NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM
KISWAHILI ni lugha ya Taifa la Tanzania tangu enzi za utawala wa mwasisi wa Taifa letu, hayati Mwalimu Julius Nyerere. Ni lugha ambayo kadiri miaka inavyozidi kwenda ndivyo kinavyozidi kukua na kutumika na nchi mbalimbali na kutandawaa duniani.
Hali hii ni tofauti na miaka ya nyuma, ambapo lugha pekee iliyokuwa ikipewa kipaumbele ni ya Kiingereza. Zipo lugha nyingine ambazo zimekua kwa kiasi kikubwa duniani ikiwemo Kichina. Kiswahili ni lugha ya pili kuzungumzwa Afrika baada ya Kiarabu na ya sita ulimwenguni.
Uchumi wa China umekua kwa kasi na kufanya kuongezeka kwa fursa nyingi za kiuchumi, kibiashara na kiteknolojia ambapo hali hiyo imesababisha watu wengi duniani kuanza kujifunza lugha hiyo.
Lakini pamoja na kukua kwa utandawazi duniani, Kiswahili bado hakijatendewa haki na serikali ya Tanzania kwa maana ya kukiendeleza na kukitoa hapo kilipo kwa kukipanua ili si tu kitumike katika nchi nyingi duniani, bali hata kuweza kuongeza fursa za kiuchumi na kiutamaduni kwa kuliingizia pato la kiuchumi Taifa la Tanzania, hasa linapokuja suala la kukifanya kitumike kwa marefu na mapana duniani.
Profesa wa lugha ya Kiswahili na Fasihi ya Kiafrika katika Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji ya Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aldin Mutembei, anasema Kiswahili kinaweza kunufaisha nchi yetu kwa njia kuu mbili za uingizaji mapato nchini zikiwemo njia ya mapato ya ndani na ya nje.
“Kiswahili kinaweza kutuletea mapato katika nchi yetu iwapo Serikali itaweka mfumo wa aina mbili za mapato, mojawapo ni kupitia mapato ya ndani ambapo utaratibu ungewekwa kwa wageni wanapokuja nchini kwa nia ya kufanya biashara au shughuli nyingine kwa zaidi ya miezi sita, basi iwepo kanuni au sera itakayomlazimu kupitia mafunzo ya Kiswahili kwenye vyuo au hata vituo binafsi vinavyotoa mafunzo hayo,” alisema Profesa Mutembei.
Akaongeza kuwa njia hiyo si ngeni kwani imekuwa ikitumika na nchi na tamaduni nyingine duniani kwa nia ya kukuza lugha zao na pia kuingizia mapato.
Mahitaji ya nje ya lugha na utamaduni wetu itaongeza mahitaji ya rasilimali watu, vitabu, filamu, riwaya na mazao ya sanaa zetu mbalimbali. Huo ni uchumi tosha kwa marefu na mapana.
Njia nyingine aliitaja kuwa ni kwa watalii ambao wanakuja kutembelea vivutio nchini kwetu; kuwepo na mfumo wa kuwapatia mafunzo ya lugha ya Kiswahili ili si tu wafurahie zaidi utalii wetu wakati wa kuwasiliana na wananchi wanapokuwa wakitalii, lakini pia Serikali itaweza kujipatia kipato kwa kuendesha hizo kozi fupi fupi. Kimsingi binadamu wengi wanapenda kujifunza mambo mapya likiwamo suala la lugha.
Kwa upande wa pato la nje, Profesa Mutembei alisema ni vyema balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali kuanzisha vituo vya lugha ya Kiswahili na Utamaduni ili kuweza kukitangaza zaidi nchi za nje.
Hata nchi jirani kama Rwanda, ziko tayari kuwaelimisha watu wake katika masuala ya Kiswahili baada ya kuamua kuwa ni mojawapo ya lugha rasmi nchini humo.
“Iwapo vituo hivyo vitaanzishwa, Kiswahili kitakua zaidi na pia nchi yetu itajitangaza na utalii wa nchi yetu na tamaduni zetu kwa jumla,” alisema.
Mchambuzi mwingine wa lugha ya Kiswahili, Dk. Bashiru Ally, anasema Kiswahili ni tunu na rasilimali kubwa ya utajiri wa nchi na hata ukilinganisha na rasilimali nyingine kama viwanda, mashamba hata migodi, hivyo hatuna budi kukitumia vizuri.
Kiswahili ndio chachu ya utaifa wetu na ni gundi ya umoja wetu kama Taifa. Amani yetu kama nchi imerutubishwa na lugha hii kwani hakuna wa kupinda ukweli wa mambo kwa faida za kisiasa kwa kutumia lugha.
Anasema wakati umefika Tanzania tuamke na kuachana na dhana ya kuwa wazito na waoga kwa kukitumia vizuri ili kujiinua kiuchumi. Akatolea mfano wa nchi ya Uingereza ambapo ilijikita katika kukuza lugha yake na hatimaye walifanikiwa kukua na hata kuanza kutawala nchi nyingi duniani na hivyo kukuza uchumi.
“Kumbuka Kiingereza ni kama Kisukuma chetu au Kichaga au Kinyakyusa na lugha nyingine nyingi ambacho wenzetu walikitanua na sasa wameendelea kiuchumi, ni Tanzania pekee ambapo bado tunasita kuitumia kikamilifu hazina hiyo. Hatujiamini, ifike wakati tufanye maamuzi kwa kuwa na mifumo mizuri ambayo itawezesha lugha yetu ikue kimataifa nasi tufaidike kwa fursa zilizomo kwenye lugha yetu,” alisema.
Akatolea mfano wa jinsi gani nchi za nje zinathamini lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya redio kwa njia ya Kiswahili, jambo ambalo ni chachu kwa Tanzania kukikuza zaidi kimataifa.
Aidha, Dk. Bashiru alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuanza kuonyesha njia ambapo amekuwa akitoa hotuba zake kwa Kiswahili na kushauri atilie mkazo zaidi.
“Rais wetu amejaribu kuonyesha mfano lakini bado haitoshi, atoe tamko rasmi na litatekelezwa kama alivyofanya kwenye kuhamishia makao makuu mjini Dodoma, ni jambo linalowezekana kabisa,” alisisitiza Dk. Bashiru.
Mchambuzi wa lugha ya Kiswahili nchini, Majid Mswahili ambaye ni Mchambuzi wa lugha, fasihi na falsafa ya Kiswahili na pia Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kiswahili Development Ltd, aliliambia MTANZANIA kuwa lugha ya Kiswahili ilianzishwa kwa nia nzuri na kwamba jitihada mbalimbali zimefanywa na Serikali tangu Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Muasisi wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini ni lazima sasa kiendelezwe na kupanuliwa zaidi ili kiweze kuwa si tu lugha ya mawasiliano lakini pia kuingizia pato nchini. Fursa ziko nyingi kwenye lugha.
“Sasa hivi tunachotakiwa ni kukiendeleza kwa kufanya jitihada zaidi zikiwemo kufanya tafsiri kwenye lugha nyingine, kukalimani, kuwafundisha wageni wanaokuja nchini na pia kukifanya Kiswahili kuwa kama bidhaa hasa kupitia balozi zetu zilizoko nchi za nje,” alisema.
Anasema nchini Tanzania mwanafunzi mmoja wa kigeni hutozwa kati ya Dola za Marekani 15 hadi 30 kwa dakika 60 kwa siku ambapo kwa nchi kama Marekani, wanafunzi wa Kiswahili hutozwa hadi Dola za Marekani 70 kwa dakika 60.
Akifafanua juu ya nini kifanyike ili kuharakisha upanuzi wa lugha hiyo, Majid alisema sera ya lugha ya Kiswahili ni lazima iundwe badala ya ilivyo sasa ambapo ipo ya utamaduni tu. Sera itaibua mambo mengi na haswa kuongeza mahitaji ya Lugha ya Kiswahili.
“Vilevile Watanzania umefika wakati sisi wenyewe kupenda na kujivunia lugha yetu badala ya kuiponda na kuiga lugha za nje,” alisema.
Kuhusu suala la sera, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliyepita, Nape Nnauye, alisema Serikali imeona mapungufu hayo na iko mbioni kutengeneza sera ya lugha hiyo na nyinginezo ili ziwe chachu ya maendeleo.
Naye Waziri Dk. Harrison Mwakyembe ameazimia kuendeleza msimamo huo wa kutengeneza sera.
Mswahili anasema vilevile ili umma uweze kuhamasika zaidi na kukipa Kiswahili umuhimu, ipo haja kwa kila chombo cha habari na kila wizara kuwa na kitengo kitakachuhusika na lugha ya Kiswahili ili kuhakikisha lugha inatumika ipasavyo na kwa usahihi. Ikiwezekana uanzishwe mpango wa kupeana zawadi kwa wale wanaofanya vizuri na haswa katika vyeti vya mitihani mbalimbali.
Aidha, alimshukuru Rais wa Awamu ya tano, Dk John Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya lugha hiyo, hali ambayo alisema imewatia moyo wadau mbalimbali na kuwapa hamasa zaidi ya kuelimisha umma juu ya umuhimu wa lugha kwa Tanzania.
Miezi miwili liyopita kulifanyika mkutano wa wadau wa sekta ya utamaduni na lugha ya Kiswahili jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa wakati huo, Nape Mnauye, alisema Serikali imepanga kuanzisha sera ya lugha ya Kiswahili ili kusaidia ukuaji wa lugha hiyo ndani na nje ya nchi ili kukikuza zaidi.
“Kwa sasa hakuna sera ya lugha ya Kiswahili badala yake ipo sera ya utamaduni pekee, ndiyo maana ili kukifanya Kiswahili kikue tumeamua kutengeneza sera ya Kiswahili iwe inajitegemea, hali ambayo itasaidia kukua kwa lugha yetu,” alisema.
Akaongeza kuwa sera hiyo mpya itakuwa ni kama mlinzi na mbolea ya lugha ya Kiswahili na kwamba itaongoza na kusimamia kikamilifu makuzi ya lugha hiyo.
Alizitaja baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha makuzi ya lugha ya Kiswahili, kuwa ni pamoja na ufinyu wa rasilimali na utashi mdogo uliopo miongoni mwa watu wanaofanya maamuzi hasa Wizara ya Elimu.
Biashara ya Sanaa
Biashara ya sanaa ikiwamo muziki, filamu, vitabu na riwaya inaonekana kukua kwa kasi na kuwa ya pili kwa kuleta mapato kwa Taifa. Ikumbukwe na kueleweka kuwa kwa kiasi kikubwa sanaa hutumia na kubebwa na lugha ya Kiswahili.
Bunge la Afrika ya Mashariki (EALA) imetambua mchango mkubwa wa sanaa katika uchumi wa nchi za eneo hili na kupongeza matumizi chanya ya lugha hiyo.
Kenya imekuwa mbele kwa kuingiza lugha hii kwenye Tehama na inafanya juhudi kuziba mchango wa Tanzania usionekane na kuhodhi historia na mwenendo wa Kiswahili na hivyo kufifisisha maendeleo ya asili ya lugha yenyewe.