21.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kipigo cha Lipumba chazua mtafaruku

Pg 1upinzani wasimamaNa Waandishi Wetu, Dar na Dodoma

WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana, Bunge lilivunja kikao chake baada ya kuibuka mjadala mkali kutoka kwa wabunge wa kambi ya upinzani.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alilazimika kuahirisha Bunge baada ya wabunge hao wa upinzani kutaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili wajadili kitendo cha Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kumpiga Profesa Lipumba na wenzake.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4 asubuhi baada ya Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), kuomba mwongozo akitaka tukio hilo lijadiliwe kwa masilahi ya taifa.
Katika mwongozo wake, Mbatia alitumia kanuni ya 47 inayoeleza jinsi mbunge anavyoweza kusimama na kuomba mwongozo kwa spika akitaka shughuli za Bunge za siku hiyo ziahirishwe ili suala muhimu lijadiliwe kwa masilahi ya taifa.
Katika mwongozo wake, Mbatia, alisema kitendo kilichofanywa na polisi hakiwezi kuvumiliwa kwa kuwa kimekiuka haki za binadamu kwa vile Profesa Lipumba na wananchi wengine walipigwa bila sababu za msingi.
“Mheshimiwa Spika, juzi Januari 27, mwaka huu kule Temeke, Dar es Salaam, Profesa Lipumba alikuwa na ratiba ya mkutano wa hadhara na maandamano.
“Lakini, dakika za mwisho kabla ya mkutano huo, polisi walizuia mkutano usiendelee na baadaye wakaamua kuwapiga raia wasiokuwa na hatia, akiwamo Profesa Lipumba, wafuasi wa CUF, watoto walio chini ya miaka mitano pamoja na waandishi wa habari.
“Mheshimiwa Spika, jambo hilo linaonyesha hali ya hatari, na mimi nilisikitika sana nikalazimika kumpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani kumweleza hali ilivyokuwa mbaya.
“Kibaya zaidi, polisi wenyewe wamesema walilazimika kufanya hivyo kwa sababu walipokea maagizo kutoka juu. Kwahiyo, Mheshimiwa Spika, tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.
“Mheshimiwa Spika, ni miaka michache tu tumeshuhudia polisi wakiua raia, wakiua waandishi wa habari na raia wakiua polisi, lazima mambo haya tuyakemee kwa nguvu zote kama tunataka kujenga taifa lenye umoja.
“Kwahiyo, Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja, tuahirishe Bunge ili tujadili jambo hili lisije likajirudia tena, naomba kutoa hoja,” alihitimisha Mbatia.
Pamoja na hayo, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, alisema kitendo cha kumpiga Lipumba kinaweza kuhatarisha amani nchini kwa kuwa anaongoza wabunge zaidi ya 30 walioko bungeni na pia ni kiongozi wa chama kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Kisiwani Zanzibar.

SPIKA ATOA MWONGOZO
Baada ya Mbatia kusema hayo, wabunge wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni walimuunga mkono kwa kusimama.
Wakati wabunge hao wamesimama, Spika Makinda alisimama tena na kusoma kifungu cha nne cha kanuni ya 47 iliyotumiwa na Mbatia.
Katika maelezo yake, alizungumzia kifungu hicho na kusema kinaruhusu jambo la dharura kujadiliwa kama spika atakuwa ameridhika nalo. Kwa hiyo, aliagiza shughuli za Bunge ziendelee, lakini akaiagiza Serikali itoe kauli bungeni juu ya tukio hilo.
“Kanuni ya 47 kifungu cha nne, kinanipa mamlaka kuahirisha shughuli za Bunge ili jambo la dharura lijadiliwe kama nitaridhishwa nalo. Kwahiyo, naiagiza Serikali ilifuatilie jambo hili, itoe kauli kamili hapa leo na nitaruhusu mjadala,” alisema Spika Makinda na kutaka shughuli za Bunge ziendelee kama zilivyokuwa zimepangwa.

WAPINZANI WAMGOMEA

Majibu ya Spika Makinda yalionekana kuwatibua wabunge wa upinzani, kwani walianza kuzungumza bila utaratibu wakionyesha kutoridhishwa na uamuzi huo.
Kutokana na hali hiyo, Spika mara kadhaa alilazimika kusimama huku akiwaomba wakae ili shughuli za Bunge ziendelee, lakini hawakumsikiliza na badala yake waliendelea kupiga kelele.
“Jamani nawaomba mkae chini na kama mnataka kutoka nje tokeni. Nawaambia jambo hili mnalolizungumza ni kubwa sana na tumelizungumza asubuhi mimi na Mbatia, Mnyaa na Tundu Lissu, nawaomba mkae chini msitake kunifanya kama Kangaroo Court,” alifoka.
Hata hivyo, kauli hizo hazikusaidia kitu, wabunge waliendelea kupiga kelele wakitaka suala hilo lijadiliwe wakati huo.
Baada ya kelele kuzidi, Spika alilazimika kuahirisha Bunge hadi jana saa 10 jioni.

MAHAKAMANI
Jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba (62), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kushawishi wafuasi wa chama chake cha CUF kutenda kosa la jinai.
Profesa Lipumba aliyekamatwa pamoja na wenzake zaidi ya 30, alifikishwa mahakamani hapo saa 8 mchana na kusomewa mashtaka yanayomkabili peke yake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Arufani.
Mshtakiwa huyo alifika mahakamani saa 7.45 mchana na ilipofika saa 9 alasiri, alipandishwa ukumbi namba mbili wa mahakama.
Alisomewa mashtaka yanayomkabili na Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, akishirikiana na Wakili Hellen Moshi.
Wakili Maugo, alidai kati ya Januari 22 na 27, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mwenyekiti wa CUF, aliwashawishi wafuasi wake kufanya kosa la jinai.
Profesa Lipumba, akitetewa na jopo la mawakili watano, wakiwamo Mohammed Tibanyendera, Peter Kibatala, John Mallya na wengine, alikana kutenda kosa hilo kwa kusema ni shtaka la uongo.
Wakili Maugo, alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo na kwamba hawakuwa na pingamizi kuhusu mshtakiwa kupewa dhamana.
Upande wa utetezi uliiomba mahakama kumpatia mshtakiwa masharti nafuu kwa kuwa ana wadhamini wanaoaminika.
Hakimu Arufani, alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana iwapo atasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni mbili, na kuwa na wadhamini wawili watakaotia saini dhamana ya kiasi hicho cha fedha.
Profesa Lipumba alitimiza masharti hayo baada ya kudhaminiwa na Diwani wa Kata ya Saranga, Kinondoni, Hilda Mtiya na Mbunge wa Viti Maalumu, Kuruthum Jumanne. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 26, mwaka huu.
Wafuasi wa CUF waliofurika mahakamani hapo, walitoka mahakamani wakiwa na furaha, huku wakiimba wakati wakielekea lango la kutokea mahakamani.
Baada ya Profesa Lipumba kukamilisha taratibu za dhamana, aliwasihi wafuasi wake kuondoka katika eneo la mahakama kwa hali ya amani na utulivu, akidai wakifanya vurugu wanaweza kukamatwa. Wafuasi hao walitii amri na kutawanyika.

HALI ILIVYOKUWA

Wanachama na wafuasi wa CUF walizingira Kituo Kikuu cha Kati cha Dar es Salaam wakisubiri kujua hatima ya mwenyekiti wao, Profesa Lipumba, aliyekuwa anatarajiwa kufika kituoni hapo kuripoti kwa kosa la kuandamana bila ya kuwa na kibali.
Baada ya askari kuona umati huo, walianza kuutawanya eneo hilo kwa madai hawakutakiwa kuwapo, kauli ambayo waliitii na kuhamia ng’ambo ya barabara.
Ilipofika saa 4.42 asubuhi, Profesa Lipumba alifika akiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 467 BLJ hali iliyosababisha wafuasi na mashabiki wa chama hicho kutoka barabarani na kusogea jirani na lango la polisi, huku wakimpa moyo kwa kutoa salamau ya ‘haki’, wengine wakiitikia ‘sawa’.
Alipoingia ndani ya kituo cha polisi kwa ajili ya kujua hatima yake, hakukaa muda mrefu alirudi nje na kuzungumza na waandishi wa habari na kuwaeleza kuwa polisi wamemruhusu kuondoka kutokana na mashtaka yake kutoandaliwa.
“Tuliitwa kuja hapa na sisi tumetii, ila wametuomba tuje leo, kwa sababu walikuwa hawajaandaa ‘charge sheet’ kwa ajili ya kutupelekea mahakamani kwa kosa la kuandamana bila kibali,” alisema.
Profesa Lipumba, alisema kitendo cha kukamatwa ni mwendelezo wa matukio yanayofanywa na Serikali kwa ajili ya kuiminya demokrasia ya vyama vingi, ambavyo vimeonekana kuwa tishio kwa kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“CUF tuliomba kibali Januari 22, mwaka huu na kutoa taarifa kwa wanachama wetu, lakini polisi wakatoa majibu ya kukataa Januari 26, mwaka huu saa 12:30 muda ambao tulikuwa tumefunga ofisi zetu.
“Kwa muda huo naamini polisi walijua isingekuwa rahisi kuwazuia wanachama wetu kusitisha maandamano hayo, hali iliyonifanya niamini walipanga kuwadhuru wanachama wetu,” alisema Lipumba.
Alisema aliamua kuchukua busara na kwenda maeneo ya Temeke kuwazuia wanachama wao wasiandamane kama ambavyo polisi walikuwa wamewaamuru.
“Niliwaomba polisi waliokuwa pale Temeke waniruhusu nikawazuie wanachama waliokuwa uwanja wa Zakhem ambao walikubaliana na mimi, lakini tukiwa njiani kwenye mzunguko wa barabara ya Mbagala, nilisimamishwa nikawaeleza wale polisi waliokuwa pale ambao walionekana kunielewa.
“Tukiwa tunajiandaa na viongozi wenzangu kuondoka, alikuja ofisa mmoja wa polisi, mweusi hivi, ambaye alikuwa na kitambi cha bia za rushwa, akawaamuru polisi kutupiga na kutukamata… Kambaya alipigwa ngeu kichwani,” alisema.
Profesa Lipumba, alisema tukio hilo analitafsiri kama njia ya ukombozi ipo wazi kwa CUF na washirika wao wa Ukawa katika uchaguzi mkuu ujao.
“Nilijiuliza kwanini mwaka huu polisi wametumia nguvu kubwa wakati kila mwaka tumekuwa tukikutana kwa ajili ya kuwakumbuka ndugu zetu waliouawa kule Zanzibar Januari 27, 2010,” alisema Lipumba.
Naye wakili wa Profesa Lipumba, Hashim Mziray, aliyekuwa akiongoza jopo la mawakili watano kutoka vyama vinavyounda Ukawa, alisema watahakikisha wanapambana ili haki ipatikane.
Baada ya wakili huyo kuzungumza hilo, ndipo alikuja askari mmoja na kumuita Profesa Lipumba na kumrudisha tena kituoni kwa ajili ya kupelekwa mahakamani.
Ilipofika saa 7:00 mchana, Profesa Lipumba aliomba kwenda kumuona daktari wake kwa sababu tangu alipokamatwa na kuswekwa rumande juzi usiku, hakupata muda wa kuonana na daktari wake kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ambapo alikuwa akisikia dalili za shinikizo la damu, maumivu sehemu za kichwani na kifuani.
Polisi walikubali kumpeleka kwa daktari wake wa kliniki ya Umoja wa Mataifa iliyopo Oysterbay chini ya ulinzi, wakitumia gari lenye namba za usajili PT 2566.
Alipewa matibabu na kubainika kwamba shinikizo la damu lilikuwa juu hali iliyomfanya daktari kumtaka apumzike kwa muda wa wiki mbili.
Jambo la kushangaza baada ya kutoka kumuona daktari wake, akiwa chini ya ulinzi wa polisi, Profesa Lipumba alichukuliwa moja kwa moja kwa gari hilo ambalo lilikuwa likienda kwa kasi kwa nia ya kuwakwepa waandishi wa habari na kupelekwa Mahakama ya Kisutu.
Akizungumzia kuhusu tukio hilo, kada wa CUF, Mbarallah Maharagande, alisema ameshangaa kuona namna ambavyo polisi wametumia nguvu zisizo za lazima.
“Natoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete azungumze na watendaji wake kuacha tabia ya kuwapiga watu, kwani watakapochoka watajibu mapigo na suala hilo ni baya ukizingatia tunaelekea katika uchaguzi mkuu na upigaji kura wa Katiba inayopendekezwa,” alisema.
Salum Abdul, alisema polisi wametumia ubabe katika tukio ambalo Profesa Lipumba alikuwa ametumia busara ya kulisitisha.
Naye Shukuru Hassan ambaye amejitambulisha kama mjumbe wa serikali ya mtaa wa Buguruni Kisiwani, alisema kuwa tukio hilo ni la kudhalilisha jeshi la polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles