23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kingunge alijitwisha mizigo mizito – Bgoya


ANDREW MSECHU

SIMULIZI mpya juu ya mambo aliyowahi kuyafanya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, imeibuliwa ikiwa ni mwaka mmoja tangu afariki dunia Februari 2, mwaka jana.

Nguli huyo wa siasa ameibuliwa katika uzinduzi wa Kitabu cha ‘Mazungumzo na “Kingunge” wa Itikadi ya Ujamaa’ kilichoandaliwa na Kavazi la Mwalimu Nyerere chini ya usimamizi wa Profesa Issa Shivji.

Walter Bgoya, Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuki na Nyota ndiye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.

Anaeleza mambo mbalimbali kuhusu misimamo na mitazamo aliyokuwa nayo Kingunge.

 “Mimi sikuwahi kumwita mzee, kwa sababu wakati wote katika mazungumzo yetu hakukuwa na wazo lililoonekana la kizee. Katika miaka yote alikuwa mnywaji mzuri, sikuwahi kumfikia, ila miaka mitatu ya mwisho ya uhai wake nilianza kumzidi kidogo (kicheko),” anaeleza kwa utani.

Anasema katika maisha yao ya utumishi na siasa, waliweza kukutana na makomredi (neno linalotumika kumaanisha mwenzangu katika mapambano) wengi ambao walikuwa wakikutanishwa na harakati na kumbukumbu za mapambano ambazo ziliwasukuma kukutana, kujenga uaminifu na kutegemeana kwa kazi ngumu.

Bgoya anasema alimfahamu kama komredi na ilibaki hivyo hivyo kama komredi ambaye alikuwa msomi makini katika Siasa na Sayansi ya Jamii.

Itikadi na msimamo

Mwanazuoni huyo anasema Kingunge alikuwa mfuasi wa itikadi za Kimarx aliyekuwa thabiti, ndiye pekee katika kumbukumbu zake aliyekuwa akiapishwa bila kushika msahafu wa dini yoyote wakati akikabidhiwa madaraka serikalini.

Anasema japokuwa baadhi ya wapinzani wake walitumia hiyo kujenga hoja zao na kumshtaki katika hilo hata hivyo alipangua hoja zao vizuri na kumfanya Mwalimu Julius Nyerere amwamini.

Bgoya anasema kutokana na hulka yake na namna alivyokuwa akisimamia yale anayoyaamini, kama si kuwa na kiongozi wa aina ya Mwalimu Nyerere, Kingunge asingepewa nafasi yoyote ya uongozi wala asingekuwa na nafasi ya kufundisha siasa ndani ya chama.

“Kama si mwalimu Nyerera Kingunge asingeweza kupata nafasi yoyote katika chama na Serikali, kutokana na namna walivyokuwa wakitofautiana kwa hoja lakini wakifikia hatua wakikubaliana.

“Alikuwa na mitizamo mipana kuna mahala waliweza kutofuatiana na Mwalimu, angekuwa kiongozi mwingine asingeweza kumpa nafasi, lakini Mwalimu aliendelea kutambua umuhimu wake na kuendelea kumpa nafasi,” anasema.

Anaeleza kuwa Kingunge hakuwa na majivuno wala kuonyesha usomi wake, hivyo waswahili wengi walidhani kuwa ni mtu mwenye kipaji tu.

Umahiri wake katika kusimamia siasa hasa ya ujamaa ilimpa umaarufu mkubwa kwa kuwa na maelfu ya wanachama waliopitia mikononi mwake.

Katika vyama vya ukombozi wengi wao walikuwa na uhitaji wa mafunzo na waliweza kusaidiwa kupitia kwa Kingunge, ambaye alitumia nafasi yake kumshawishi Mwalimu wakae nchini na kupata msaada.

Bgoya anasema siku zote Kingunge alikuwa tayari kukabiliana na jambo lolote hata kama lingemgharimu na mara nyingi alijitwisha mizigo mizito lakini hakujuta kwani aliamini kwa kufanya hivyo ataleta tofauti na kusimamia haki itendeke.

Anasema miongoni mwa mambo ambayo hata yeye hakuyatarajia ni pale alipowashangaza wana CCM siku alipoibuka Arusha kwenye mkutano wa Edward Lowassa alitumia kutangaza kujiondoa CCM na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo -Chadema.

Hatua hiyo ya Lowassa ilikuwa baada ya CCM kukata jina lake katika hatua za awali, akiwa miongoni mwa wagombea waliokuwa wakiomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Anasema alimwelewa Kingunge kwa kuwa jambo kubwa alilochukua kwake ni kwamba katika maisha yake yote tangu alipokuwa mdogo alichukia sana kuona watu wanaonewa, na katika uamuzi wake huu alilalamika sana kwamba CCM haikumtendea haki Lowassa.

Bgoya anasema hakusita kumuuliza Kingunge sababu ya kuungana na Lowassa, na kujibu ni kwa sababu Lowassa alivikwa kashfa iliyomsababisha ajiuzulu katika nafasi yake ya uwaziri mkuu kuinusuru Serikali, lakini wenzake hawakwenda naye.

“Kingunge alikuwa akisisitiza kuwa kujiuzulu kwake hakukumaanisha kuwa yeye binafsi alikuwa na hatia, alijiuzulu ili kuepusha uwezekano wa Serikali yote kuanguka na kulazimika kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

“Ilikuwa imekubaliwa  katika ngazi za uongozi wa juu wa chama kuwa katika muda mfupi baada ya kujiuzulu kwake mazingira yangeandaliwa ya kumsafisha na kurejesha heshina na stahili zake za kisiasa, lakini hayo mazingira hayakuandaliwa kwa hiyo kwake, hatua ya chama kutotekeleza ahadi yake iliongeza uzito wa uonevu,” anasema.

Mwanazuoni huyo anaendele kueleza kuwa ukiacha suala la Lowassa kuonewa, pia alipata picha nyingine ambayo ilihusisha wale waliopita kwenye kinyang’anyiro na  nilimuuliza Komredi, kwani ni mara ya kwanza kwa CCM kuwatema wale ambao kamati kuu iliwakataa?

“Nilimuuliza ni suala la historia, wanachama wangapi wa ajabu ajabu waliwahi kupitishwa na kuwa viongozi ambao waliitwa feki? na wangapi walioonekana kwa wananchi kuwa wanafaa lakini wakatemwa?” anasema.

Bgoya anasema aliendelea kumuuliza Kingunge kuwa alipokuwa ngazi za juu hakuliona hilo, ilhali lilikuwa linafanyika katika chama chake?.

Hata hivyo anasema kitendo cha kukubalika kwa Lowassa anafikiri Kingunge alikuwa sahihi kwa kuwa taarifa zilienea kwamba alikuwa amejiandaa vizuri sana na angalau kwa uchache alishapata asilimia 70 ya wajumbe wa NEC, kabla hata mkutano mkuu haujaanza.

“Mtakumbuka kuwa wakati mwenyekiti akiingia kwenye mkutano wa wajumbe wa NEC walikuwa wakiimba ‘Tuna imani na Lowassa, oyaa oyaa oyaa’, kitendo ambacho anaamini kilizidi kuitibua kamati kuu katika hatua hiyo hata aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume alisema kwamba yeye alikuwa karibu sana na Lowassa na aliona hiyo haikubaliki. Sasa ndani ya mjadala huo huwezi kujua nini kilichochea zaidi,” anasema.

Anasema kwa misimamo ya Kingunge katika kuamua alikuwa thabiti na iwapo angekuwa hai, anadhani angefurahi pia kwa hatua ya Lowassa kurejea CCM, kwa misingi kuwa kasoro zilizojitokeza zimepatiwa ufumbuzi.

Anasema katika jambo jingine, Kingunge aliwahi kulalamika kuwa miongoni mwa mambo yaliyomuuliza ni pale marafiki zake walipoa acha kwenda kumtembelea.

Anasema katika hilo, hakushangaa sana kwa sababu ni kawaida kwamba unapoondoka katika madaraka au mamlaka fulani, watu nao wanakusahau, kwa kuwa hawawezi tena kupata kile walichokuwa wakihitaji kwenye mamlaka yako.

Mjadala wa Kingunge haukuishia kwa Bgoya tu, mwanahabari wa siku nyingi na mwanasheria Jenerali Ulimwengu, alimzungumzia nguli huyo wa siasa.

Anasema aliwahi kuwa karibu na Kingunge na anatambua kuwa alikuwa ni zao la makutano ya harakati tofauti katika kipindi kimoja, suala lililomjenga kuwa kiongozi wa aina yake.

Anasema kutokana na umahiri wake, kingunge alikuwa kiungo hai kati ya matumaini na matarajio ya Watanzania na harakati za ukombozi zilizokuwa zikiendelea katika nchi za dunia ya tatu.

Kingunge ni mtu aliyekuwa na upeo mpana ambaye katika ujana wake alipata fursa ya kukutana na watu kutoka karibu katika maeneo yote ya nchi za dunia ya tatu, kutokana na harakati za kombozi alizokuwa akishiriki.

“Alikuwa mtu mwenye utashi na uwezo mkubwa wa kujieleza au kutetea jambo. Alikuwa mwanasiasa wa kipekee. Wengi wanaojiita wanasiasa na wanaofanya siasa leo si wanasiasa bali ni wanamipango wanaofanya mipangilio.

“Hawana wanachokiamini bali wanaimba kile anachokisema ‘bwana mkubwa’ na unaobaki ni mwangwi wa bwana mkubwa kasema nini, hakuna anayehoji. Huo ndiyo ufu wa siasa ambao upo kwa saa lakini pia kwa upande mwingine ulikuwepo tangu enzi hizo,” anasema.

Ulimwengu anasema Kingunge alikuwa mtu huru ndani ya mfumo uliokuwepo kwa kuwa alikuwa haogopi kusema na kutetea anachokifikiri na anachokiamini na kuchukua hatua inayofaa, tofauti na wanasiasa hawa wa mipango.

Mtaalamu wa lugha za kigeni, Profesa Martha Qorro naye hakusita kumwelezea alivyomfahamu Kingunge kutokana na urafiki wake na Patrick Qorro, kwamba alimuona kuwa kiongozi makini, shupavu na imara, mwenye ushawishi na muwezo mkubwa wa kufanya mambo.

“Ninakumbuka kikosi chao kilikuw akikija pale nyumbani (kwa Patrick Qorro, mimi nikiwepo kazi yangu ilikuw ani kuwahudumia vinywaji. Waliweza kufika pale saa 12 jioni na mazungumzo na mijadala yao ikikolea wanaweza kiendelea hadi alfajiri, hadi majibu yapatikane,” anasema.

Mwingine aliyemzungumzia ni Profesa Hamudi Majamba ambaye anasema alimfahamu kama mume wa dada yake, lakini pia mlezi na mshauri aliyemsaidia katika vipindi vyote, hasa alipopata matatizo ya kufukuzwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991 kwa madai ya kumtukana Rais matusi ya nguoni.

Anasema katika yote, Kingunge ambaye alifariki akiwa upinzani, tangu alipochukua uamuzi wa kujiweka kando CCM aliendelea kusisitiza kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na kukiukwa kwa kanuni walizokuwa wamejiwekea hivyo aliamua kukaa kando kwa kuwa yeye si mkubwa kuliko chama.

Jaji Joseph Warioba, anasema alifahamiana na Kingunge walipoanzisha Kikundi cha Kujisomea cha TANU mwaka 1966 wakiwa na akina Bgoya, Lawrence Gama, Patric Qorro na wengine na kuwa alimtambua kuwa mtu anayejiamini na aliyesema anachokiamini bila woga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles