zake katika uchaguzi wa mwaka 2000 ziliongezeka kwa asilimia 100 na hiyo kwake ilikuwa kama kuambiwa ‘songa mbele’.

“Pia anasimulia namna Rais wa Zanzibar wa wakati ule Salmin Amour, alipotaka kubadilisha katiba na kutaka kutawala kipindi cha tatu, lakini yeye mwenyewe na wafuasi wake waliamua yaishe.

“Anasema wakati wa utawala wake wanadipolmasia walionyesha upendeleo kwa vyama vya upinzani na kukutana nao mara kwa mara, wapo walioamini walistahili upendeleo kuliko wengine,” alisema Profesa Mukandala.

Aidha alisema Mkapa pia amesimulia namna alivyovumilia ukosoaji wa vyombo vya habari huku wakiamini kuwa ni dikteta.

“Anasema ingawa alikuwa anashikilia msimamo wake na alihitaji kuuza sera zake, ndiyo maana akaanzisha utaratibu wa kulihutubia taifa kila mwezi,” alisema Profesa Mukandala.

Alisema katika kitabu hicho, Mkapa pia anaeleza kwamba moja ya upungufu wake ni kutokuwa mwepesi kutoa pole.

“Mojawapo ya mapungufu yangu si mwepesi wa kuonyesha hisia zangu, si rahisi kutoa pole, lakini mrithi wangu Jakaya Kikwete ni mwepesi katika hili,” alisema Profesa Mukandala akinukuu sehemu ya kitabu hicho.

Pia Mkapa amesimulia namna alivyowahurumia wafungwa 100 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Aidha katika kitabu hicho, Mkapa alisema ingawa hachukii kukosolewa, lakini kukosolewa binafsi kulimwumiza sana.

Alisema madai kwamba alimpendelea baba mkwe wa mwanawe katika kubinafsisha Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira ilimuumiza sana.

Vilevile katika kitabu hicho anasimulia namna suala la EPA lilivyomuumiza na anaamini uongozi wake haukuwa wa kwanza kuruhusu ununuzi kama huo.

“Pia kuna jambo lilitokea wakati wa kumaliza muda wangu, suala la EPA, uongozi wangu haukuwa wa kwanza kuruhusu ununuzi kama huo.

“Ingawa nilisita, lakini Gavana wa BoT wakati huo, Daudi Balali alinielewesha kuwa watu hao walikuwa tayari kuchangia mfuko wa kampeni ya uchaguzi wa CCM.

“Wahuni walitumia uaminifu wangu kwa chama kunishawishi nikubali. Ninajisikia kuwa nilitumika na kusalitiwa na ukweli ni kwamba sikufaidika na kupata chochote,” alisema Mukandara akimnukuu Mkapa katika uchambuzi wake.

Pia Mkapa amezungumzia kukosolewa kuhusu anwani ya Ikulu wakati wa uongozi wake, kwamba yeye na mke wake Anna walichukua mkopo Benki ya NBC kununua nyumba.

“Ukweli ni kwamba wakati ule tulikuwa tunaishi Ikulu, tulichukua mkopo kwa masharti ya kawaida ya biashara, kabla sijaondoka Ikulu, nilimaliza malipo ya mkopo huo kwa mshahara wangu wa mwisho na mafao yangu tukapewa hati ya nyumba hiyo,” anasema Mkapa katika kitabu hicho.

Kuhusu suala la rada, alisema ilikuwa lazima inunuliwe, lakini iligubikwa na udanganyifu na hatimaye fedha zilirudishwa serikalini.

Alionyesha wasiwasi wake siku za mbeleni kwamba umasikini utaenda bega kwa bega na uvunjfu wa amani na lazima taifa wajiulize kama wanajikita katika utulivu na amani.

Aliwataka viongozi wa wakati ujao waonyeshe nia na bidii katika majukumu wanayopewa na kwamba wawe tayari kusikiliza na kutafuta walezi.

Mkapa pia ameelezea umuhimu wa mke wake Anna kuwa ndiye gundi aliyekuwa ameshikilia familia.

Anakiri kuwa yeye si mtu rahisi wa kuishi naye, lakini alikuwa mtu wa subira na uwezo mkubwa na kwamba alimvumilia kwa mengi na safari za mara kwa mara.

Sehemu ya tatu katika kitabu hicho ambayo ni ya kustaafu, Mkapa anasema amebaini marais wastaafu wanathaminiwa sana kimataifa jambo ambalo hata Mwalimu Nyerere alipata kuliona.

Anaelezea pia wasiwasi wake kukosekana kwa itikadi na fikra pevu kuhusu mustakabaIi wa taifa ambapo inahitaji mkombozi wa pili kisiasa, uchumi na kwamba anaona aibu taifa kuwa ombaomba na inahitaji kujitegemea.

Kuhusu siasa na demokrasia, anasema anaiona CCM bado inajiona kama iko kwenye siasa za chama kimoja wakati ni mfumo wa vyama vingi.

“Hivyo kunahitajika ‘more political interaction’ na ‘engagement’” alisema Profesa Mukandala akimnukuu Mkapa.

Anaendelea; “Uwepo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia.  Watu wanaingia katika siasa kusaka manufaa ya kiuchumi sio kwa nia tukufu ya kuwatumikia watu.”

Mkapa anaeleza pia umuhimu wa kuanzishwa kwa baraza dogo kama sehemu ya Bunge kupitia miswada iliyopitishwa na Bunge kabla ya utekelezaji.

 Vilevile anagusia uongozi kwamba ni kipaji au karama na sayansi pia, “unazaliwa na karama hizo lakini unajifunza pia”.  

“Kiongozi bora ni lazima awe mfano wa kuigwa katika utendaji kazi wake, uaminifu na uadilifu,” anasema.

Akisimulia wakati alipoingia madarakani mwaka 1995, anasema hali ya uchumi wa nchi ilikuwa mbaya, lakini anasema hakuogopa, “kiongozi lazima awe jasiri”, alikumbana na uzembe, kutowajibika na rushwa.

Anasema kazi kubwa ya kwanza ilikuwa kuwashawishi wahisani kuwa mambo yatabadilika.

“Nchi ilikuwa na madeni makubwa sana, deni la taifa lilikuwa dola za Marekani bilioni saba, lakini tulisamehewa dola bilioni tatu, hii ilikuwa hatua kubwa sana na ilimfurahisha Mwalimu Nyerere ambaye alishaanza kuumwa,” anasema Mkapa.

Anasema aliamini tulihitaji kujiangalia upya na kujifikiria kimkakati upya namna tulivyo kuwa tunaendesha nchi.

Mkapa anasema kuwa kuna waliona staili yake na kusema na kuelekeza kuwa ilijaa kiburi na majivuno lakini ilikuwa lazima kuonyesha kuwa hatatetereka.

Profesa Mukandala akiendelea kuchambua kitabu hicho anamnukuu Mkapa akisema; “Matokeo yake ni kwamba mapato yaliongezeka karibu mara tatu kutoka dola za Kimarekani 612,587 mwaka 1995 kufikia dola za Kimarekani 1,796,862 miaka 10 baadaye.

“Fedha za kigeni ziliongezeka kutoka uwezo wa kununua bidhaa za mwezi mmoja na nusu kufikia uwezo wa kununua bidhaa za miezi mitano na theluthi moja, riba za benki ilishuka kutoka asilimia 36 kufikia asilimia 15 mwaka 2005.

“Tukaanisha TRA (Mamlaka ya Mapato) kuimarisha ukusanyaji wa mapato Julai mwaka 1996, ukaanzishwa mfumo wa VAT Julai mwaka 1998, Public Service and Act na Public Procurement Regulatory Authority vilianzishwa mwaka 2001, Commision for Human Rights and Good Governance ilianzishwa Julai mwaka 2001, Prevention of Corruption Bureau nayo ilianzishwa.”

Profesa Mukandala anasema hayo yote yalifanya baadaye Mkapa akaitwa Mr Clean.

Mwisho katika simulizi hiyo Mkapa anamalizia kwa kusema kuwa: “Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani.”

Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongozi Institute, Profesa Joseph Semboja, alisema kuandika vitabu kuhusu maisha ya viongozi inasaidia wengi kujifunza namna bora ya kuishi, akibainisha kuwa viongozi wengi hawaandiki vitabu kutokana na kukabiliwa na mambo mengi.

“Tunapoandika historia ya kiongozi, tunaandika historia ya nchi na ndiyo maana imeshirikisha maisha ya Watanzania wengi, hili tukio si la kifamilia ila ni la taifa la Tanzania,” alisema Profesa Semboja.

Alisema kitabu hicho kilianza kuandikwa mwaka 2016 na kimechukua muda mrefu kutokana na mambo mengi ya kuhakikiwa, kukutana na watu ili kukikamilisha.

Profesa Semboja alisema kitabu hicho kimegharimu Sh milioni 230 na kinapatikana katika maduka mbalimbali ya vitabu na mitandaoni.

“Miaka 81 iliyopita siku ya Jumamosi, mkoani Mtwara alizaliwa mtoto wa kiume, leo (jana) anasherehekea siku yake ya kuzaliwa na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai.

“Ameamua kutuzawadia kitabu sehemu ya maisha kwa historia ya maisha yetu, ameamua hatachukua hata senti moja ya mauzo ya kitabu hii faida itarudi Taasisi ya Uongozi,” alisema Profesa Semboja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles