22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kilio cha mkazi Kibiti dhidi ya waliomsababishia upofu

ASHA BANI – DAR ES SALAAM

“NATAMANI kuwa na uwezo wa kuona tena ili nirudi katika shughuli zangu za kujitafutia kipato. Awali nilikuwa na uwezo wa kuhudumia vizuri familia yangu kutokana na kipato nilichokuwa napata kwenye kazi ya udereva na kilimo.

“Tangu nipate ulemavu wa macho, nimekuwa nikiishi kwa kuomba omba  misaada kwa watu mbalimbali, jambo ambalo linanikwaza mno.”

Anaanza kuzungumza kwa masikitiko, Michael Buchayandi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Rondo, Kijiji cha Mangwi, Kata ya Mchukwi wilayani Kibiti.

Buchayandi alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana waliokuwa wakitekeleza mauaji wilayani hapo, Juni, 2017.

Akiwa ofisini kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Buchayandi anaeleza kwa uchungu huku akitokwa machozi, namna anavyoteseka na hali aliyonayo. Hivyo, anaomba msaada wa hali na mali ili aondokane na matatizo anayopitia hivi sasa.

Anasema watu wasiojulikana walimpiga risasi kwenye jicho la kulia na kumpiga na kitu chenye uzito katika jicho la kushoto hivyo, kumsababishia macho yake kupoteza uwezo wa kuona.

Buchayandi ambaye ana mke anayemtaja kwa jina la Selina Mponyi, na watoto wanne, anaomba wasamaria wema wamsaidie kupata fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba yake, ili apate makazi ya kudumu na si kutangatanga, hasa ukizingatia hali aliyonayo kiafya.

Pamoja na hilo, anatafuta fedha kwa ajili ya matibabu ya macho, ambapo kwa mujibu wa madaktari kama atatibiwa angalau jicho moja, basi ataweza kuona.

Asimulia mkasa mzima

Anasema siku ya tukio, Juni 27 mwaka 2017, watu wasiojulikana zaidi ya 10 walivamia kijijini hapo na kufanya mauaji, ambapo walianza kumuua Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangwi, Hamis Mkina (CCM) na baadaye kufika kwenye nyumba yake kwa lengo hilo hilo na kuchoma nyumba yake moto.

Anakumbuka ilikuwa saa tano usiku, ambapo watu hao walifika nyumbani kwake, wakavunja mlango na kufanikiwa kuingia ndani, ambamo walikuwamo yeye, mkewe na watoto wawili.

“Walinichukua na kunifunga kamba mithili ya mtu anayekwenda kunyongwa. Walinifunga kitanzi huku wakinivuta na kuondoka name, nyuma niliwasikia wakimwambia mke wangu na watoto watoke nje.

“Baada ya muda nilisikia kitu kikilia kama bomu, kumbe walikuwa wanachoma nyumba yangu kwa kutumia mafuta ya petroli waliyoyachukua kwenye pikipiki yangu.

“Waliichoma nyumba moto huku wakiwaacha mke na watoto wangu nje,” anasimulia.

Anasema walipofika naye mbali kidogo na nyumba yake walimpiga risasi ya jicho, na kumpiga na kitu kingine kizito mithili ya rungu akapoteza fahamu.

Anasema alizinduka baada ya wiki tatu akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, akiwa hana uwezo wa kuona tena, wala kuhisi harufu ya kitu chochote kile.

Anasema aliendelea na matibabu kwa muda mrefu Muhimbili na hospitali ya Mnazi Mmoja.

“Nilisaidiwa nikapata dawa zilizonisaidia angalau kunusa, lakini macho hadi sasa hayawezi kuona. Nilishauriwa kwenda Hospitali ya Mkoa Mbeya, lakini nashindwa kutokana na kukosa fedha,” anasema.

Mkewe anena

Mke wa mwenyekiti huyo, anasema alishuhudia nyumba yake ikichomwa moto, akatoa taarifa kwa majirani ambao kesho yake asubuhi walianza kumtafuta mumewe na kumkuta mahali akiwa amevuja damu nyingi.

“Majirani na ndugu walimchukua mume wangu na kumpeleka Hospitali ya Kibiti kwa ajili ya matibabu ya awali, lakini baadaye hali ilizidi kuwa mbaya akahamishiwa Muhimbili.

“Huko alipata matibabu lakini hakufanikiwa kupona macho. Kila wakati amekuwa ni mtu wa kujisikia mnyonge na kulalamikia macho yake na hata wakati mwengine anaomba nimuazime jicho moja ili aweze kuona,” anasema Selina.

Anamuelezea mumewe kwamba alikuwa na msaada mkubwa katika familia kwani alikuwa hachagui kazi na kipato alichokuwa akipata kiliweza kusaidia mambo mbalimbali nyumbani.

Anasema baada ya hali kuzidi kuwa mbaya, waliamua kuhama Kibiti na kwenda kuishi Kinondoni ili wawe karibu na huduma za afya.

“Mume wangu alifanikiwa kupata vidonge vya kuondoa maumivu ya macho, na kuwa na uwezo wa kunusa, lakini bado hadi sasa hajaweza kuona kabisa.

“Bado hatujakata tamaa, tulikwenda Hospitali ya CCBRT kwa ajili ya uchunguzi zaidi, walitupa moyo kuwa jicho moja la kushoto linaweza kuona, wakatuelekeza kwenda hospitali iliyopo Kibaha Pwani, kwa ajili ya matibabu zaidi, tulipofika tulitajiwa gharama ya Sh milioni nne ambazo tulishindwa kuzimudu tukarudi,” anasema Selina.

Anasema pia kuna hospitali nyingine iliyopo mkoani Mbeya ambako kuna daktari amewaahidi kuwasaidia matibabu pindi watakapolipia kiasi cha fedha.

Anasema wao kipato chao ni kidogo hivyo anaiomba Serikali na jamii kwa ujumla wawasaidie ili mumewe aweze kuona na kurejea katika shughuli zake za kujitafutia kipato.

Pamoja na hayo, wanaishukuru Serikali iliyojitolea kuwasaidia huduma za matibabu waliyopata awali, bila kumsahau Naibu Waziri wa Nishati ambaye kila wakati amekuwa akimtafuta na kumsaidia.

“Hata leo yeye ndiye ametutafuta na kutuita hapa ofisini kwake ili aweze kujua ni namna gani anaweza kusimamia tukapata wafadhili watakaotusaidia kupata matibabu,” anasema Selina.

Gharama za maisha na matibabu

Hivi majuzi wanakijiji wa Mangwi walifanya mkutano uliomuhusisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ambaye aliwasikiliza kilio chao ambapo kikubwa kilikuwa ni kumsaidiaBuchayandi aweze kupona na kuboreshewa mazingira kijijini kwao.

Risala hiyo iliyosomwa na Maganga Simoni, iliweka bayana tatizo la fedha za kukamilisha ujenzi wa nyumba ya kijana huyo kiasi cha Sh 5,725,000 na fedha za matibabu.

Simona anataja changamoto nyingine kuwa ni mazingira magumu ya maisha kwa wajane na watoto wa marehemu mwenyekiti wa kijiji hicho, kukosekana kwa vifaa na nyumba ya mganga wa Zahanati ya Mangwi na nishati ya umeme.

Naibu Waziri Mgalu

Mgalu anasemaBuchayandi anahitaji kusaidiwa hivyo ni vema watu wakajitokeza kumchangia gharama za matibabu na kumalizia ujenzi wa nyumba yake.

Anasema amekuwa akimpigia simu mara kwa mara kujua anavyoendelea na hata kumsaidia kidogo, lakini bila kuwashirikisha wengine hatoweza.

Mkakati wa Kibiti

Anasema matukio mengi ya uhalifu yanafanyika gizani hivyo, ni jukumu lake sasa kuhakikisha vijiji hivyo vinawekwa umeme kupitia mpango madhubuti wa kuweka umeme vijijini REA.

Anasema tayari baadhi ya vijiji vilivyopo Kibiti, Rufiji na Mkuranga ameshaviombea na kuingizwa katika mpango huo.

“Wakipeleka umeme itasaidia kuondoa haya matukio ya kutisha,” anasema.

Anabainisha kuwa hadi sasa takribani vijiji 6000 tayari vina umeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles