29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KISA CHA MAJI TANGA KUWA YA KAHAWIA

Mwonekano wa bwawa la Mabayani ambalo hutumika kusambaza maji kwa wakazi wa Jiji la Tanga.

 

 

Na Sussan Uhinga, TANGA 

SIKU za hivi karibuni, kuliibuka mjadala katika mitandao ya kijamii kuhusu ubora wa maji jijini Tanga.

Mjadala huo ulitokana na picha iliyokuwa ikizunguka ikionesha mto uliokuwa na maji yenye rangi ya kahawia, watu wakidai kuwa ndiyo yanayotumiwa na wakazi wa jiji hilo.

Hali hiyo imesababisha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga UWASA), kukanusha habari hizo.

Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Joshua Mgeyekwa aliwataka wakazi wa jiji hilo kupuuza picha zinazozunguka katika mitandao akisema zina lengo la kukuza ukubwa wa tatizo na kuharibu sifa ya mamlaka.

Hata hivyo alikiri kuwapo kwa tatizo la maji, kwani watu wanapata maji wasiyoyazoea – yenye rangi isiyokuwa ya kawaida hivyo kuibua sintofahamu kwa watumiaji.

Mhandisi Mgeyekwa anasema wanajitahidi kuhakikisha maji yanabaki salama, hivyo wamepunguza kiasi cha maji yanayozalishwa kwa siku, hali ambayo imelazimu kuweka mgawo kwa watumiaji.

Naye Mratibu wa shughuli za mazingira Tanga UWASA,  Ramadhan Nyambukah anazungumzia mto Zigi na Muzi akisema inaanzia katika safu ya milima ya Tao la Mashariki hususan milima ya Usambara Mashariki.

Akizungumzia eneo la Mowe ambapo ndipo kwenye kituo cha kusafisha maji, Nyambukah alisema ndiyo sehemu ambayo maji hutibiwa.

Anasema eneo hilo hutumika kusafisha maji yanayosambazwa katika Jiji la Tanga na kuwekwa dawa kwa lengo la kuyatibu. Akizungumzia maji yaliyokuwapo katika bwawa la Mabayani, ambayo hayakuwa katika hali nzuri, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uzalishaji Maji, Faraji Nyoni anasema wamekuwa wakipokea maji yenye tope jingi hivyo hujikuta wakiongeza gharama ya uzalishaji.

Anasema ni kawaida kwa maji hayo kuwa machafu na kwamba huwa na tope lenye kiwango kisichozidi 10NTU kwa wakati wa kiangazi na 180NTU wakati wa masika.

Anasema mwaka huu imekuwa tofauti kwani kiwango cha tope kimekuwa ni zaidi ya 1000NTU ambacho huingia katika mitambo ya kusafishia maji na hivyo kusababisha ugumu wa kuyatibu.

Anasema hali hiyo inatokana na athari ya uchafuzi wa mazingira katika vyanzo vya maji.

“Kwa zaidi ya muongo mmoja sasa tangu chembechembe za dhahabu zigunduliwe katika safu ya milima ya Usambara Mashariki, kumekuwapo harakati nyingi za uchimbaji haramu wa madini hayo.

“Licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali, bado kuna uharibifu mkubwa wa sehemu oevu katika tengamaji la Zigi. Kibaya zaidi uchimbaji unafanyika katika mito na kubomoa kabisa njia za maji hivyo kusababisha tope kujaa katika maji hasa kipindi cha mvua,” anasema.

Nyambukah anasema ongezeko la shughuli za kibinadamu, uchimbaji madini haramu, ukataji miti na kilimo kisichozingatia taratibu, ni moja ya sababu za uchafuzi mkubwa wa maji.

Mtaalamu huyo wa mifumo simamizi ya ubora (Quality Management System), anasema tafiti zilizofanyika katika bwawa la Mabayani zinaonesha kuwa ukubwa wa bwawa unapungua. Moja ya tafiti iliyofanywa na Kampuni ya Kimisri ACE Consulting Engineers Moharram Bakhoum, mwaka 2010 ulibaini kuwa kina cha bwawa kimepungua kwa asilimia 38 kutoka wastani wa mita 8.7 hadi kufikia mita 5.4.

Hata hivyo, licha ya kupungua kwa kina cha bwawa kutokana na kutuama kwa udongo, shughuli za kibinadamu zimeongeza virutubisho kwa mmea wa magugumaji ambayo yamefunika eneo kubwa la bwawa.

Anasema magugu maji ambayo kitaalamu huitwa 'eichhornia crassipes' au 'Water Hyacinth' huleta athari kubwa za kimazingira ikiwa ni pamoja na kusababisha utando mkubwa katika maji na kuzuia kupenya kwa mionzi ya jua na hewa ya oksijeni chini ya maji.

Pia huzuia upatikanaji wa viumbehai wengine katika eneo hilo, ikiwamo kupunguza uwezo wa samaki kuzaliana.

Katika Mto Muzi kuna mashimo makubwa yayonasababisha mmommonyoko wa kingo za mto na kuingiza udongo mwekundu katika maji.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia maji Zigi Juu (JUWAMAZIJU)  Philip Mdoe anasema hali hiyo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na jamii na wakati mwingine ni ndugu wa damu wa viongozi hivyo wanashindwa kuchukulia hatua zinazostahili.

“Mahandaki yamekuwa makubwa na uongozi wa vijiji hauchukui hatua zozote kukabiliana na jambo hili, wanatupiana lawama tu.

“Ukiuliza Kwamtili wanakwambia waharibifu wanatokea Kambai na ukienda Kambai wanasema waharibifu wanatokea Kwamtili, lakini wachimbaji ni watoto wetu tunao kaa nao humu humu,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Kwamtili, anasema walishapiga marufuku shughuli za uchimbaji.

Mmoja wa wakazi jijini Tanga, anasema anakerwa na uchimbaji holela kwenye vyanzo vya maji katika milima ya Usambara.

“Ili kukomesha shughuli hizi eneo hili linapaswa likabidhiwe kwa jeshi na waweke kambi kabisa ili kulinda vyanzo hivi visitoweke,” anasema mama huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Wambera.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Kwamtili, James Zakaria anasema sasa hivi wamedhibiti uharibifu wa mazingira.

Mama Kijazi ni Mhifadhi wa Hifadhi ya asili ya Amani ambaye ni mwathirika mkubwa wa uchimbaji wa madini hasa katika maeneo yaliyo ndani ya hifadhi. Mama Kijazi anasema sheria zilizopo haziwaadabishi waharibifu wa mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles