23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Kipunguni wahakikishiwa kulipwa fidia kabla ya Oktoba

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imetenga Sh bilioni 143.9 kuwalipa fidia wakazi 1,865 wa Mtaa wa Kipunguni Kata ya Kipawa wanaotakiwa kuhama kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Wakazi hao awali walifanyiwa tathmini mwaka 1997 na tangu wakati huo wamekuwa wakisubiri kulipwa fidia kupisha upanuzi huo.

Wananchi wa Mtaa wa Kipunguni Kata ya Kipawa wakimsikiliza Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kipunguni, Dar es Salaam. (Picha na Nora Damian).

Akizungumza na wakazi hao leo Julai 7,2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kipunguni, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema fedha hizo zitalipwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2023/24.

Amesema wanapomaliza mwaka wa fedha huwa kunakuwa na masuala ya kimfumo lakini kuanzia Agosti watawatangazia siku rasmi ya kulipwa.

“Tathmini zimeshafanyika, ridhaa ya mama (Rais) imeshatoka, tunachoweza kufanya ni kujipanga kuhusu kuwalipa. Mbunge (Bonnah Kamoli) ametubana anasema ndani ya robo ya kwanza hili jambo lifanyike.

“Jambo hili limeshafika mwisho kilichobaki ni ninyi kulipwa fedha…nitalitekeleza hili kwa haraka,” amesema Dk. Nchemba.

Naye Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amesema wananchi hao wamesubiri fidia kwa miaka 26 hali iliyosababisha washindwe kuendeleza makazi yao.

“Nilikuwa diwani wa kata hii nimeliongelea sana suala hili, nimeongea bungeni, tuna imani huu utakuwa mkutano wa mwisho, hatutakaa tena mkutano mwingine kujadili suala hili,” amesema Bonnah.

Mbunge huyo ameiomba Serikali kuharakisha malipo hayo ili kurahisisha pia utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Awali Mkurugenzi wa Uhandisi na Huduma za Ufundi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Focus Kadeghe, amesema mwaka 2009 waathirika wa mradi walikuwa 1,125 lakini wameongezeka na kufikia 1,865 kutokana na baadhi ya wananchi kukata maeneo yao na kuyauza.

Hata hivyo TAA imependekeza wananchi waliopewa viwanja Msongola na Majohe warudishe kwa Serikali vinginevyo wakubali kukatwa fedha kufidia thamani ya viwanja walivyogawiwa awali.

“Tunapendekeza kuundwa kikosi kazi cha kushughulikia changamoto za viwanja kwa wananchi waliohamishwa kutoka maeneo ya Kipawa, Kigilagila na Kipunguni pamoja na wananchi waliokuwa wamiliki wa asili katika eneo la Pugu Mwakanga,” amesema Kadeghe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles