24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kimbunga Lekima chatikisa China, 13 wapoteza maisha

WENLING, CHINA

WATU takribani 13 wamekufa na zaidi ya milioni moja wamelazimishwa kuondoka katika nyumba zao wakati kimbunga Lekima kikiikumba China.

Vyombo vya habari vya Serikali vimechapisha taarifa inayoeleza kuwa watu 16 hawajulikani walipo baada ya kimbunga hicho kuukumba mji wa Wenling .

Mji wa Wenling, upo katikati ya Taiwan na Jiji la kibiashara la Shanghai.

Awali kimbunga hicho kilielezwa kitakuwa kikubwa, lakini kilipungua baada ya kutokea kikielezwa kuwa na kasi ya kilomita 187 kwa saa (116mph).

Kimbunga hicho kimekuja wakati bwawa likivunjika kingo zake huko Wenzhou, karibu na mahali ambako kilitua.

Hadi kufikia jana mchana kilikuwa kimepungua kasi kikielekea jimbo la Zhejiang,  huku kikitarajia kuikumba Shanghai, jiji lenye watu zaidi ya milioni 20.

Kabla ya kimbunga hicho kutua, mamlaka za China zilikuwa zimejipanga na hata kilipotokea timu ya wafanyakazi wa dharura walikuwa wakionekana kuokoa waendesha magari  waliokuwa wamekwama  kwenye mafuriko.

Kimbunga hicho kimesababisha miti kuanguka na umeme kukatika katika maeneo mengi.

Inakadiriwa nyumba milioni 2.7 zimekosa umeme, kutokana na kuwapo kwa upepo mkali.

Katika jiji la Shanghai tayari mamlaka zilizuia zaidi ya maelfu ya safari za ndege  na huduma za treni ikiwa ni maandalizi ya kukabiliana na kimbunga hicho.

Pamoja na kwamba kinatarajiwa kufika Shanghai kikiwa kimepungua kasi lakini bado kinaweza kusababisha athari kutokana na mafuriko makubwa.

Wakazi takribani 250,000 wameokolewa, huku wengine  800,000 wa mji Zhejiang wakichukulia kutoka katika majumba yao.

Hiki ni kimbunga cha tisa kutokea ndani ya mwaka huu.

Shirika la habari la nchini China la Xinhua lilisema kuwa pamoja na kwamba kimbunga hiki ni cha tisa kwa mwaka huu lakini kilikuwa kikali.

Jana mchana mamlaka ya hali ya hewa nchini China ilisema kuwa kimbunga hicho kilikuwa kikiondoka kuelekea Kaskazini kwa kasi ya kilomita 15 kwa saa (9mph).

Awali wakati kilipopita Taiwani kilisabaisha madhara ikiwamo watu kujeruhiwa na mali nyingi kuharibika.

Kimbunga hicho kimekuja siku moja baada ya wataalamu kuonya juu ya kutokea kwa tetemeko lenye mgandamizo sita, hali ambayo kukutana kwa vitu hivyo viwili kwa pamoja kungesababisha mvua kubwa na maporomoko ya ardhi.

Wakati kimbunga Lekima kikiwa ni miongoni mwa vimbunga viwili vinavyotikisa sasa Magharibi mwa Pasifiki, upande wa Mashariki unatikiswa na kimbunga Krosa ambacho kimesababisha mvua kubwa katika visiwa vya Mariana na Guam.

Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa kimbunga hicho kinaelekea kaskazini magharibi na huenda kikaikumba Japan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles