25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kinacho mtesa Neymar ni wembamba wa miguu

Badi Mchomolo Na Mitandao

KABLA ya kufungwa kwa dirisha la usajili barani Ulaya uhamisho ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa ni nyota wa PSG, Neymar Jr kurudi katika klabu yake ya zamani ya Barcelona au kujiunga na mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid.

Klabu hizo mbili zipo vitani kupambana kuinasa saini ya mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba wa kuitumikia PSG hadi 2022, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kufikia muda wa kumaliza mkataba wake baada ya uongozi wa timu hiyo kuchoshwa na tabia zake.

Neymar Jr ni mchezaji ambaye hadi sasa ameweka rekodi ya usajili akitokea Barcelona mwaka 2017 na kujiunga na PSG kwa uhamisho wa kitita cha pauni milioni 198, lakini kwa kipindi cha muda mchache aliokaa sasa anataka kuondoka.

Kuondoka kwa Neymar ndani ya PSG kuna mambo mengi nyuma yake, miongoni mwake ni kushindwa kuelewana na baadhi ya wachezaji wenzake, viongozi na majeruhi yanayomsumbua.

Majeruhi makubwa ambayo ameyapata akiwa na PSG ni kuanzia Februari 2018, Junari 2019 na Juni 2019. Kuumia kwa vipindi hivyo kumemfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Timu nyingi haziwezi kusajili mchezaji ambaye ni majeruhi, tena majeruhi hayo hayajulikana yatadumu kwa muda gani, wakati mwingine hawawezi kumsajili mchezaji ambaye mara kwa mara amekuwa akiumia.

Neymar sasa ni mchezaji ambaye anaonekana hawezi kukaa muda mrefu bila ya kuumia tofauti na ilivyo wakati anakipiga Barcelona, kitendo hicho kinawafanya viongozi wa PSG kuona haina haja ya kuendelea kuwa na mchezaji wa aina hiyo ikiwa pamoja na sababu nyingi.

Kwa sasa Neymar anasumbuliwa na mifupa ya vidole ambapo aliumia Juni mwaka huu ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Copa America ambayo imefanyika nchini Brazil.

Tangu kuumia huko hadi sasa bado hayupo sawa japokuwa ameanza mazoezi wakati huo akisubiri kundoka wakati huu wa kiangazi.

Kwa mujibu wa daktari mkuu wa zamani wa timu ya PSG, Eric Rolland, ameweka wazi kuwa, Neymar ataendelea kusumbuliwa na tatizo hilo la kuumia mifupa ya vidole kutokana na miguu yake kuwa miembamba.

Kitaalamu inasemekana mchezaji mwenye miguu miembamba ana nafasi kubwa ya kuumia mara kwa mara mifupa inayounga vidole kwa kuwa inakuwa karibu na ngozi, hivyo ikiguswa kwa nguvu inakuwa na tabia ya kutawanyika kwenye sehemu zake za kawaida.

“Miguu ya Neymar ndio tatizo, amekuwa na miguu miembamba hicho ni chanzo cha mchezaji huyo kupata tatizo kama hilo la kuumia mifupa ya vidole mara kwa mara.

“Kama miguu ni miembamba mifupa hiyo ikigongwa kwa nguvu inaumia kwa haraka kwa kuwa inakosa nyama za kuweza kuizuia, hivyo inajitawanya, wapo wachezaji wenye miguu kama ya Neymar lakini hawajakutana na tatizo kama hilo, wakikutana litawasumbua,” alisema Rolland.

Hata hivyo, daktari huyo aliongeza kwa kusema, mchezaji wa aina hiyo anatakiwa kukaa nje kwa muda mrefu ili aweze kupona kabisa, lakini akirudi viwanjani mapema ni rahisi kupata tatizo kama hilo mara kwa mara.

“Kwa sasa Neymar ameanza mazoezi lakini bado hajacheza michezo ya ushindani, kutokana na aina ya miguu yake ni rahisi kuumia tena mifupa ya vidole kama hajapona vizuri.

“Anatakiwa kutumia muda mrefu kufanyiwa matibabu ili mguu uweze kuwa sawa, lakini kama atarudi uwanjani mapema kuna uwezekano wa kuendelea kuumia mara kwa mara,” alisema.

Neymar ni mmoja kati ya wachezaji wa kizazi cha sasa ambaye alipewa nafasi kubwa ya kuwa mfalme wa soka nchini Brazil baada ya mastaa mbalimbali kutikisa kama vile Ronaldo de Lima, Ronaldinho Gaucho, Kaka na wengine.

Kutokana na majeraha anayokumbana nayo, wengi wanaamini ndoto za mchezaji huyo kuwa mfalme nchini Brazil haitokamilika kwa kuwa umri wake unazidi kuwa mkubwa akiwa na miaka 27 sasa, lakini anakumbwa na majeraha ya mara kwa mara.

Alitakiwa kuwa na mafanikio makubwa akiwa na umri mdogo, lakini majeruhi yanaweza kupunguza thamani yake.

Mbali na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, Real Madrid na Barcelona zinatoana jasho kuwania saini ya mchezaji huyo raia wa nchini Brazil.

PSG wanadai thamani ya mchezaji huyo ni pauni milioni 206, ila wamewataka Barcelona kuweka mezani kiasi cha pauni milioni 93 pamoja na wachezaji watatu akiwa Philippe Coutinho, Ivan Rakitic na Nelson Semedo, lakini Barcelona wamedai hawezi kutoa wachezaji wote hao.

Madrid wao wamedai wapo tayari kumsajili mchezaji huyo kwa kitita cha pauni milioni 110 pamoja na kuwapa PSG wachezaji wawili. Kazi kubwa ya PSG ni kuangalia ukubwa wa ofa lakini kwa upande wa Neymar mwenyewe ameonesha dalili za kutaka kurudi Barcelona.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles