Kirigini asema JPM si mbinafsi kukataa kuongeza muda madarakani

0
874

Na Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAM

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa, Paul Kirigini amempongeza Rais John Magufuli kwa kuwa mtiifu wa Katiba ya nchi kwa uamuzi wake kutoongeza muda wa kukaa madarakani.

Kirigini ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Rais Magufuli kusisitiza kwa mara nyingine atafuata Katiba kwa kuondoka madarakani muda wake kwa mujibu wa katiba ukimalizika.

Akizungumzia suala hilo Kirigini amesema Rais Magufuli amekuwa rais bora anayefuata Katiba kutokana na msimamo wake huo tofauti na marais wengine Afrika na duniani ambao wamekuwa na uchu wa madaraka kwa kujiongezea muda wa uongozi.

“Rais wetu ameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa, hili ni funzo kubwa kwamba Katiba ya nchi siyo kitu kidogo inapaswa kuheshimiwa   kwa kuwa ameapa kuilinda. Kwa hili rais wetu anastahili pongezi.

“Wengi ni mashahidi tumeshuhudia marais wengi wakiwamo wa nchi jirani ambao wamebatilisha Katiba za nchi zao ili wapate uhalali wa kuendelea kutawala.

“Hii ndiyo aina ya kiongozi ambaye Tanzania inamuhitaji, Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa katika kipindi chake cha uongozi, tumeshuhudia ununuzi wa ndege, miundombinu ambapo barabara hadi zile zikizokuwa korofi za vijini zikijengwa kwa kiwango cha lami, madaraja, elimu bure na huduma nyingi za kijamii ambazo zimerahisishwa, kwa kweli anastahili pongezi,” amesema Kirigini.

Pamoja na mambo mengine, Kirigini amesema Rais Magufuli si mbinafsi ndiyo sababu kutokana na utendaji kazi na kuheshimu Katiba baadhi ya nchi duniani zimekuwa zikimshangaa kwa kukataa kuongeza muda wa uongozi licha ya wananchi kumtaka kufanya hivyo.

Baadhi ya viongozi  na wanachama wa CCM wamekuwa wakimtaka Rais Magufuli aongeze muda wa kukaa madarakani wakihofia maendeleo aliyoyaanzisha kukwama.

Hata hivyo, Rais Magufuli amekuwa akikataa kufanya hivyo na alionyesha kutofurahishwa na mjadala huo huku akimtaka Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kuwaambia wanachama wa CCM na Watanzania kuachana na fikra hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here