31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kippi aondoa kesi kupinga ushindi wa Mdee

Kippi WariobaNa Kulwa Mzee, Dar es Salaam

ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kippi Warioba, ameondoa kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Kippi aliyegombea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu alifungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Mdee, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.

Katika kesi hiyo namba 7 ya mwaka jana, Kippi alikuwa akiiomba mahakama hiyo ibatilishe uchaguzi huo akidai kuwa  haukuwa huru na wa haki.

Hata hivyo, Mdee kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala, alimwekea pingamizi akitoa hoja sita akiiomba mahakama hiyo itupilie mbali kesi hiyo.

Mbali na Kibatala pia AG naye alimwekea Kippi pingamizi na akiomba mahakama itupilie mbali kesi hiyo.

Kutokana na pingamizi hilo, Kippi, kupitia kwa wakili wake, Emmanuel Makene, alikubaliana na hoja za pingamizi hilo na kuomba kuiondoa mahakamani kesi hiyo.

Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo jana, Jaji Zainabu Mruke, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kwa kuwa mlalamikaji amekubaliana na hoja za pingamizi na ameamua kuiondoa mahakamani kesi hiyo, nayo inaamuru iondolewe.

Mbali na kuiondoa pia mahakama ilimwamuru Warioba kumlipa Mdee gharama za kesi hiyo.

Katika pingamizi lake, Kibatala aliiomba mahakama iifute kesi hiyo akidai kuwa ina kasoro za kisheria zinazoifanya isiwe na msingi.

Kibatala alidai kuwa baadhi ya tuhuma za mlalamikaji ni ya kikatiba na hayana nafasi katika kesi hiyo na iko kinyume cha sheria kwa kuwa imesainiwa na wakili ambaye hayuko katika kumbukumbu za mahakama za kesi hiyo.

Kwa upande wake, AG alidai kuwa kesi hiyo iko kinyume cha sheria kwa kuwa haikuzingatia kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) za mwaka 2010.

Katika kesi ya msingi, Kippi, alikuwa akidai pamoja na mambo mengine kuwa kulikuwa na tofauti ya namba kati ya kura halali na kura zilizokataliwa kulinganisha na jumla ya kura zote.

Pia alikuwa akidai kuwa katika baadhi ya vituo vya kura zilizokataliwa hazikuonyeshwa na badala yake ziliongezwa katika kura za Mdee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles