Na Mwandishi Wetu
“NAFIKIRI tunatakiwa tujitahidi kuibua wananchi wanaosoma. Ni ukweli ambao tunapaswa tuutambue, katika kuhangaika na dunia ya kisasa, watoto barani Ulaya wana bahati mbili kubwa wakilinganishwa na wa kwetu.
“Moja ni kwamba wana mazoea na vitu vinavyotumia mashine; nyingine na ambalo ni muhimu zaidi wanayo mazoea na vitabu. Kwa bahati mbaya katika jamii yetu kwamba mtu akionekana amekaa akijisomea tunamtuhumu kwamba ni mvivu au anapenda kujitenga na jamii. Tabii hii lazima tuibadilishe,” hii ilikuwa ni kauli ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa jijini Arusha Novemba 29, 1965.
Shuleni kuna watu wenye tabia ya kujisomea tu nyakati mitihani inapokaribia lakini baada ya hapo vitabu huwekwa mbali.
Takwimu za Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) zinaonesha kuwa wastani wa kujisomea miongoni mwa Waisraeli ni asilimia 64 kwa mwaka, Wajapan asilimia 40, Wamarekani asilimia 21 wakati Wafaransa ni asilimia 20. Ikilinganishwa na Watanzania ni asilimia ndogo wanaomiliki maktaba zao wenyewe, lakini kwa upande wa vijana ni kama hilo halipo.
Kujisomea si tu kwamba kuna faida kwa wasomaji kwa mkondo wa moja kwa moja, bali pia ni jambo ambalo kizazi kijacho kinatakiwa kiwe nalo.
Tabia ya kawaida ya kujisomea duniani kote inapotea hususani hivi sasa ambapo vifaa vya kielektroniki vinafanya iwe rahisi kuzipata taarifa kupitia mtandao wa intaneti.
Kutokana na hali hiyo sehemu kubwa ya Watanzania wanakosa taarifa nyingi za msingi zilizo na manufaa kiuchumi na kijamii.
Tigo na Kitabu App
Hata hivyo yamekuwapo maendeleo mapya kwani Tigo Tanzania hivi karibuni ilizindua vitabu –elektroniki (e-books).
Mfumo huu unatoa aina mbalimbali za vitabu ambapo msomaji anaweza kuarifiwa kipi akisome. Meneja wa Mawasiliano ya Tigo, Woinde Shiasel anasema kampuni hiyo itaendelea kuhakikisha kuwa utamaduni wa kujisomea unarudi. Tigo inaamini kuwa jukwaa hili litaamsha utamaduni wa kujisomea miongoni mwa wanajamii na hivyo kuurudisha utamaduni wa kujisomea ambao ulikuwa umetoweka. Hakuna shaka kwamba kila Mtanzania ataitumia simu yake ya mkononi kwa manufaa kupitia kujisomea.
“Wateja wetu wengi hivi sasa wanapenda kutumia simu za kuchati na marafiki na wanafamilia,” alibainisha Shisael na kuongeza; “Kupitia Kitabu App tunawapatia jukwaa sahihi kwa waandishi, waelekezaji na wasomaji kwa ujumla sehemu ambayo wanaweza kusoma kwa urahisi mada mbalimbali kupitia simu za mkononi.”
Kitabu App, imeingia katika soko ikiwa ni suluhisho si tu kwa wasomaji bali pia kwa waandishi ambao hivi sasa wanaweza kuuza na kufuatilia mauzo ya vitabu vyao kupitia simu zao za mkononi, kwa kutumia mtandao wa Tigo 4G LTE ambao ni mtandao mkubwa wa kasi na mpana uliounganishwa nchini.
Kuwapo kwa vitabu vinavyojieleza kwa sauti katika jukwaa hilo moja, zana hii inatarajiwa kubadilisha namna ambavyo Watanzania wanavyoipokea hali ya kujisomea dhidi ya kushuka ambako kwa kiwango kikubwa kunahusiana na utamaduni duni wa kujisomea,” anaelezea Shisael.
Akitoa maoni yake kuhusu zana hiyo, Mkurugenzi wa Jackson Group, Kelvin Twissa anasema; “Zana yetu ya Kitabu App ni ubunifu uliochochewa na mkakati, kulikohamasishwa na kukua kwa teknolojia jumuishi. Kupitia zana hii tunaruhusu waandishi kufikia viwango vya juu vya usomaji kupitia simu zao za kisasa. Wakati tuna waandishi wengi walio na vipaji katika aina tofauti za vitabu , pia kuna hitaji kubwa la uelewa kwa mapana.
“Tunaamini kwa kuingiza mada nyingi katika katalojia (Catalogue) yetu inayokua tunaweza kuleta mapinduzi katika usambazaji wa mada ndani ya nchi na hivyo kuleta hamasa ya kujisomea kwa Watanzania.”
Twissa aliongeza, “Kitabu App ni zana ya kuelimisha, kuburudisha na kuunganishwa na mada za kidini. Elimu ni moja ya mtazamo wetu wa msingi, hivyo tunajenga ushirikiano na kutoa wito kwa taasisi za kielimu kupakua mada zao, hivyo kuokoa gharama za kuchapisha na hata usambazaji wa vitabu”.
Kitabu App ni zana inayopakuliwa bure; hivi sasa na inapatikana kupitia simu za Android ambapo mtumiaji anatakiwa kulipia mada inayotakiwa na mtu binafsi.