23.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kimbau atua rasmi Ukawa

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omari Kimbau,  ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kimbau alisema ameamua kujiunga na CUF baada ya kuchoshwa na ubakaji wa demokrasia ndani ya CCM.

Kimbau ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa muda mrefu wa Mafia, Kanali Shomari Kimbau, alisema haki ya wananchi wa Mafia imetekwa na watu wachache wenye fedha.

“Mimi na familia yangu, rafiki zangu tumeamua kukihama CCM na kujiunga na CUF, hii ni baada ya kuchoshwa na genge la matajiri ambalo sasa limebaka haki ya wananchi wa Mafia,”alisema Kimbau.

Mwanachama huyo mpya wa CUF alikuwa ni mmoja wa  wagombea ubunge kupitia CCM na kushika nafasi ya pili katika kura za maoni.

Alisema pamoja  na kuamua kugombea kwa mapenzi yake lakini dhuluma na rushwa zilitawala katika uchaguzi huo.

Nia yake ya kuwakomboa wananchi wa Mafia iko pale pale kwani atagombea jimbo hilo kupitia CUF, alisema.

“Mwaka 2010 wakati nagombea ubunge yalitokea mambo kama haya ya rushwa lakini hata  nilipofuata taratibu kwa kukata rufaa sikusikilizwa, sasa mimi ni binadamu na nina roho na nyongo hivyo nimeamua kwa moyo wangu kuachana na CCM,”alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye pia alipata kuwa diwani wa Kijitonyama kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, alisema ndani ya CCM haki imekuwa haitendeki kwa vile  viongozi wa juu hupigania kuwapitisha watu wao wanaowataka.

“Refa anafanya kazi ya timu, washika bendera wanafanya kazi ya timu, vyombo vinabeba mgombea sasa katika mazingira kama haya unadhani timu itashinda kwa haki kweli,”alihoji Kimbau.

Alisema ameamua kujiunga na CUF kutokana na kaulimbiu yao ya haki sawa kwa wote.

“Kwanza nawashukuru CUF kwa kunipokea. Pia nilivutiwa zaidi na kaulimbiu yao ya haki sawa kwa wote,”alisema Kimbau.

Wakati huohuo,  Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema leo  Ukawa utatangaza matokeo ya mgawanyo wa majimbo yote nchini.

Pia alisema Kimbau atakuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Mafia kupitia Ukawa.

“Leo (jana) tulikuwa tumepanga kutangaza matokeo ya majimbo ya uchaguzi lakini bado mambo hayajawa sawasawa lakini kesho tutawaita na tutatangaza,”alisema Mketo.

Alisema Agosti 19 mwaka huu Katibu Mkuu wa chama hicho,   Seif Sharif Hamad atafanya ziara wilayani Mafia ambako atamkaribisha Kimbau na kuwapokea wanachama wa CCM ambao watajiunga na CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles