31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kingereza ni kikwazo kwa wanafunzi sekondari

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ihsan wakiwa darasani.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ihsan wakiwa darasani.

Na Hamisa Maganga,

UTOAJI elimu nchini umekuwa na changamoto nyingi hasa kwa shule za serikali na zile za binafsi. Baadhi ya changamoto hizo ni miundombinu mibovu, nguvu kazi, maadili, sera za elimu, mfumo wa elimu na nafasi ya wazazi wa leo katika malezi na usimamizi wa watoto nyumbani na wawapo shuleni.

Mbali na hayo, changamoto nyingine ambayo walimu wengi wa sekondari wanapata ni vijana wanaojiunga na shule hizo kuwa na msingi mbovu ambao unasababisha kutafsiriwa kuwa vijana hao wana uwezo na uelewa mdogo wa masomo darasani.

Katika mahojiano na gazeti hili hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ihsan, iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, Yusuph Ramadhani, anasema shule za sekondari zinapokea wahitimu waliopata elimu ya msingi wapo katika makundi mawili.

Anayataja makundi hayo kuwa ni  kuwapo kwa wanafunzi wenye msingi mzuri wa elimu. Pia hupokea wanafunzi ambao hawana msingi mzuri. Pamoja na kuwa wanatofautiana, mwishowe siku vijana wote wakisimamiwa vizuri kulingana na mahitaji yao hufanya vizuri katika mitihani ya taifa.

“Kwa kweli hii ni changamoto, huwa tunapokea baadhi ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba ambao wakati mwingine wanakosa nafasi katika shule za serikali na huwa wana uwezo mdogo unaotokana na sababu mbalimbali.

“Aina hii ya wanafunzi wakiachwa walivyo inakuwa ngumu kumudu masomo ya sekondari. Kinachofanyika ni kubaini matatizo ya mtoto mmoja mmoja na kuwasaidia kulingana na tatizo lake… kwa kweli baadae huwa wanafanya vizuri darasani na huwa tunatoa zawadi ya cheti na ngao ambayo hutambua juhudi za maendeleo kitaaluma kutoka chini hadi kufika juu,” anasema mwalimu huyo na kuongeza kuwa: “Ni muhimu kujua changamoto zao ili kuinua kiwango cha elimu.”

Ramadhani anasema kuwa hali hiyo inasababisha walimu wa shule za sekondari kutumia muda mwingi kuwajengea uwezo kwa kufundisha muda wa ziada ili wamudu masomo hususani katika mwaka wa kwanza wa kujiunga na masomo ya sekondari na wakati wa likizo kwa madarasa mengine.

Anasema hali hiyo ndiyo inayofanya baadhi ya shule za binafsi kupendelea kuchukua wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika masomo yao ya kuhitimu darasa la saba pekee. Anaongeza kuwa katika shule yao wanaona huo kama ubaguzi, ndio maana wanalazimika kuwapa nafasi wanafunzi wote na kuhakikisha wanawapika vya kutosha ili kumudu masomo ya sekondari.

Anafafanua kwamba shule ya Ihsan inajivunia kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanya kwa jamii, kwa kuwapika vijana kiasi cha vijana wote kupata daraja la I, II na III.

Anasema wana mikakati kabambe ya kuimarisha utoaji wa elimu ambayo ni bora zaidi kwa kuhakikisha wanawajenga wanafunzi wenye uwezo mdogo ili wawe na utayari wa kujifunza. Anasema hiyo ndiyo tofauti iliyopo kati ya Shule ya Sekondari ya Kiislamu Ihsan na nyinginezo.

Anafafanua kwamba kwa vile lugha ya kufundishia kwa elimu ya sekondari ni Kingereza, tatizo la kwanza wanalokumbana nalo ni weledi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kutokuwa na ufahamu mzuri wa lugha hiyo.

“Nikiri kwamba lugha ya Kingereza bado ni tatizo kubwa kwa wanafunzi wetu wanaohitimu darasa la saba hususan wale wanaotoka katika shule za msingi zinazotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia.

“Hivyo, serikali ya awamu ya tano inalo jukumu la kusaidia kuboresha eneo hilo katika shule za msingi ili wanafunzi wanapojiunga na elimu ya sekondari wawe na uwezo wa kutambua kile wanachojifunza kupitia lugha inayotumika – Kingereza.

“Walimu wenye mafunzo hayo wapo ila nadhani serikali haijaweka mkakati maalumu kama ilvyokuwa zamani kwamba kunakuwa na walau wiki nane za kumjengea uwezo mwanafunzi kujua istilahi za msingi za somo husika ili kurahisisha mawasiliano baina ya mwalimu wa somo na mwanafunzi,” anasema.

Anasema kutokana na hilo, katika shule yao walimu hulazimika kuwa na programu maalumu ya kufundisha lugha hiyo kwa awamu mbili:

“Kwanza huwa na wiki nane kabla ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza ambayo huanza Oktoba hadi Desemba. Mpango wa pili hufanyika kila siku baada ya masomo ya darasani pamoja na ufundishaji vipindi vya ziada yakiwamo masomo mengine kama Hisabati,” anasema Ramadhan. Pia anasema mitihani ya mara kwa mara hufanyika ikiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wao wapya kumudu masomo.

Anabainisha kuwa Ihsan ni shule ya bweni na kwamba wamejitahidi kuweka miundombinu yote muhimu ya kujifunzia na kufundishia. Anasema imani ya shule yao ni kwamba wanafunzi wakijengewa uwezo mzuri hufanya vyema na kwamba hilo wanalitimiza kwa vitendo na hivyo wamekuwa wakitoa wanafunzi walioelimika vyema.

Mkuu huyo anasema shule yao ina walimu bora walioiva na ambao wako tayari kuwalea vijana, maktaba ya kisasa, maabara za sayansi, maabara ya kompyuta, chumba cha kiifadhio(saver room), madarasa ya kisasa pamoja na mtandao wa maji na umeme wa uhakika, vitu ambavyo vinawapa uhakika wa kutoa elimu bora.

Anasema menejimenti ya shule yake inajitahidi kuhakikisha inaajiri walimu wa kutosha na mahiri kwa kuwa ndio msingi mkubwa na muhimu katika kuwapa wanafunzi elimu.

“Kwetu sisi tunajitahidi kuwa na walimu mahiri waliotoka vyuo vikuu kwa kuwa tunaamini wanao uwezo mkubwa zaidi wa kufundisha na kutuletea mafanikio kwa matokeo ya kidato cha pili, nne na sita kama yalivyo sasa.

Anasema kwa misingi hiyo, changamoto inabakia kwa wanafunzi ambao kama nilivyosema baadhi yao msingi wao walioupata kwenye elimu ya msingi si mzuri.

Anasema pamoja na hayo katika kuwajengea uwezo walimu wao na kuwafanya watekeleze majukumu yao kwa ufanisi, wamekuwa pia wakishiriki katika mafunzo mbalimbali na kufanyiwa tathmini ya mara kwa mara.

“Tunafanya tathmini ya namna walimu wanavyofundisha na wanafunzi wanavyopokea maarifa na stadi mbalimbali. “Haya yanafanyika na tunategemea kupata matunda,” anasema.

Anataja jambo jingine linalohimizwa na shule hiyo kuwa ni nidhamu, kwani wanaamini kwamba bila nidhamu si rahisi mwanafunzi kumudu vyema masomo yake na mwishowe kuwa kijana aliyeandaliwa kuwa kiongozi mwema katika umma. Katika kufikia azma hii, shule inahimiza na kujenga mazingira ya wanafunzi kupata mafunzo ya dini ya Kiislam.

Anasema mwanafunzi wa shule hiyo anajengewa kuheshimu taratibu za shule, sheria za nchi, hofu ya Mungu na kuwa tayari kujitolea kwa ajili ya taifa na jamii yake kwa ujumla.

“Tunaandaa wanafunzi ambao wameiva kiakili, kiroho, kimwili na nidhamu ili waweze kuwa wanajamii ambao watashiriki kuleta maendeleo ya taifa kwa namna moja au nyingine,” anasema.

Anasema shule hiyo pia inajielekeza katika kumfanya mwanafunzi awe na utayari wa kuchukua hatua muhimu ya kujenga uwezo wake na wenzake, uwezo unaolenga katika kuondokana na umaskini, maradhi na ujinga.

Anataja michepuo wanayotoa kuwa ni Sayansi, Sanaa  na Biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles