Kinamama wajawazito wanajifungulia chini ya sakafu

0
744

Abdallah Amiri, Igunga

BAADHI ya wajawazito wanaokwenda kujifungua Hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wanalazimika kujifungulia chini na kulala kitanda kimoja wawili kutokana na upungufu wa majengo na vitanda.

Hali hiyo, imebainishwa na mmoja wa wajawazito, Mwasiti Juma alipozungumza na gazeti hili mjini Igunga mwishoni wa wiki.

Alisema pamoja na hospitali hiyo kutoa huduma nzuri kwa kina mama wanaokwenda kujifungua, bado kuna shida ya upungufu wa majengo na vitanda.

“Tunashida kina mama,tukienda kujifungua unakuta kila kitanda tunalala wawili wawili, tunalazimika kujifungulia kwenye sakafu,”alisema.

Alisema hali hiyo ikiendelea inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa kwa watoto wachanga unaweza kutokea.

Pia mama mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema kuna upungufu wa majengo ya wodi za kina mama kutokana na kupokea wajawazito wengi  kutoka mikoa ya Singida, Shinyanga na  Simiyu.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Ruta Deus alithibitisha kina mama kujifungulia chini na kulala kitanda kimoja wawili wawili.

Alisema hali hiyo inatokana na ubora wa huduma wanayoitoa wamekuwa wakipokea wajawazito wengi kutoka mikoa ya jirani.

Alisema wodi iliopo inao uwezo wa kulaza wajawazito 18 kwa siku, lakini kutokana na wingi wa wajawazito wanaokwenda kujifungulia hapo wastani wa kila siku wanapokea 40.

Alisema kutokana na changamoto hiyo, tayari wametenga Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wajawazito na kuwataka kuwa wavumilivu kwa sababu Serikali imejipanga kikamilifu kuboresha huduma kwa mama na mtoto sambamba na maeneo yote ya afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here