27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

KINACHOSABABISHA KIFO CHA GHAFLA HIKI HAPA

Madaktari wakimfanyia mgonjwa upasuaji kwa ajili ya kuzibua mishipa ya damu iliyoziba.

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MIAKA ya nyuma ilikuwa ni nadra kusikia mtu amefariki dunia ghafla hasa akiwa usingizini, wazee wetu waliishi maisha marefu kuliko ilivyo miaka ya sasa.

Waliishi maisha ya kiasili ambayo yaliwasaidia kujiepusha kupata maradhi mengi. Leo hii maisha yamebadilika mno… wengi wanapenda kuishi kisasa bila kujua tunajiumiza wenyewe miili yetu.

Siku hizi si ajabu tena kusikia mtu amefariki ghafla usingizini, kifo cha namna hiyo huwa kinauma mno na kuliza wengi.

Mtindo mbovu wa maisha tulionao miaka ya sasa unatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.

Watu wengi hupenda kula vyakula visivyokuwa vya asili, hawafanyi mazoezi wala kupima afya mara kwa mara kujua mwenendo wake.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Pedro Pallangyo anasema kutozingatia ulaji bora, kutokufanya mazoezi na kupima afya ni hatari kwa afya zetu.

Wengi hufa usingizini

Anasema vifo vingi vinavyotokea watu wakiwa usingizini, sababu yake kuu huwa ni kuziba kwa mishipa ya damu.

“Tatizo la kuziba mishipa ya damu tulizoea zamani lilikuwa linazikabili zaidi nchi zilizoendelea pekee, lakini sasa ni tatizo kubwa hadi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania,” anasema.

Anasema tatizo hilo lilikuwa nchi zilizoendelea kwa sababu ndipo ambapo kulikuwa na sababu hatarishi zinazosababisha mishipa kuziba kuliko nchi zinazoendelea ambako hazikuwapo.

“Sababu hatarishi zinazotajwa hapa ndizo hizo, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, kutokufanya mazoezi, unywaji wa pombe kupita kiasi na kuvuta sigara.

“Nyingine ni uzito mkubwa kupindukia kulinganisha na urefu wa mtu husika, magonjwa ya shinikizo la damu na sukari,” anasema.

Dk. Pallangyo anaosema vitu vyote hivi vinapokuwa kwa mtu ndivyo hujiongezea hatari ya kupata tatizo la kuziba kwa mishipa ya damu.

“Yaani unakuta mtu ni mvutaji wa sigara wakati huo huo ana kisukari na shinikizo lake la damu lipo juu, mtu huyu uwezekano wa kupata tatizo la kuziba kwa mishipa yake ya damu lazima utaongezeka,” anasema.

Anasema visababishi vyote hivyo huashiria kuongezeka kwa kiwango cha mafuta kwenye damu.

Anasema athari za kuwapo kwa kiwango cha mafuta kikiwa kingi kwenye damu kwa muda mrefu huwa hakijitokezi mapema kwa watu wengi.

“Miaka ya nyuma, wengi walianza kuona athari za mafuta kwenye damu mara walipofikisha umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea. Lakini leo hii athari zinajitokeza zaidi kwa watu walio katika umri wa ujana, yaani chini ya miaka hiyo,” anasema.

Dk. Pallangyo anasema kadri mafuta yanavyotanda mwilini hupunguza uwazi wa damu kupita au huziba kabisa na hivyo damu kushindwa kupita.

“Kwa kawaida mshipa wa damu hautakiwi kuwa na mafuta yeyote lakini uwazi unapokuwa umezibwa kwa kiwango cha asilimia 50 na kuendelea, huyu mtu lazima apate shida kwa sababu damu inakuwa inapita chini ya asilimia 50 inavyotakiwa,” anasema.

Anaongeza; “damu inapokuwa inapita chini ya kiwango cha asilimia 50 au kuendelea, ni lazima tumfanyie uchunguzi mgonjwa na kumfanyia upasuaji ili kuzibua mishipa iliyoziba.

Ushuhuda wa mgonjwa

Faustine Mwandike ni miongoni mwa wagonjwa waliofanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na tatizo hilo ambapo tayari amefanyiwa upasuaji wa kuzibuliwa mshipa wake wa damu uliokuwa umeziba.

Anasema kabla hajachukua hatua ya kwenda hospitalini, alianza kuhisi maumivu makali katika upande wa kushoto wa mwili wake (kwenye moyo).

“Maumivu hayo yalikuwa yakijirudia mara kwa mara, baadae nilianza kuona mkono wangu wa kushoto unapoteza nguvu na maumivu yalikuwa yakishuka wakati mwingine hadi kwenye miguu,” anasimulia.

Anasema ilifika mahali akawa anashindwa kumudu kuendesha vema gari lake kwani maumivu hayo yalikuwa makali mno.

“Nikachukua hatua ya kwenda hospitalini, nikaanza kufanyiwa vipimo mfululizo tangu Januari 11, mwaka huu, madaktari waliona kuna umuhimu wa kuchunguza moyo wangu hasa mishipa ya damu.

“Waligundua tatizo lilikuwa ni kuziba baadhi ya mishipa ya damu, mmoja ulikuwa umeziba kwa kiwango cha asilimia 66 na mwingine ambao ni wa kuingiza na kutoa damu kwenye moyo uliziba kwa asilimia 80,” anasema.

Anasema baada ya uchunguzi huo alirejea jijini Arusha kwenye makazi yake na kwenda moja kwa moja JKCI, Januari 23 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.

“Kulikuwa na kambi ya upasuaji, Januari 25, nilifanyiwa upasuaji na mishipa hiyo ikazibuliwa, namshukuru Mungu sasa ni mzima,” anasema.

Sababu

“Ni mfumo mbovu wa maisha niliokuwa nikiishi na nadhani kama nisingewahi kufika hospitalini basi hali yangu ingekuwa mbaya zaidi kwani mishipa mingi ingeziba, sasa nafuata ushauri wa madaktari kuzingatia mtindo bora wa maisha,” anasema.

Dalili za tatizo

Dk. Pallangyo anataja dalili ya kwanza ni mtu kulalamika kuhisi  maumivu ya kifua upande wa moyo mara kwa mara hata akifanya shughuli nyepesi.

“Kawaida mtu akifanya shughuli yoyote mahitaji ya damu yanakuwa makubwa, sasa yanapoongezeka damu haiwezi kupita kwa sababu ule uwazi wake umeshapunguzwa kutokana na hayo mafuta,” anasema.

Anasema baadae mtu hupata mshtuko wa moyo hatimaye kufariki ghafla.

“Dalili hizi huwa ni muendelezo, huanza kupata maumivu ya kifua, mshituko hatimaye kufariki ghafla, hali hii hutokea pale ambapo mshipa unakuwa umeziba kwa asilimia 100, damu hushindwa kabisa kwenda kwenye moyo na katika sehemu zingine za mwili. Mshipa unapoziba damu na hewa ya oxygen huwa zinashindwa kupita,” anasema.

Wengi wanaugua

Daktari huyo anasema kila siku watu watatu hadi saba hufika katika taasisi hiyo na kufanyiwa uchunguzi na wanaokutwa na tatizo hufanyiwa upasuaji wa kuzibuliwa.

“Idadi hii kwa wiki ni sawa na watu 35 na kwa mwezi ni sawa na watu wapatao 140. Kwa mwaka jana pekee tuliwafanyia uchunguzi watu wapatao 400 katika mtambo wetu wa ‘cath lab’ kati yao asilimia 45 waligundulika kuwa na tatizo,” anasema na kuongeza kuwa mishipa ilikuwa imeziba kwa kiwango ambacho walihitaji kuzibuliwa au kuwekewa mrija (stand) kuizibua.

Anasema hata hivyo si wote ambao hufanyiwa upasuaji bali wale ambao mishipa yao imeziba kwa kiwango cha asilimia 50 na kuendelea.

“Wale ambao huwa imeziba chini ya kiwango hicho huwa tunawapa dawa za kutumia,” anasema.

Ushauri

Anasema kwa kuwa tabia hatarishi zinazosababisha tatizo hili zinaepukika watu wabadili mtindo wa maisha.

“Matibabu yake ni gharama kubwa, wanaomudu ni wale wenye bima, kipimo na upasuaji hufikia hadi Sh milioni nne, wengi wasiokuwa na bima hushindwa kumudu hivyo ni vema wakakate sasa,” anashauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles