25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Kina Bulembo waonywa

Andrew Msechu – Dar es Salaam

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imeelezwa kusikitishwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi na makundi ya kisiasa na kijamii, zinazoashiria uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora nchini.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Mathew Mwalimu, alisema kauli hizo zimekuwa zikichochea kwa kiasi kikubwa wananchi kujichukulia sheria mikononi mwao kutokana na kutoridhishwa na vitendo vya baadhi ya wanasiasa.

Taarifa ya tume hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu Mbunge wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo kutoa kauli ambayo baadhi waliitafsiri kuwa inalenga kumtisha Mbunge wa Kigoma Ujiji, Zitto Kabwe.

Katika kauli yake, Bulembo alisema; ”kuna mtu mmoja aliyechukua maswala yetu ya ndani na kuyapeleka nje ya taifa, hafai kuruhusiwa kurudi na anafaa kuuawa pale alipo. Uhaini. Kile ambacho Zitto Kabwe amekuwa akilifanyia taifa hili ni uhaini.”

Bulembo alitoa kauli hiyo ikiwa ni baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuzungumzia kitendo cha Zitto kuandika barua kwenda Benki ya Dunia kuitaka kusitisha mkopo iliyokuwa itoe kwa Serikali kusaidia elimu.

Zitto alidai kutolewa kwa fedha hizo ni kukubali watoto wa kike kutengwa kutokana na kauli ya Serikali kuwa watakaopata mimba hawataendelea na masomo kwa mfumo wa kawaida.

Katika maelezo yake ya Januari 31, Spika Ndugai alisema anamshangaa Zitto kwa barua hiyo na kutaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatilia suala hilo kuona kama lina jinai ndani yake.

“(Rais wa Marekani, Donald) Trump ameshtakiwa kwa sababu alikuwa anakula njama na mataifa ya kigeni ili kuingilia maswala ya ndani ya Marekani. Tuna mbunge ambaye amekuwa akifanya vitendo kama vya Trump, kuna swala la uhaini hapo,” alisema.

TAARIFA YA TUME

Kutokana na kile kinachoonekana ni kukemea kauli kama hizo, tamko la tume hiyo linasema; “hivi karibuni kumesikika katika mitandao ya kijamii kauli mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya watu wakitoa kauli za vitisho dhidi ya wengine kutokana na kutofautiana kimtazamo.

“Aidha, makundi mengine yamejitokeza kupinga hatua hiyo na kuahidi kuchukua hatua ambazo hazitoi sura nzuri katika ustawi wa misingi ya haki za binadamu na utawala bora nchini.

“Kutokana na hali hiyo, tume inapenda kusisitiza juu ya umuhimu wa kuvumiliana na kutumia taratibu za kisheria katika kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayolalamikiwa.

“Kauli hizi zisipodhibitiwa zinaweza kupelekea pia uvunjifu wa amani na utulivu tulio nao hapa nchini.”

Jaji Mwalimu alisema tume inaviomba vyama vya siasa kusimamia kuwadhibiti wafuasi wao kutotumia lugha ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

“Sisi sote tusimame imara katika kupinga kauli hizo ili kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu, tunu ambayo tumekuwa nayo kwa muda mrefu,” alisema Jaji Mwalimu.

Tume hiyo imetoa onyo hilo kufuatia matukio ya hivi karibuni ya wanasiasa kutamka hadharani, wakitaka wale wenye mawazo mbadala wauawe.

WALIOTOA MATAMKO

Akizungumza baada ya mkutano wa chama mwishoni mwa juma, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Kenani Kihongosi alisema watu ‘walioichafulia’ jina Tanzania walifaa kuuawa.

”Tumewachoka watu wachache wasio na maana ambao wanalichafulia jina taifa letu, lakini pia tumechoka na wale wanaotumiwa na wakoloni.

”Natoa wito kwa vijana kuandika kuhusu mambo mazuri ambayo Serikali inafanya, lakini pia kutochoka kukosoa wale wanaokandamiza taifa letu, wao ndio maadui wetu wa kwanza na wanastahili kuuawa,” alisema Kihongosi.

Awali, kabla ya kauli hiyo ya Kihongosi, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Heri James alikaririwa akiwalaumu vijana wa CCM kuwaacha wanasiasa wa upinzani Zitto na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakitembea mitaani bila kubughudhiwa kwa madai kuwa wanataka kulipasua taifa kwa vitendo vyao vya kuhujumu Serikali na taifa.

Hata hivyo, Februari 3, James alikaririwa akitoa ufafanuzi wa kauli hiyo kwa kusema kuwa viongozi wengi wa upinzani wamekuwa wakiendekezwa kufanya upotoshaji bila kuchukuliwa hatua na vyombo husika.

Alisema alichokimaanisha katika hotuba yake ni kushangazwa na utamaduni wa wapinzani kuichafua Tanzania bila kuchukuliwa hatua na vyombo vya dola.

“Kuna kipindi walizusha CAG Profesa Mussa Assad (amestaafu) katekwa, walichukuliwa hatua? Ule uvumi wa rais wetu walichukuliwa hatua?

“Sasa sisi tutaingia kwenye mapambano kwa hoja, wakienda kutuchafua nje, tutawafuata huko huko,” alisema  James huku akikiri kauli za viongozi zinaweza kuhatarisha amani.

 Aliongeza; “Amani ya nchi hii imeshikiliwa na sisi viongozi, tukichochea uongo tutaharibu nchi hii.

“Alichokizungumza mwenyekiti wa Iringa siyo msimamo wa UVCCM na tunakemea kauli za aina hiyo, sisi msimamo wetu ni kuhimiza utekelezaji wa misingi ya kisheria.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles