Amina Omari, Korogwe
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Mkongea Ally amegoma kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika Barabara ya Hoza – Ramia iliyoko katika Halimashauri ya Mji Korogwe kutokana na kubadilishwa shughuli ya kuweka jiwe la msingi badala ya kuzindua barabara.
Awali, ratiba ilionyesha Mwenge wa Uhuru unahitaji kuzindua barabara hiyo na badala yake ukatakiwa uwekewe jiwe la msingi.
Akizungumzia mara baada ya uamuzi huo, amesema ameshangazwa na kitendo cha kupewa maelekezo tofauti na taarifa ambayo ilikuwepo kwenye ratiba.
“Leo asubuhi nimepokea barua kutoka kwa Katibu Tawala wa mkoa ya kunitaka niweke jiwe la msingi badala ya kuzindua,wakati tunaingia kwenye mkoa huu nilikabidhiwa ratiba inayoonyesha shughuli ambazo mwenge wa uhuru utafanya”amsema Ally
Hata hivyo, kiongozi huyo aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza mradi huo kwani una dalili zote za ubadhirifu.
Awali, akisoma taarifa ya mradi huo wa barabara ya kiwango cha lami, Mhandisi wa Wilaya Godfrey Bwire, amesema barabara hiyo yenye urefu wa Kilometa 0.696 iligharimu zaidi ya Sh milioni 843.