Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili wanaokabiliwa na kesi ya kutakatisha fedha wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokamilika.
Mbali na Kitilya ambaye pia Mwenyekiti wa Kampuni inayoshughulikia Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Miss Tanzania (1996), Shose Sinare na Ofisa wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon.
Kesi hiyo imetajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakalika huku Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi akidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa upelelezi wake haujakamilika na kwamba wanaelekea ukingoni kukamilisha.
Akijibu Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa alihoji ni ukingo gani huo ambao unazungumziwa na upande wa mashtaka.
Hakimu Shaidi aliutaka upande wa mashtaka kufanya jitihada za kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo ili hatma ya washtakiwa hao ijulikane na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 30, mwaka huu na kuutaka upande wa mashtaka kufanya jitihada kukamilisha upelelezi.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha ambapo Machi 2013 jijini Dar es Salaam walijipatia Dola za Marekani milioni sita, wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.