25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Kinana ammwagia sifa Lowassa

Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amemmwagia sifa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa ni miongoni mwa viongozi waliotekeleza kikamilifu ilani ya chama hicho.
Kinana ambaye yupo mkoani Arusha kwa ziara ya chama hicho ya siku tisa, aliyasema hayo yeye na msafara wake alipopokewa katika Kata ya Makuyuni Wilaya ya Monduli.
“Napenda kumpongeza mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya katika jimbo hili….maendeleo yote hapa hayakosi mkono wa Lowassa,” alisema Kinana.
Wakati akimsifu, Kinana alikwenda mbali na kuzungumzia suala la kustaafu ubunge jambo ambalo halijawahi kuzungumzwa na Lowassa mwenyewe.
Katika hilo, Kinana alisema kuwa Lowassa anastaafu ubunge wake kwa heshima kubwa.
“Ndugu Lowassa ameamua kustaafu ubunge, anaondoka kwa heshima kubwa…tunashukuru sana ndugu Lowassa,” alisema Kinana.
Lowassa ambaye amekuwa mbunge wa Jamhuri tangu mwaka 1990 na baadaye mwaka 1995 kuwa mbunge wa Jimbo la Monduli,anatajwa kuwa miongoni mwa makada wa CCM wenye matamanio na kiti cha urais.
Ingawa yeye mwenyewe hajawahi kutangaza iwapo atagombea kiti cha urais baadaye mwaka huu, hata hivyo jina lake limekuwa likitajwa sana kuwa ni miongoni mwa wana-CCM ambao watachukua fomu kuwania nafasi ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Kabla ya kuzungumzwa na Kinana, taarifa za Lowassa kustaafu ubunge zimeibua mjadala mpana hasa aina ya mtu ambaye ataweza kumrithi na kuendeleza harakati zake katika Jimbo la Monduli.
Tayari majina ya wanachama watano wanatajwa kupambana kutaka kurithi mikoba ya Lowassa katika Jimbo la Monduli.
Wanachama hao ni pamoja na Daniel Porokwa, Loota Sanare, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM),Namelok Sokoine, Isaack Joseph “Kadogoo” na Julius Kalanga.
Hata hivyo, hivi karibuni viongozi wa mila wa Kabila la Wamasai (Laigwanani), Wilaya ya Monduli waliibuka na kusema wapo tayari kumuunga mkono, Namelok Sokoine, endapo atatangaza nia kugombea ubunge wa Monduli licha ya baadhi yao kumpinga kugombea.
Wakitoa tamko hilo Monduli hivi karibuni,walisema kumuunga mkono Namelok itakuwa sehemu muhimu ya kuenzi uongozi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine.
Katika kikao chao, viongozi hao walidai taarifa zilizotolewa hivi karibuni na vyombo vya habari (sio MTANZANIA) zikidai hawamuungi mkono Namelok si za kweli.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wenzake, Katibu wa Malaigwanani wilayani humo, Buluka Ngaimerya kutoka Kijiji cha Nanja, Kata ya Lepurka, alisema wao kama viongozi hawatambui kauli zilizotolewa na baadhi ya wanaojiita viongozi wa Malaigwanani wilayani humo.
Kauli kama hiyo iliungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa Malaigwanani wilayani humo, Mohammed Mebukori Perekeri, ambaye alisema hawaoni sababu ya kumkataa Namelok kama atatangaza nia.
“Sasa tunasema hivi, hata wakiweka koti la hayati Sokoine sisi tupo tayari kulipigia kura kwa lengo la kuenzi uongozi wake,” alisema Perekeri ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Monduli na kuongeza:
“Namelok akiwa mbunge wa jimbo kuna ubaya gani, kwetu sisi itakuwa ni heshima kubwa katika jamii na nje ya jamii. Mbona majimbo mengine wapo wabunge wanawake kwanini isiwe Monduli.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles