FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM
MANISPAA ya Kinondoni imekuja na mbinu mpya ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ngozi kwa kufanya maonesho ya bidhaa hizo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mkuu wa Wilaya hiyo, Daniel Chongolo, alisema Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na ng’ombe wengi barani Afrika nyuma ya Ethiopia lakini matumi ya ngozi yamekuwa hafifu.
“Takwimu za mwaka 2018/19 zinaonyesha Tanzania ina ng’ombe milioni 32.2 mbuzi milioni milioni 5.5 na kaya takriban milioni 4.6 zinajihusisha na ufugajihali ambayo imeonyesha kuwa ufugaji ni eneo muhimu katika kuondoa umaskini.
“Lakini kama haitoshi Tanzani ina viwanda tisa tu vya kuchakata ngozi vikiwa na uwezo wa kuchakata vipande milioni 3.8 vya ng’ombe na vipande milioni 12.8 vya mbuzi /kondoo kwa mwaka, hivyo tukaona kama wilaya tuna haja ya kuja na maonyesho haya ya bidhaa za ngozi ambayo yatafanyika katika viwanja vya Tanganyika Peckares Kawe jijini Dar es Salaam,” alisema Chongolo.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuwahamasisha kutangaza uwezo wa wadau wa bidhaa za ngozi katika wilaya hiyo na nchini kwa ujumla.
“Lakini pia kuelimisha jamii juu ya kutumia bidhaa za ndani zenye ubora, kuongeza na kukuza viwanda vya ndani vya ngozi ambavyo vitaongeza uzalishaji na ubora wa ngozi sanjari na kuongeza ajira,” alisema.
Chongolo pia alisema wanatarajia kupata washiriki zaidi ya 100 ambao wataonyesha bidhaa zao kwenye maonyesho hayo huku akiwataka wananchi wenzi zaidi kujitokeza.