29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

KISHINDO IPTL

Na Patricia Kimelemeta

-DAR ES SALAAM

KUBWA lao limeibuka. Ndivyo unaweza kusema baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuwaburuza mahakamani, Mwenyekiti wa Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Limited/PAP, Habinder Seth Sigh  na mwenzake wa Kampuni ya VIP Engenering na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL,  James Rugemalira.

Vinara hao   walifikishwa   katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu   Dar es Salaam jana na kusomewa mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababisha  serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60  (Sh bilioni 309.5).

Washtakiwa hao wote walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Washtakiwa   walirudishwa rumande hadi Julai 3, mwaka huu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza wala kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.

Inadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18 , mwaka 2011 na Machi 19 , 2014   Dar es Salaam, watuhumiwa walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Imedaiwa kuwa katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18,  mwaka 2011na Machi 19, 2014   Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma na wakisaidiana na watumishi wa umma, walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la nne mtuhumiwa Sethi anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua si kweli.

Seth anadaiwa kutoa nyaraka hiyo ya usajili wa Kampuni kwa Ofisa Msajili wa Makampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka jingine, washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi Tawi St. Joseph kwa ulaghai, walijipatia kutoka Benji Kuu ya Tanzania  (BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60  (zaidi ya Sh bilioni 309.5).

Ilidaiwa   kuwa katika shtaka la kusababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa  Novemba 29, mwaka 2013 katika Benki ya Stanbic Tawi la  Kinondoni, kwa vitendo vyao, waliisababishia Serikali hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh bilioni 309.5.

Baada ya kumaliza kusomewa mashtaka yao, Wakili wa utetezi,  Respicius Didas kwa niaba ya mawakili wenzao, aliomba mahakama iwapatie wateja wao dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.

Upande wa mashtaka ulipinga vikali hoja hizo na kuiomba mahakama kutupilia mbali maombi ya utetezi ya kuwapatia dhamana washtakiwa hao.

Akiwasilisha hoja zake, Wakili Kadushi alisema mahakama ya Kisutu haina mamlaka si tu ya kutoa dhamana, bali hata kusikiliza maombi ya dhamana.

Alisema mahakama pekee yenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mahakama Kuu na ndiyo maana washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote wakati wakisomewa mashtaka yao.

Wakili huyo wa Serikali alisema mazingira pekee ambayo yangeifanya Mahakama ya Kisutu iweze kusikiliza maombi hayo na kesi kwa ujumla ni pale ambako Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) angetoa cheti maalum cha kuipa mamlaka Mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.

“Maombi ya dhamana yameletwa katika mahakama isiyoweza kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria,” alisema Kadushi.

Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisisitiza na kuiomba mahakama kutupilia mbali hoja zote za maombi ya dhamana zilizotolewa na upande wa utetezi na ijielekeze kwa jinsi inavyoona inafaa, washtakiwa waende mahabusu wakati wakisubiri taratibu za kesi zinazoendelea.

Akijibu hoja hizo, Hakimu Shaidi alisema sheria inaelekeza kwamba kesi za uhujumu uchumi zinazozidi Sh milioni 10 Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza wala kutoa dhamana isipokuwa kwa cheti maalumu kutoka kwa Mwendesha Mashataka wa Serikali (DPP),  kinachoiwezesha mahakama kufanya hivyo.

Kesi hiyo itatajwa tena Julai 3 mwaka huu na watuhumiwa wote wamepelekwa mahabusu.

 Sethi alivyodakwa uwanja wa ndege

Jumamosi   Juni 17, mwaka huu saa 9.00 mchana wakati Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL/PAP,  Habinder Seth Sigh akiwa na mkewe Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  Dar es Salaam,   alikamatwa   wakiwa safarini kwenda   Afrika Kusini ambako ndiko yaliko makazi yao.

Wakiwa katika eneo watu mashuhuri (VIP) uwanjani hapo  wakihakikiwa nyaraka zao, ghafla maofisa wa Serikali wakiwamo wa Takukuru, waliwazuia na kuchukua hati zao za kusafiria huku wakimtia mbaroni Sethi.

Baada ya tukio hilo maofisa hao walimtaka mke wa Sethi kuendelea na safari lakini kutokana na   kukamatwa mumewe   naye aliamua  kuahirisha safari na kurejea katika nyumba yao   iliyopo Masaki huku akilazimika kuwaita viongozi wa juu wa IPTL na kuwaeleza mkasa uliompata mume wake huku wakishindwa kujua alikopelekwa.

“Haikuwa kazi nyepesi vikao vilifanyika hadi Jumapili usiku wa manane huku kila mtu akiwa na taarifa zake wakiwa hawajui alipo Sethi.

“Hata hivyo jana (Jumatatu) wakiwa kwenye harakati za kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ndipo walipopata taarifa za kufikishwa kortini kwa mmiliki huyo wa IPTL,” alisema.

TAKUKURU

Jana asubuhi Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola alisema watuhumiwa hao wawili  wamewafikisha mahakamani   kwa tuhuma za uhujumu uchumi   na mashitaka yanayofanana na hayo.

“Kwa muda mrefu nimekuwa nikiulizwa kuhusu kesi za Escrow na IPTL zimeishia wapi. Kama tulivyosema awali kwamba Takukuru ina jukumu la kimsingi la kupambana na rushwa na makosa ya ufisadi.

“Kwa hiyo katika mwendelezo wa majukumu yetu tulichunguza shauri hili kwa muda mrefu na ikafika wakati mwafaka wa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa hawa wawili, James Rugemalira na Harbinder Singh Sethi.

“Nitoe wito kwa wananchi kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kupambana na vitendo vya uhujumu uchumi wa nchi hii ili wananchi wetu wapate maisha bora zaidi,” alisema.

IPTL

Makubaliano kati ya Serikali na Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha MW100 katika miaka 1990 ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa umeme uliokuwepo.

Serikali ilialika sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji umeme kwa vile haikuwa na fedha za kugharimia miradi ya umeme.

Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania (VIP) chini ya Rugemalira iliweza kuishawishi Serikali kualika Kampuni ya Mechmar Corporation ya Malasyia (MECHMAR) baada ya kampuni hiyo kuonesha kuwa inaweza kuzalisha kiwango hicho cha umeme katika Jiji la Dar es Salaam na kusaini makubaliano (MoU) na Serikali.

Mwaka 1994 Kampuni ya MECHMAR na Kampuni ya VIP kwa pamoja zilianzisha Kampuni ya IPTL, kama kampuni binafsi iliyokuwa inamilikiwa na MECHMAR kwa asilimia 70 na VIP kwa asilimia 30.

Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga-kumiliki na-kuendesha mtambo wa kuzalisha MW 100 za umeme wa mafuta mazito katika eneo la Tegeta-Salasala.

AKAUNTI YA ESCROW

Akaunti hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na Kampuni ya IPTL kuhusu kiwango kinachopasa wa kulipwa na baadaye suala hilo kupelekwa mahakamani.

Fedha hizo zilitakiwa zitolewe baada ya mahakama kutoa uamuzi wa mgogoro huo lakini zilitolewa na kulipwa kwa mmiliki mpya wa Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP) na kusababisha kuibuka kwa kashfa hiyo.

Jumla ya Sh bilioni 321 ziliwekwa kwenye akaunti ya Tanesco kusubiri suluhisho la kesi yake na IPTL.

RUGEMALIRA, SETHI

Siku chache baada kuibuliwa   kashfa hiyo, Mwenyekiti wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira alisema kati ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo, alilipwa mgao wake wa asilimia 30 hisa zake (Dola za Marekani milioni 75  sawa na Sh bilioni 120 za Tanzania ) ambazo aliziita ‘vijipesa vya ugoro’.

Fedha nyingine zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ya Escrow zilikwenda kwa Harbinder Sigh Seth, ambaye ni mmiliki mpya wa IPTL kupitia kampuni yake ya Pan African Power Tanzania Limited (PAP) kwa kile kilichoitwa ‘amri ya mahakama’.

ESCROW ILIVYOWANG’OA VIGOGO

Kashfa ya Escrow iliwang’oa vigogo kadhaa wa Serikali.

Desemba 16, mwaka 2014, Jaji Werema alitangaza kujiuzulu na kusema kuwa amejiuzulu kwa sababu ushauri wake kuhusiana na suala ya Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka na umechafua hali ya hewa.

Aidha Desemba 22, 2014 wakati akiwahutubia wazee wa Dar es Salaam, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alimfukuza kazi hadharani, aliyekuwa Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

‘Tumemuuliza Tibaijuka fedha hizo nyingi amezipata vipi, akatujibu kwamba ni kwa ajili ya kuendesha shule. Sisi hatukuwa na tatizo kwa nini shule imepewa fedha tatizo lilikua kwa nini fedha zimeingia kwenye akaunti yake badala ya akaunti ya shule? alitujibu kuwa hayo ndiyo masharti aliyopewa na Rugemalira.

“Tukaona kwamba hapa kuna mapungufu, tukakubaliana na tukamwomba atuachie nafasi ili tumteue waziri mwingine,” alisema Rais Kikwete.

Desemba 23, 2014 aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yake.

Januari 24, 2015 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alijiuzulu na kusema kuwa alifanya hivyo ili kuzima mjadala huo aliodai kuwa ulikuwa ukimsubiri yeye ajiuzulu.

KAFULILA, WEREMA

Juni 2014, aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, aliwahi kuomba mwongozo bungeni kuhusu uchotwaji wa fedha hizo ulivyofanyika katika Akauti ya Tegeta Escrow.

Hatua hiyo ilisababisha Kafulila na Jaji Werema kutoleana maneno ya kashfa hadharani ambapo Werema alimfananisha Kafulila na tumbili huku yeye akimwita mwizi.

Werema alitumia maneno ya kabila la Wanyankole, aliosema kuwa wana usemi unaosema kwamba ‘Tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni’.

“Naomba nisikilize, hata kama ni mtuhumiwa, nina fursa ya kusikilizwa, nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.

Kafulila naye alisimama na kumwambia Werema atangaze masilahi yake. Huku akisema, “Wewe (Werema) ni mwizi tu.

IPTL ILIVYOMSHTAKI KAFULILA

Baadaye Kampuni ya IPTL ilimfungulia kesi ya madai Kafulila kwa kuichafua kutoa taarifa za uongo kwa umma, huku ikimdai fidia ya Sh bilioni 310.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Dar es Salaam ilitupilia mbali kesi hiyo namba 301 ambayo ilifunguliwa na IPTL, PAP na VIP.

Katika kesi hiyo, Jaji Rosemary Temba alisema Mahakama Kuu imejiridhisha kwamba Kampuni ya IPTL, PAP na VIP hawakuwa na hoja za msingi kuthibitisha madai yao.

MAAZIMIO YA BUNGE

Kutokana na kashfa ya Escrow, Bunge lilipitisha maazimio nane huku likiitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine kuwachukulia hatua stahiki mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Seth na wengine.

Pia Bunge liliazimia Serikali kuangalia uwezekano wa kuichukua mitambo ya kampuni hiyo na kuimilikisha kwa Tanesco kwa mujibu wa sheria za nchi.

Bunge liliazimia kupitiwa upya mikataba ya umeme na Serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Takukuru kwa ajili ya kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulika kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa.

Katika azimio la tano, Bunge lilimtaka Rais kuunda tume ya kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji waliotuhumiwa.

Azimio la sita, lilitaka mamlaka husika za fedha na za uchunguzi kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine yoyote itakayogundulika kutokana na uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.

Azimio la saba, Bunge lilitaka mawaziri, mwanasheria mkuu wa Serikali na katibu mkuu na Bodi ya Tanesco kuwajibishwa kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi huo, jambo ambalo lilikwishafanyika.

Katika azimio la nane na la mwisho, Bunge liliitaka kamati husika za kudumu za Bunge kuchukua hatua za haraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles