24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

KIMBUNGA CHALETA MAAFA ZANZIBAR

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR


ZAIDI ya nyumba 70 zimeezuliwa mapaa kisiwani Unguja, Zanzibar baada ya kimbunga cha dakika 45 kutikisa.

Kimbunga hicho ambacho kimeathiri zaidi wakazi wa maeneo ya Kinuni na Nyarugusu, Wilaya ya Magharibi Unguja, kiliwafanya wananchi hao kushindwa kufanya lolote kutokana na hali hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wakazi wa eneo la Nyarugusu, Mohamed Khamis Issa, alisema kuwa hatua ya nyumba zao kuezuliwa na kimbunga hicho imewaacha wasijue la kufanya.

“Sijui tutaishi vipi leo, maana kwetu ni mtihani mkubwa, nyumba yangu pamoja na jirani zangu zote zimeezuliwa mapaa. Sijui kuna nini maana binafsi sijawahi kuona upepo mkali kama huu ambao sasa umesababisha athari kubwa kwetu.

“Tunaomba mamlaka za Serikali zitusaidie kwa haraka maana sasa tupo kwenye hatari hata ya kuibiwa. Ewe Mwenyezi Mungu tupe heri na ustahamilivu waja wako,” alisema Issa.

Kutokana na athari hiyo, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari.

“Sisi Serikali tupo pamoja nao wananchi wote walioathiriwa na kimbunga hiki. Tutatoa kila aina ya msaada uliopo ndani ya Serikali.

“Pia ninawapongeza wananchi waliopatwa na athari hizi kwa ushirikiano wa aina zote walioutoa kama ilivyotokea Pemba, ambapo pamoja na kusuguana katika siasa, lakini kwa tukio lililotokea la mafuriko wote walikuwa wamoja. Hakuna CCM wala CUF, wote walikuwa wamoja.

“Naamini sote tukiendelea na mshikamano huu wa kuwa wamoja, ikiwemo kuwasaidia wenzetu waliopatwa na maafa, hakika nchi yetu itasonga mbele,” alisema.

 Balozi Seif aliwapa pole viongozi wa Serikali wa eneo hilo kutokana na maafa hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles