BADI MCHOMOLO
KIING Stephen Curry ni jina kubwa sana katika jiji la California, kutokana na staa huyo kile ambacho amekuwa akikifanya kwenye mchezo wa Kikapu katika Ligi Kuu ya NBA nchini Marekani akiwa na timu yake ya Golden State Warriors.
Mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakiamini bila ya uwepo wake uwanjani timu inakuwa kwenye wakati mgumu sana, haina tofauti na mchezaji wa soka katika klabu ya Barcelona ambapo wanaamini bila ya staa wao Lionel Messi mambo yanakuwa magumu.
Katika kipindi cha miaka mitano iliopita Stephen Curry alikuwa na mchango mkubwa wa mafanikio ya timu hiyo, huku wakichukua ubingwa mara tatu na yeye akichukua tuzo ya mchezaji bora wa mwaka MVP mara mbili, ndipo wakaona wamuite King.
Alistahili kuitwa hivyo hasa kutokana na aina yake ya mitupo, alikuwa mmoja kati ya wachezaji ambao wanaweza kuwa na pointi nyingi mara baada ya kumalizika.
Msimu uliopita ambao umemalizika Juni mwaka huu timu hiyo iliweza kufika fainali dhidi ya Toronto Raptors kutoka nchini Canada, lakini King Curry na kikosi chake kilikubali kichapo kwenye michezo minne hivyo kuwafanya Toronto Raptors kuwa mabingwa.
Jambo ambalo liliwaumiza Golden State Warriors na kuahidi kwa mashabiki zao kuwa msimu huu watahakikisha wanaleta furaha, lakini hali imeanza kuwa tofauti msimu huu mpya baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye michezo ya Playoff.
Mbali na kuanza vibaya, lakini mashabiki walikuwa na matumaini makubwa kwamba wanaweza kuinuka muda wowote, ila matumaini hayo yameanza kuingia nyongo baada ya staa wao huyo King Curry kuvunjika mkono wa kushoto mapema wiki hii wakati wa mchezo dhidi ya Phoenix Suns kwenye uwanja wa Chase Center.
Katika mchezo huo Golden State Warriors walikubali kichapo cha vikapu 121 kwa 110. Habari kubwa haikuwa kichapo, ila ilikuwa kuumia kwa staa huyo.
King Curry aliumia wakati anajaribu kumiliki mpira na kutaka kuwatoka wachezaji wa Phoenix Suns, Kelly Oubre Jr na Aron Baynes, hivyo kujikuta akianguka chini na wachezaji hao kumlalia juu yake.
Alionekana kuugulia maumivu na kisha kutolewa nje kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini hakuonekana kama ameumia sana kwa kuwa alitoka nje huku akiwa ameng’ata jezi yake mdomoni, ila baada ya kufanyiwa vipimo akagundulika kuwa amevunjika mkono wa kushoto.
Taarifa ambayo imewashtua wengi kutokana na safari iliobakia kwenye michuano hiyo kwa upande wa Playoff timu za Western Conference. Hata hivyo haijawekwa wazi muda ambao mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja.
Huo ni mtihani mkubwa kwa Golden State Warriors ambayo itakuwa inaikosa huduma ya aliyekuwa nyota wao misimu kadhaa iliopita Kevin Durant, ambaye aliondoka baada ya kumalizika kwa msimu na kujiunga na timu ya Brooklyn Nets.
Sehemu kubwa ya kulaumiwa Golden State Warriors ni kitendo cha kumuacha Durant akiondoka wakati ni mmoja kati ya wachezaji waliokuwa wanatengeneza umoja na King Curry, wakaona bora wamsajili D’Angelo Russell akipishana na Durant ndani ya kikosi cha Brooklyn Nets.
Wakamuacha nyota mwingine Andre Iguodala ambaye alikuwa hapo kwa misimu sita kabla ya mwaka huu kwenda kujiunga na Memphis, wakati huo mkali wao mwingine ambaye walikuwa wanamtegemea Klay Thomson kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuumia kwenye mchezo wa fainali ya sita dhidi ya Toronto Raptors. Anasumbuliwa na goti, hivyo anaweza kuonekana viwanjani kuanzia Februari mwakani.
Hii sio mara ya kwanza kwa King Curry kuumia, Novemba 8, alipata tatizo la nyonga jambo ambalo lilimfanya akose michezo 11, hivyo ikatajwa moja ya sababu ya timu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwenye fainali.
Kwa upande mwingine bado ni mapema kwa kukata tamaa ya ubingwa, wapo wachezaji ambao wanaweza wakaziba nafasi hiyo na kuwashangaza mashabiki kama ilivyo kwa timu ya Chicago Bulls mwaka 1997 dhidi ya San Antonio Spurs, baada ya kuwakosa baadhi ya mastaa wao, lakini waliweza kuishangaza michuano hiyo.
Kutokana na ubora wa kocha wa Golden State Warriors, Steve Kerr, timu hiyo inaweza kuendelea kufanya vizuri na kuna uwezekano wa kumtumia staa wake Draymond Green katika nafasi ya King Curry na kuleta matokeo.