Na Seif Takaza, Iramba
KIONGOZI wa Mbio za za Mwenge Kitaifa, Abdallah Shaib Kaim amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kwa kufanikisha miradi ya mbio za Mwenge ambapo miradi yote iliyokaguliwa iko katika kiwango kizuri.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge ameyasema hayo juzi wakati akitoa ujumbe wa Mwenge katika uwanja wa CCM Lulumba mjini Kiomboi mkoani Singida ambapo amesema Mwenda na timu yake akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Warda Abdallah ambaye alisoma Risala ya Utii kwa Rais Smia Suluhu Hassan wametekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.
“Miradi yote tuliyoikagua iko katika kiwango kinachoridhisha ingawaje kuna baadhi ya miradi inahitaji kufanyiwa marekebisho, ndugu yangu Suleiman Yusuph Mwenda kwa dhati kabisa nakupongeza wewe na timu yako pamoja na madiwani wote wakiongozwa na Mwenyekiti wa halmashauru ya wilaya, mmefanya vizuri mnastashili pongezi,” alisisitiza Kiongozi huyo wa Mwenge Kitaifa.
Aidha, Kaim amekemea tabia ya baadhi ya wananchi na wenye dhamana kutojihusisha na rushwa kwani rushwa humnyima mwananchi haki yake na kupewa mtu mwingine na hudhoofisha maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleimn Mwenda amemshukuru kiongozi wa mbio za kitaifa kwa kukagua miradi na kuipitisha na kwamba hiyo ni dalili ya kwamba wataalam pamoja na wananchi kwa ujumla tumeutendea haki mwenge wa uhuru.
“Kwa kweli ndugu zangu wakimbiza mwenge Kitaifa sisi wananchi wa Iramba tumeutendea haki ambapo miradi nane yenye thamani ya Sh bilioni 4.15 imefunguliwa, kuonwa na kuwekewa mawe ya msingi,” amesema Mwenda.
Aidha mwenge huo umezindua mradi wa upandaji miti katika kijiji cha Mseko huku ukizindua mradi wa Masjala ya Ardhi katika kijiji cha Masagi lengo likiwa ni Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara (MKURABITA).
Akitoa maelezo kuhusu masjala hiyo Mkuu wa Idara ya Ardhi wilayani Iramba, Magesa Aspeaas Magesa alisema mradi huo utawezesha kijiji kutoa huduma kwa ukaribu kwa wananchi wa kijiji hicho.
Magesa amesema mradi huo umegharimu Sh milioni 64 ikiwemo michango ya wananchi Sh milioni 3, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali katika kijiji cha Msingi ambapo katika Wilaya ya Iramba umekimbizwa zaidi ya kilomita 135.
Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleman Mwenda alikabidhiwa juzi na mkuu wa mkoa wa Singida, Peter Serukamba aliyekabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dk. Batrida Buriani.