27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kilio watumia M-pesa, Tigo Pesa, Airtel Money

Atm Machine
Atm Machine

*Kila ukituma 1000/-  unakatwa kodi 280/-

*Wanaochukua fedha  kwenye ATM nao kuonja joto ya jiwe

Elizabeth Hombo na Johanes Respichius, Dar es Salaam

WACHAMBUZI na wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, huku watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu wakikumbwa na maumivu wa kodi.

Hiyo ni siku moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 20116/17.

Pamoja na mambo mengine, bajeti hiyo inapendekeza kuongeza ushuru wa vinywaji baridi, maji ya juisi, vinywaji vikali, bia na sigara.

Pia itawagusa watumiaji wa M-pesa, Tigopesa, Airtel Money, Ezypesa   kwa kukatwa Sh 280 kwa kila Sh 1000 watakayotuma.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema hatua hiyo ya Serikali kuendelea kutafuta kodi kwa kuzidi kuwaumiza wananchi inakwenda kinyume na matarajio ya Watanzania wengi.

Alisema katika bajeti hiyo ya Serikali na ukusanyaji wa mapato yake, katika kila Sh  1000 itakayokatwa kwa huduma kwenye ATM kuanzia Julai Mosi mwaka huu, Sh 280 zitachukuliwa na TRA.

Zitto alisema hali hiyo pia itawakumba watumiaji wa miamala ya M-pesa, Tigopesa, Airtel Money, Ezypesa ambalo ndilo kundi kubwa la Watanzania wanaotumia huduma hiyo nchini.

Aawali kodi ya bidhaa ilikuwa asilimia 10 lakini kwa hatua ya kuongezwa kwa kodi ya ongezeko la thamani kodi itapaa na kufikia asilimia 28.

Kwa mantiki hiyo, katika kila Sh 100 kodi ni Sh 28 na  katika Sh 1000 kodi ni Sh 280.

Kutokana na hali hiyo kodi ya VAT hulipwa na mtumiaji wa mwisho ambaye anatuma au kupokea fedha, hali ambayo itawaumiza watumiaji wa mwisho.

“Hivyo hivyo katika miamala ya M-pesa, Tigo pesa na kadhalika, katika kila Sh 1000 itakayokatwa kwa huduma kwenye ATM kuanzia Julai 1, 2016, Sh  280 zitachukuliwa na TRA,” alisema Zitto.

Alisema   ameshangazwa na hatua ya Serikali kuongeza kodi ya VAT kwenye utalii hali ambayo inaweza kusababisha Tanzania kupoteza watalii wengi kwa washindani wake kwa sababu itaongeza gharama kwa watalii.

“Kama tunataka kutumia utalii kama kichocheo cha ajira ni vema kufikiria upya suala hili,” alisema.

Akizungumzia mapendekezo ya Serikali katika Sheria ya Kodi ya VAT ili kutoza kodi bidhaa zinazotoka Zanzibar, alisema hatua hiyo inavunja misingi iliyowekwa na sheria ya zamani ambayo ilifanana na ile za Zanzibar.

“Ikumbukwe kuwa Sheria ya Kodi ya VAT ya 2014 ilivunja misingi iliyowekwa ya sheria ya zamani ambayo ilifanana na ile ya Zanzibar. Mapendekezo ya sasa yana madhara makubwa kwa Zanzibar kwa sababu  hakuna atayewekeza Zanzibar ili kufaidika na soko la Bara.

“Biashara nyingi zinazozalisha Zanzibar zitahamia Tanzania Bara. Mapendekezo haya yanaweza kusababisha  mgogoro kati ya pande mbili za Muungano,” alisema.

Kodi kiinua mgongo

Mbunge huyo alisema ni sahihi kwa wabunge kukatwa kodi hiyo kwa vile  ni pato ambalo ni lazima litozwe kodi.

“Mapendekezo ya kutoza kodi kwenye kiinua mgongo kwa wabunge ni sahihi kwa sababu  ni pato ambalo lazima litozwe kodi. Hata hivyo kiini ni kanuni ya kukokotoa kiwango kinacholipwa.

“Mabadiliko ya maana ni kufuata sheria kwenye kulipa na kutoza kodi. Vile vile, pato hili halipo mwaka ujao wa fedha na halitakuwapo mpaka mwaka 2020. Kwa nini lisemwe sasa, ni jambo la kushangaza kidogo!

“Nadhani pato linalopaswa kutozwa kodi ni posho ya vikao, hili ni pato kama pato jingine lolote na halilipiwi kodi. Sitting Allowance kwa watu wote wanaopata ikitozwa kodi kwa sababu inaonyesha haiwezi kufutwa  itarudisha fedha nyingi Serikalini,” alisema Mbunge huyo wa Kigoma Mjini

Profesa Baregu

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema bajeti hiyo ya Serikali ni ya matobomatobo.

Profesa Baregu, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), alihoji kama vyanzo hivyo vya mapato vilivyoorodheshwa vitazalisha huku kukiwa na deni la Sh trilioni nane.

Alieleza kushangazwa na kitendo cha makampuni makubwa ya madini kuachwa bila kuongezewa kodi.

“Hii ni serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Bajeti ya mwaka uliopita ilitekelezwa asilimia 60 tu yaani ilikuwa kiini macho.

“Tukija kwenye bajeti hii ya 2016/17 kwanza vyovyote vile lazima tuangalie malengo matatu kwa sababu bajeti ni utendaji; malengo ya serikali, mapato na matumizi.

“Kuna madeni kama Sh trilioni nane, tayari ina matobomaboto, imeongezeka kwa asilimia 30 zaidi ya ile ya mwaka jana.

“Maswali ya kuhoji, je hizo fedha watazipata wapi? Hivyo vyanzo vitaweza kuzaa vyanzo hivyo vya mapato? Kwa nini makampuni makubwa ya madini yameachwa bila kuongezwa kodi?” alihoji Profesa Baregu.

Mtatiro

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na mchambuzi wa masuala ya siasa, Julius Mtatiro alisema kipaumbele cha Rais John Magufuli ni viwanda lakini wizara inayohusika na sekta hiyo imepewa bajeti kidogo ambayo ni sawa na sifuri.

“Moja ya vipaumbele vikubwa ya bajeti ya sasa ni suala la viwanda. Lakini tumekwenda kwenye bajeti ya Wizara ya Viwanda imetengewa fedha kidogo sana ambayo ni sawa sawa na sifuri.

“Kwanza hawajabuni vyanzo vipya vya mapato vimeendelea kuwa vilevile vya kodi. Katika dhana hiyo hiyo hata katika maeneo yatakayoipatia fedha kama madini, hayaongelewi kabisa lakini bajeti yetu ni bia tu. Tulidhani hapa kazi tu ingekuja na utaratibu mpya,”alisema Mtatiro.

Katika muktadha huo, alisema makampuni matatu yanayozalisha bia   nchini yanalipa kodi   mara 10 ya makampuni yote ya madini nchini.

Kibamba

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba aliifananisha bajeti hiyo na ng’ombe wa maziwa anayekamuliwa sana hata kama hana maziwa.

“Bajeti imening’ata. Haya mambo ya kukamua ng’ombe yule yule kila siku mwishoni sasa unaweza ukakata chuchu za ng’ombe. Serikali ilipaswa ipanue wigo kwenye vyanzo vingine na kutegemea bia, sigara, na soda.

“Sikutegemea kama serikali hii ya awamu ya tano nayo ingerudi kule kule. Ng’ombe amenenepa kule kwenye migodi kuna misamaha ya kodi.

“Hakuna mifumo ya ufumbuzi wa biashara na hata   mtu akajitokeza kufanya biashara mpya anakatishwa tamaa…mara unakwenda halmashauri kulipa mara hivi… yaani unajikuta fedha nyingine imekutoka kabla hata hujaanza kufanya biashara.

“Hii tabia ya bajeti kutegemea kwenye bia itafika wakati watanzania wote wataokoka,”alisema Kibamba.

Sendeka

Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka, alisema bajeti hiyo ya Serikali inalenga kuwaondolea mzigo wananchi kwa kuwa fedha nyingi zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo.

“Mfano tumeona bajeti hii fedha zimeelekezwa katika barabara, reli ya kati, usafiri wa anga na vyombo vya majini vitu vyote hivyo ni faida kwa wananchi,”alisema Sendeka.

Alisema CCM kina imani na Rais John Magufuli  na kuwa fedha zote zitapatikana  na miradi yote ya maendeleo itatekelezwa kwa kuwa kiongozi huyo ni mfuatiliaji.

TGNP

Mtandao wa Jinsia Tanzania  (TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati mbalimbali ngazi ya jamii, wametoa tamko la maboresho na upungufu wa bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17.

Akizungumza   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Maendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, alisema licha bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongezwa,   bado haiwezi kuendana na hali iliyopo kwa sasa.

Alisema bajeti hiyo haijazingatia kumwezesha mama mjamzito kupata huduma za uzazi.

“Mfano vifaa vya kujifungulia havikupewa uzito wa kutosha pia ni vema serikali ikaondoa kodi zote kwenye vifaa kama pedi na taulo za kujihifadhia wanawake wakati wa hedhi hususan kwa wasichana walioko  shuleni,” alisema Mawinza.

Akizungumzia ahadi ya serikali kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji, Mawinza alisema kuliko serikali kutoa fedha hiyo kama mikopo ni bora ikazitoa kama ruzuku   kuwapunguzia wananchi madeni.

Kuhusu elimu bure, alisema jitihada za kutoa elimu bure ziendane na uchambuzi wa kina na uwekezaji wa rasilimali ambao utaondoa changamoto ambazo zimeanza kujitokeza.

“TGNP tunatoa angalizo kwamba juhudi za kutoa elimu bure ziendane na uchambuzi wa kina na uwekezaji wa rasilimali ambao utaondoa changamoto na kero ambazo zimeshaanza kwa watoto wa kike na wenye ulemavu,” alisema Mawinza.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha COTWU (T),  Idrisa Washington, ameitaka serikali kuangalia upya kodi za mishahara kwa wafanyakazi kwa kuwa imekuwa ikizidi kuwaumiza waajiriwa nchini.

Alisema ongezeko la kodi hiyo limekuwa mzigo kwa wafanyakazi hasa wale wa kipato cha juu hivyo kuna haja ya kuangalia namna ya kuwapunguzia mzigo huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles