24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

KILIO CHA WATU WENYE UALBINO KUTAKA TAKWIMU SAHIHI

Mwenyekiti wa TAS, Nemes Temba akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) hivi karibuni.

Na ASHA BANI,

LICHA ya kwamba ni miaka 37 sasa tangu Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) kianzishwe, bado ukosefu wa takwimu sahihi za idadi ya watu wenye ualbino inaonekana ni tatizo linalowanyima usingizi viongozi wake.

Kutokana na hilo viongozi hao wameamua kuibana serikali ieleze lini itakuja na takwimu sahihi ili jamii isaidie kuwalinda watu wa jamii hiyo.

Ikumbukwe kuwa Juni 13 ilikuwa kilele cha siku ya kimataifa ya Maadhimisho ya Watu wenye Ualbino Duniani, ambapo kitaifa ilifanyika mjini Dodoma.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilisema; ‘Umuhimu wa Takwimu na Tafiti kwa Watu Wenye Ualbino’, ikienda sanjari na mpango mkakati wa serikali kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika jitihada za kuhakikisha jamii yote ya Tanzania inakwenda pamoja.

Ili kufikia malengo hayo ni wazi kuwa takwimu sahihi za idadi ya watu wanaoishi na ualbino ni muhimu ili iwe rahisi kwa jamii kuwalinda na kuwatunza.

Maadhimisho ya mwaka huu yalikuwa ya 11 kufanyika hapa nchini, wakati kidunia ni mara ya tatu na kuonyesha kuwa Tanzania ilikuwa ya kwanza kutambua thamani na umuhimu wa kuwapo kwa watu wenye ualbino ulimwenguni.

Ndio maana hapa nchini, Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS), kilianzishwa rasmi mwaka 1980 kwa usimamizi madhubuti wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere.

Tangu wakati huo na hadi kifo chake mwaka 1999, Mwalimu Nyerere pamoja na mambo mengine alihakikisha watu wa kundi hili wanaishi kwa upendo na kuchangamana na makundi mengine katika kila jambo.

Ndio maana wakati huo haikushangaza Mwalimu Nyerere alisaidia chama hicho kila hitaji lake, licha ya kwamba ahadi ya kukipa gari moja aina ya Landrover haikutimia.

Mweka Hazina wa TAS, Abdilah Omari anasema ahadi hiyo ya mwalimu kwa chama chao iliamsha hamasa kubwa kwa sababu si tu alishiriki katika kuhakikisha kinasajiliwa, pia aliweka nguvu kubwa kwa jamii kuona watu wenye ualbino wanapata nafasi ya kusikilizwa.

“Katika harakati zake, kati ya mwaka 1981, 1982 Mwalimu Nyerere alijaribu kukutana na Ikulu na Msasani viongozi wa TAS na wa vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (CHAWATA), Chama cha Wasiooma Tanzania (TLB) Chama cha Wenye Ualbino Tanzania wakati huo kikiitwa CCMT, lakini sasa jitihada nyingi zimepuuzwa,” anasema.

Omari anasema wakati huo Mwalimu Nyerere kwa kutambua changamoto zilizoanza kujitokeza, aliweka utaratibu wa kuvisaidia vyama hivyo vifaa vya ofisi na kila kimoja alikipa ruzuku ya fedha Sh milioni tatu.

“Pamoja na ruzuku hiyo, Mwalimu Nyerere pia aliahidi kukipa chama chetu gari kwa ajili ya kufanikisha kwa ufanisi shughuli za kiutawala lakini kwa bahati mbaya ahadi hiyo haikutekelezwa na serikali iliyokuwa chini ya uongozi wake,” anasema.

Omari anasema huu ni wakati mwafaka kwa serikali kuweka wazi mchango wake wa moja kwa moja kibajeti ili kusaidia TAS kujiendesha bila wasiwasi.

Akizungumzia siku ya wenye ualbino ambayo ni kesho, Mwenyekiti wa TAS, Nemes Temba anasema kauli mbiu ya mwaka huu inakwenda sanjari na kauli ya kimkakati ya Hataachwa Mtu Nyuma.

Temba anasema, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kukabiliana na changamooto wanazokumbana nazo watu wenye ualbino, lakini amezungumzia kuwapo kwa sheria mbili za Takwimu na Makosa ya Mtandao.

“Sheria hizi ni nzuri lakini zina changamoto kubwa katika utekelezaji wake. Mfano, sheria Namba 9 ya Takwimu ya mwaka 2015 ambayo imeanza kutumika rasmi  Novemba 2, 2015 kupitia tangazo la serikali namba 461 la Oktoba 30, 2015,” anasema.

Temba anasema pamoja na nia njema ya kutungwa kwa sheria hii, lakini imeweka masharti magumu kwa wakusanya takwimu ambapo wote watakaojaribu kukusanya na kuchapisha takwimu zozote, ni lazima kwanza wapate kibali cha Ofisi ya Taifa ya Takwimu, jambo ambalo ni kikwazo kwao.

Anafafamua kuwa, kikwazo kinaibuka kwa makundi maalumu ya wahitaji wa takwimu hizo, ikiwamo TAS na kwamba, masharti hayo yanawazuia watu wengi wakiwamo waandishi wa habari kukusanya takwimu za wenye ualbino.

“Sheria nyingine ni Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ambayo inaweka masharti ya kudhibiti ukusanyaji, usambazaji na uchapishaji wa habari ambapo imeanza kufanyakazi miezi michache kabla ya siku ya maadhimisho yake kufika,” anasema.

Anasisitiza kuwa wakati sheria hizi zinaanza kutumika jamii ilikuwa bado haijazielewa vizuri, huku takwimu za idadi kamili ya watu wenye ualbino na kaya zao haifahamiki vizuri.

“Kwa mfano, katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, serikali imesema idadi ya watu wenye ualbino ilikuwa ni 16,376 wakiwamo wanaume 7,920 na wanawake 8,756, ambapo hiyo ilikuwa ni hatua kubwa kwa taifa maana ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kujumuisha watu wa jamii hiyo,” anasema.

Hata hivyo, Temba anahoji kama kweli idadi ni hiyo serikali inashindwaje kuwafikia watu hao na kuwasaidia huduma za msingi ikiwamo upatikanaji wa huduma za afya na chakula kwa wale wanaougua kiasi cha kushindwa kujifutia riziki.

Hata wakati huu ambapo inakadiriwa kuna ongezeko la watu kwa asilimia tatu kila mwaka tangu mwaka 2013, inakisiwa kuwa hivi sasa watu wenye ualbino wanafikia 18,033, wanaume 8,763 na wanawake 10,070. Lakini bado wanaishi kwa hofu ya kukosa ulinzi jambo ambalo linawafanya watu wa jamii hiyo kuwa na hamu kubwa kusikia serikali imejiandaaje sasa kukabiliana na hali hiyo.

“Watu wenye ualbino wanapoteza maisha kutokana na kuugua saratani ya ngozi kwa sababu ya kukosa matibabu. Hapa ndipo tunaposema maadhimisho hayo yanalenga zaidi kuhamasisha jamii kutambua juu ya mahitaji ya watu wenye ualbino,” anasema.

Meneja wa programu katika miradi wa TAS, Seveline Malya anasema si vibaya wakati wa maadhimisho hayo watu wanaosheherekea siku zao za kuzaliwa waungane na TAS katika kuifanya siku hii kuwa maalum zaidi kwao.

Anasema maadhimisho yalianza rasmi Juni 9 hadi siku ya kilele Juni 13, ambapo kulikuwa na Kliniki ya Macho na Ngozi kwa watu wenye Ualbino ambapo wataalam wakiwamo madaktari kwa Kichina wanaoishi nchini walitoa huduma bure.

“Shughuli hiyo ilifanywa katika Viwanja vya Nyerere Square sambamba na watalaamu wa afya wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambapo wametoa huduma katika viwanja hivyo wakisaidiana na maafisa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Chinese Medical Team kutoka Tanzania,” anasema Malya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles