FRANCIS GODWIN – IRINGA
TAASISI isiyo ya kiserikali ya Iringa inayojishughulisha na masuala ya msaada wa kisheria mkoani Iringa, Parelegal Centre (IPACE) imesema vifo vya baadhi ya wanaume mkoani Iringa, vimekuwa vikisababishwa na vinyongo walivyonavyo kwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kama kupigwa na wake zao na kutunza siri hiyo moyoni.
Mwenyekiti wa IPACE, Issac Kikoti aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku 16 za ukatili wa kijinsia Tanzania yanayofanyika kimkoa Kijiji cha Kiwere.
Kikoti alisema suala la ukatili wa kijinsia ndani ya mkoa huo ni kubwa pamoja na kuwa bado hakujawa na takwimu sahihi.
Alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa sababu zinazochangia vifo kwa baadhi ya wanaume, hasa wale ambao wamekuwa wakivumilia mateso ya kupigwa na kutunza siri hizo.
Kikoti alisema utunzaji wa siri moyoni ni miongoni mwa mambo yanayowatesa wanaume na hata kujikuta wanapatwa na vifo vya ghafla.
“Wanaume wengi wananyanyasika katika ndoa zao, wapo ambao wanapigwa na wapo ambao wananyimwa ‘ugali wa usiku’ na wake zao, ni waoga wa kutoka nje kwenda kulalamika juu ya manyanyaso hayo na hii ni hatari kukaa na kitu kibaya moyoni,” alisema Kikoti.
Alisema pamoja na matukio ya ukatili dhidi ya watoto kuwa makubwa katika jamii, jamii haipo tayari kujitokeza kupinga ukatili huo.
Kikoti alisema suala la kupinga ukatili wa kijinsia ni jukumu la kila mmoja.