Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Zaidi ya tani 2,000 za mkaa mbadala zinatarajiwa kuzalishwa kila siku na Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni ili kunusuru uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti.
Kuzalishwa kwa mkaa huo ni matokeo ya mradi ujulikanao kama ‘Taka ni Mali’ unaotekelezwa na Shirika la Afya la Amref ambalo limekuwa likitoa mafunzo kwa vikundi mbalimbali vya kijamii vikiwemo vituo vya taarifa na maarifa ambavyo viko chini ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Akizungumza wakati wa kukitambulisha kiwanda cha kutengeneza mkaa huo Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Biashagazi, amesema walipata mafunzo yaliyotolewa na Amref kupitia TGNP.
“Baada ya kupata mafunzo tulianza kutengeneza mkaa na tulikuwa tunaonyesha kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, watu wa Amref wamekuwa wakiona jitihada zetu kwahiyo utendaji wetu wa kazi ndiyo umefanya tupate huu mradi,” amesema Bishagazi.
Aidha amesema walifanikiwa pia kuwafundisha watu wengine 800 kutoka vikundi mbalimbali katika Kata za Majohe, Kivule, Chanika, Ubungo, Kimara, Kisarawe na Mbeya.
Mkurugenzi huyo amesema kwa kuanzia kiwanda hicho kitatoa ajira kwa watu 30 wakiwemo vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya na kwamba wateja wakubwa wa mkaa huo watakuwa ni wanajamii.
Naye Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) Mkoa wa Dar es Salaam, Ridhiwani Makange, amekipongeza kikundi hicho na kukikabidhi cheti cha utambuzi huku akiahidi kuendelea kukilea ili kuhakikisha kinatimiza malengo yake.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kikundi hicho kinaunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira sambamba na kampeni ya kusafisha Jiji la Dar es Salaam ijulikanayo kama ‘Safisha Pendezesha Dar es Salaam’.
Kumbilamoto pia ameahidi kutoa vyerehani, luninga na feni kwa vijana wanaojifunza ushonaji ambao ni moja ya mradi unaondeshwa na Sauti ya Jamii Kipunguni.
Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Liundi, amesema kuna vituo vya taarifa na maarifa 70 hapa nchini ambavyo vimeweza kuwafikia zaidi ya watu milioni 5 na kwamba Sauti ya Jamii Kipunguni ni mojawapo ambacho wanajivunia.
Mradi huo uliofadhiliwa na Amref una thamani ya Sh milioni 26 unahusisha pia kufungwa kwa mashine mbalimbali za kutengeza mkaa huo, sehemu ya kukaushia taka na gari la kubebea taka.