BERLIN, UJERUMANI
KIONGOZI wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto nchini hapa cha Social Democrats (SPD), Andrea Nahles amejiuzulu baada ya kipigo ilichokipata chama chake katika uchaguzi wa bunge la Ulaya.
Nahles alisema katika taarifa yake jana kuwa anataka uwazi baada ya maswali kuzuka hivi karibuni kuhusiana na uwezo wake wa kukiongoza chama hicho mshirika katika Serikali ya muungano inayoongozwa na Kansela Angela Merkel, na kuonesha kwamba anakosa uungwaji mkono wa wanachama.
Nahles alisema atajiuzulu kutoka wadhifa wake wa mwenyekiti wa chama cha SPD na kiongozi wa kundi la wabunge wa chama hicho bungeni, kuhakikisha kwamba mrithi wake anapatikana kwa utaratibu mzuri.
Chama cha SPD kilishika nafasi ya tatu nyuma ya chama cha Kansela Merkel cha CDU na kile cha Kijani katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya nchini Ujerumani.