31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Kina Zitto wawatia mbaroni vigogo TPDC

TPDCNa Fredy Azzah, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Michael Mwande na Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo, James Andilile, wametiwa mbaroni baada ya kukaidi amri ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotaka kukabidhiwa mikataba 26 ya gesi kwa takribani miaka mitatu sasa.

Vigogo hao walikamatwa jana Dar es Salaam katika ofisi Ndogo za Bunge walipokutana na kamati hiyo ambayo ilikaa kama mahakama.

Tangu mwaka 2012, PAC imekuwa ikiomba kupewa mikataba hiyo hatua ambayo imewahi kusukuma viongozi wa Serikali bungeni kusema mbunge anayetaka kuiona mikataba hiyo, ipo wazi na wakati wowote anaweza kuiona.

Tangu kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge, TPDC imekutana na PAC mara kadhaa huku mara zote wakitoa sababu mbalimbali za kutowasilisha mikataba hiyo, ikiwa ni pamoja na kukwama kutekeleza adhima hiyo kwa sababu ya ukubwa wa mikataba na pia kusema hawawezi kufanya hivyo bila idhini ya wawekezaji.

Kufuatia hali hiyo, jana PAC ilikaa kama mahakama chini ya Mwenyekiti wake Zitto Kabwe, Makamu Mwenyekiti Deo Filikunjombe na Mwanasheria wa Bunge, Nenelwa Mwinambi.

Mwinambi alianza kwa kuwaapisha viongozi wa TPDC kabla kuanza kuwasomea vifungu vya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

Baadhi ya vifungu walivyosomewa ni pamoja na vile vinavyolipa Bunge ama Kamati ya Bunge haki ya kupata taarifa kutoka kwa taasisi yoyote ya sheria.

Alisema kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2012, kamati hiyo imekuwa ikiomba kupewa mikataba 26 ya gesi jambo ambalo halijawahi kutekelezwa.

Alisema nyaraka ambazo haziruhisiwi kutolewa ni zile zinazohusu mambo ya jeshi na usalama pekee.

“Kamati imekuwa ikiomba mikataba 26 ya gesi na mapitio yake, kwa kipindi chote hiki (tangu 2012) hawajawahi kusema kama inahusiana na masuala ya kijeshi ama usalama,” alisema Mwinambi.

Baada ya maelezo hayo, Mwenyekiti wa PAC, Zitto, alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Andilile aeleze kama alikuwa na mikataba hiyo kama ambavyo aliagizwa na kamati hiyo.

Katika maelezo yake, alisema baada ya agizo la PAC la Oktoba 27 la kuwasilisha mikataba hiyo, waliwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa maelezo kuwa mikataba yote ya Serikali ipo chini yake hivyo walitaka kupata mwongozo.

Alisema pia waliomba ushauri kwa watu walioingia nao mikataba lengo likiwa ni kutoingiza nchi kwenye matatizo kama wangetoa mikataba hiyo na wawekezaji hao washitaki.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo alivyotakiwa kutaja mkataba mmoja ambao umewahi kutolewa kwa Kamati ya Bunge na Serikali ikashitakiwa, alisema hana kumbukumbu ya tukio kama hilo kutokea.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Mwande alisema hawajawasilisha mikataba hiyo na kuwa rejea zake walishaziwasilisha kwa Waziri wa Nishati na Madini na kuwa yeye ndiyo mwenye jukumu la kuziwasilisha bungeni.

Baada ya vigogo hao kuhojiwa, Mwinambi alisoma vifungu mbalimbali vya sheria ya kinga na mamlaka ya Bunge ikiwa ni pamoja na kile cha 31 (J) kinacholipa Bunge mamlaka ya kumtoza mtu aliyekiuka sheria hiyo faini isiyozidi Sh 500,000 ama kifungo kisichozidi miaka mitatu.

Alisema TPDC kutowasilisha nyaraka walizotakiwa tangu mwaka 2012, ni kuvunja sheria hiyo kwa kuwa wameifanya kamati hiyo ishindwe kutimiza majukumu yake.

Baada ya maelezo hayo, Zitto aliamuru watu wote kutoka nje ya ukumbi huo na kubaki yeye na wajumbe wa PAC.

Baadaye watendaji hao wa TPDC waliitwa tena ndani ya ukumbi huo wakiwa pamoja na askari polisi ambao nao awali walikuwa wametoka nje.

Muda mfupi baadaye, Mwande na Andilile walitoka wakiwa chini ya ulinzi wa polisi na kwenda kuhifadhiwa kwenye moja ya vyumba vya ofisi hizo kabla ya kupakiwa kwenye gari la polisi na kupelekwa kwenye kituo kikuu cha polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya viongozi wa TPDC kukamatwa na polisi, Zitto alisema wametumia mamlaka yaliyopo kisheria kutimiza majukumu yao na kuwa wataendelea kusimamia sheria.

“Tayari nimeshaandika barua kwenda kwa Spika Anne Makinda kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.

Pia aliliambia gazeti hili ni muhimu mikataba hiyo ikajulikana kwa umma kwani ina maslahi makubwa kitaifa.

Alisema wafanyabiashara walioingia mikataba hiyo na Tanzania, baadhi wanaiwasilisha kwenye mabunge ya kwao na karibu yote yanaiwasilisha kwenye masoko mbalimbali ya hisa dunia.

“Sasa kwanini sisi hapa Bunge kupewa hiyo mikataba iwe tatizo,” alisema.

Alisema mkataba wa Kampuni ya Statoil  uliovuja hivi karibuni, ulionyesha udhaifu mkubwa kwani wakati Serikali ilitakiwa kupata asilimia 80 na kampuni hiyo asilimia 20, mkataba huo ulionyesha mgawanyo wa mapato ni asilimia 50 kwa 50.

“Kwa hiyo, kwa mkataba huo wenyewe tumepoteza asilimia 30 ambayo ni dola za Marekani bilioni moja kwa mwezi ambayo ni karibu sawa na Sh trilioni moja kwa kila mwezi, sasa utaona ni kiasi gani hii mikataba ilivyo muhimu,” alisema.

Alisema mikataba hiyo 26 inamilikiwa na kampuni 18 tofauti.

Naye Filikunjombe, alisema licha ya kuwapo dalili ya Wizara ya Nishati na Madini na TPDC kubebana, aliahidi kuendelea kushughulikia suala hilo hadi mwisho.

Waachiwa na polisi

Hata hivyo taarifa zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewaachia huru, Mwanda na Andilile kusubiri  ufafanuzi wa Bunge kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Taarifa ya jeshi kwa vyombo vya habari ambayo ilisainiwa na Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Suleiman Kova, ilisema walishindwa kuchukua hatua zaidi ya hapo kwani shauri hilo halikuwa na mlalamikaji aliyekuja kufungua jalada na kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi hao wa TPDC.

“Viongozi hao walikamatwa kutokana na maelezo ya mashahidi wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambapo  Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe alisema wapelekwe polisi waende kusubiri mwongozo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye atawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maagizo ya mwisho,” ilisema taarifa hiyo.

“Hatimaye iligundulika kwamba katika sheria ya Haki Kinga na Madaraka ya Bunge sura ya 296 kifungu 12 (3) kinaonyesha kwamba mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali alitakiwa kwanza apendekeze kwa Spika wa Bunge juu ya jambo lolote aliloliona kama ni kosa, Spika akisharidhika kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa mezani kwake na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

3 COMMENTS

  1. Hongera Muheshimiwa Zitto, hivi ndivyo inavotaka kuzibitiwa watendaji wa serikali na serikali yake kwa ujumla.Naziomba kamati nyengine zifuate mwenendo wa kamati yako muheshimiwa Zitto kwa kuwafuatilia wale vijana wa CCM waliotumia madaraka ya chama chao kupiga Muheshimiwa Jajai Joseph Warioba kwani wanaeleweka na wachukuliwe hatua mmojammoja pamoja na wale waliowatuma. Nakumbuka kijana aliempiga Muheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alishughulikiwa na kumalizikia jela iweje hawa?

  2. Wamewaonea maana ulaji, utapeli, na kutuhumiwa ndiyo falsafa ya nchi yetu kwa sasa. Mnamo mwaka 2007 Viongozi Waandamizi 11 akiwemo: Rais Msitaafu Benjamini Mkapa, Rais Kikwete, Lowassa na wengineo walituhumiwa na Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willbrod Slaa lakini mpaka sasa hivi hawajakamatwa wala kushitakiwa. Hivyo, Ufisadi na uhujumu uchumi ndiyo falsafa ya nchi chini ya utawala wa C. C. M. Hivyo, ni bora na hawa waachwe wale mabaki yaliyobaki ni haki yao.

  3. MIMI SINA RAHA KWA JINSI VIJANA WA KITANZANIA WANAVYOFANYWA MANDONDOCHA, SIJUI NI NINI KWA KWELI INAWEZEKANA TANZANIA TUNALAANA! NINAWAOMBA MASHEHE NA MAASKOFO NA MAPADRI WOTE TUFANYE MAOMBI KUIOMBEA TANZANIA YETU AMBAYO KWA SASA INAONEKANA INAUZWA KWA BEI POA.SASA HAWA WAHESHIMIWA KWANINI WAMEKATAA KUTOA HIYO MIKATABA INAONEKANA HAIKUFANYIKA KWA UWAZI NA INAWEZEKANA INAMAJINA YA HAO VIONGOZI AU MAKAMPUNI YAO.

    HIVI KUMPIGA MTU KAMA WARIOBA HUONI KUWA HIYO NI LAAANA UNAIPATA, KWANINI TUNAPATA TAABU MBONA KULIKUWA NA PICHA INAMAANA TENDO LOTE LILIONEKANA VIZURI SANA. SASA NATOA USHAURI WA BURE NA WAKISAYANSI ZAIDI KUWA TUUKATAE UTAWALA HUU KWENYE UCHAGUZI TUKIANZIA KWENYE UCHAGUZI HUU WA SERIKALI ZA MTAA, NAOMBA SANA TUACHE KULALAMIKA TUJIANDIKISHE NA TUPIGE KURA HAPO NDIO MWISHO WA MCHEZO CCM BYEBYE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles