29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KISA CHA MWANAMKE ALIYEPITIA MACHUNGU YA NDOA

* Mume alimwagia tindikali na kuoza miguu


Na MALIMA LUBASHA -SERENGETI

WAKATI mwingine ugumu wa maisha ya ndoa huwafanya wanawake kujuta kuolewa.

Majuto haya yamempata Kadogo Isaya (37), baada ya kufanyiwa ukatili na mume wake Daud Isaya.

Kadogo ambaye aliolewa uke wenza na mume wake huyo, anasema amejikuta akipata ulemavu wa kudumu baada ya kumwagiwa tindikali na mumewe chanzo kikiwa ni wivu wa mapenzi.

Baada ya tukio hilo

alilazwa katika Haspitali Teule ya Wilaya ya Serengeti ya Nyerere DDH, mkoani Mara, kwa miaka minne mfululizo.

 Anasema kuwa aliuguza majeraha ya kumwagiwa tindikali miguu yote miwili iliyofanya nyama kunyofoka na kubakia mifupa.

Akisimulia kisa hicho kwa masikitiko, Kadogo anasema anajuta kuolewa na Daud kwani hakuwahi kufikiria kama siku moja atakuwa mlemavu.

“Sikutegemea kama ipo siku nitakuwa nikitembea kwa masaada wa magongo, baiskeli ya miguu mitatu au kujivuta chini…

“Ndoa ni jambo gumu ambalo linaweza kujenga au kuharibu maisha ya mtu, uvumilivu na uaminifu katika ndoa ni jambo la msingi mno, bila kuaminiana mnaweza mkajikuta mkitendeana ndivyo sivyo, kama yaliyonikuta mimi,” anasema Kadogo.

Dada huyu ambaye ni mkazi wa Mugumu Mjini, wilayani Serengeti anaonekana kukata tamaa ya maisha kutokana na changamoto anazokumbana nazo sasa.

Anasema tangu apate ulemavu, suala la kula, malazi na kusomesha imekuwa ni shida.

Kadogo anasema kabla ya kuolewa alikuwa akitembea kwa miguu yake kama watu wengine, lakini sasa ndoa imebadili maisha yake na kumfanya kuwa ombaomba kwa kuwa hana uwezo wa kufanya kazi kama zamani.

Anasema anajuta kuolewa na mwanamume ambaye hajui thamani ya mwanamke…

“Sijui kama na wanawake wenzangu walioolewa wanapitia changamoto hizi… sikuwahi kufikiria kama mume wangu anaweza kuwa na roho ya kikatili kiasi hiki,” anasema.

Kadogo anaikumbuka siku ya Agosti 4, mwaka 2000 majira ya usiku ilivyobadili mwelekeo wa maisha yake.

“Nilikuwa bado kijana mdogo mwenye miaka 21 nikiwa na mtoto wa mwaka mmoja.

“Mume wangu aliniadhibu kwa kipigo na kunimwagia tindikali miguuni, akidai nimechelewa kurudi nyumbani,” anaeleza jinsi ilivyokuwa.

 

Anasema siku ya tukio nyumbani kwake kulikuwa hakuna mboga hivyo, kwa kuwa alikuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza ndizi mbivu, alikwenda Mugumu mjini kufanya biashara ili aweze kununua chakula cha nyumbani.

Mumewe alitaka mkewe arudi nyumbani kabla ya jua kuzama, lakini alijikuta akitembeza ndizi mbivu alizokuwa akiuza hadi ilipotimu saa 11 jioni na kuanza safari ya kurudi nyumbani licha ya kwamba hazikuisha.

Anasema kwa bahati mbaya alichelewa kufika nyumbani hivyo, mumewe alikasirika na kuanza kumpiga.

“Aliniamuru niingine ndani na na nivue nguo zote, kisha akanifunga kamba miguuni na kunining’iniza kichwa chini miguu juu kwa kufunga kamba ya miguuni kwenye dari.

 

“Akaanza kunilazimisha nimwambie huko Mugumu nilikua na mwanamume gani aliyenifanya nichelewe kurudi nyumbani.

“Ndani alikuwa na rundo la fimbo ambazo alizikata nikiwa kwenye biashara zangu akinisubiri nirudi aanze kuniadhibu… alizificha sehemu ambayo si rahisi kuziona,” anasimulia Kadogo na kuongeza;

“Alienda kuzichukua na kuanza kunichapa huku nikiwa naning’inia darini.

Anasema kuwa baada ya hapo ndipo akamwagia tindikali miguuni.

Kadogo anasema kuwa wakati hayo yanaendelea aliogopa kupiga kelele kwani angeweza kumuua.

“Nilikuwa nalia kimya kimya huku nikimuomba Mungu anisaidie nisikatwe na sime aliyokuwa ameifunga kuinoni,” anasema Kadogo.

Anasema baada ya mumewe kumaliza kumfanyia ukatili huo, alimfungua kamba na kumpiga marufuku kutoka nje.

Kadogo anasema mumewe hakutaka hata aende hospitali kwa ajili ya kupata matibabu.

“Nilikaa ndani siku nane nikiuguza majeraha bila majirani kujua kinachoendelea.

“Watu walishtushwa na ukimya wangu baada ya kuona hawanioni nikitoka nje, wakaanza kuniulizia, wakimuuliza mume wangu anakosa majibu ya kuwapa hivyo wakaanza kuingiwa na wasiwasi.

“Ikawalazimu kwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji, Chacha Baru ambaye alikuja nyumbani na kunikuta nikiuguza majeraha ndani,” anasema.

Anasema kuwa baada ya ukatili huo kubainika, wakati wanakwenda hospitali mwenyekiti alimlazimisha kwenda Kituo cha Polisi Mugumu kutoa taarifa na kupewa fomu ya PF 3 kwa ajili ya kumuwezesha kupata matibabu.

Alipofika hospitalini alipewa kitanda huku akiuguzwa na mama yake Elizabeth Gibayi.

Anasema madaktari walimshauri kuwa ili kuokoa  maisha yake ni lazima akatwe miguu yote miwili kwa kuwa iliharibika na nyama zilioza huku zikinyofoka baada ya kucheleweshwa kufika  hospitali.

 “Nilimsikia Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere, wakati huo alikuwa Dk. Noel Makuza akimwambia mama ili kuniokoa lazima miguu yangu yote ikatwe. Hata hivyo, madaktari hawakutekeleza agizo hilo badala yake waliendelea kunitibu kwa kuondoa sumu iliyokuwa inazidi kunyofoa nyama za miguu yangu.

“Lakini nyayo za miguu zilikatika zenyewe na kubaki  mifupa… namshukuru Mungu, madaktari na wauguzi  wa hospitali hiyo kwa kunisaidia kadri ya uwezo wao kuhakikisha napona,” anasema.

Anasema alitoka hospitali Desemba mwaka 2003 na kurudi nyumbani kuanza maisha upya.

“Sikwenda kwa mume wangu kwa kuwa familia ilishasambaratika, mama mkwe wake ambaye walikuwa wakiishi pamoja alikimbia na kutokomea kusikojulikana akiogopo kukamatwa.

Akizungumzia hulka za mumewe wa kwanza anasema alikuwa ni mtu ambaye anapenda kupiga na kwamba hata mke mwenzake aliamua kukimbia baada ya kuona kipigo kimezidi ndani ya ndoa.

Anasema hakuwahi kumchukia mumewe kwa kuwa alijua kuwa ndio Mungu aliyempangia.

“Katika ndoa yangu sikuwahi kumsaliti mume wangu. Ndani ya miaka miwili ya ndoa niliyoishi nilikuwa mwaminifu na mnyenyekevu kwa mume wangu.

Kadogo ambaye kwa sasa anaishi Mugumu Mjini, licha ya ulemavu alionao na changamoto za ndoa alizokabiliana nazo ameweza kuzaa watoto sita na mwanamume mwingine na hivyo kujikuta akiishi maisha magumu hasa ukizingatia kuwa ni mlemavu hawezi kutafuta  kama ilivyokuwa awali.

Anasema aliamua kuishi na mwanamume mwingine, Juma Nicholus akidhani kuwa atamsaidia katika maisha kumbe sivyo.

“Nimeishia kuzaa bila mpangilio na sasa nina watoto sita ambao siwamudu kuwalisha wala kuwasomesha,” anasema na kuongeza kuwa katika kuhangaika alilazimika kuanza biashara ya pombe haramu ya gongo ambayo ilimsababishia kukamatwa mara kwa mara na polisi.

Anasema alishawahi kufikishwa mahakamani kwa kuuza gongo na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.

Anasema adhabu hiyo ilimlazimu mtoto wake mkubwa Neema Isaya (18) kuacha shule akiwa kidato cha pili na kurudi nyumbani kulea wadogo zake.

“Hadi sasa maisha yangu ni magumu nalala chini, wakati wa mvua nyumba inavuja na watoto wote sita naishi nao katika chumba kimoja kidogo… nawatandikia sandarusi huku mwisho wa mwezi nikitakiwa kulipa kodi ya Sh 10,000.

“Sina pa kukimbilia  kwani mama yangu ambaye naye alikuwa ni tegemeo langu alishafariki dunia.

“Naomba msaada kwa Watanzania wanisaidie kusomesha, kupata malazi kwani familia niliyonayo ni kubwa hivyo inanishinda,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles