KILIMO CHA MPUNGA KILOMBERO KUWAKOMBOA WATANZANIA

0
4954
Mtafiti Julius Kwesiga akiwafundisha wakulima kilimo bora cha mpunga{wa kwanza kutoka kushoto }

 

 

Na Lilian Justice, Kilombero

MPUNGA ni zao la pili la chakula  nchini kwa umuhimu linalolimwa sehemu nyingi duniani  ambapo Tanzania umuhimu wa zao hilo umeongezeka kuanzia muongo uliopita kutokana na jamii za mjini na vijijini kupendelea zaidi kula wali na kupunguza ulaji wa vyakula vingine na hivyo kulifanya zao hili kuwa na  mvuto wake kwa kuwa  ni la chakula na biashara.

Zao hili linaloshamiri kwa haraka na kuongeza heshima kwa Mkoa wa Morogoro kama ghala la chakula, ni pamoja na mpunga ambao kwa siku za karibuni limeongeza umaarufu miongoni mwa mazao ya chakula na biashara yanayoingiza kipato kwa wakulima nchini na kutegemewa na wananchi wa Wilaya ya Kilombero katika kukuza uchumi.

Hata hivyo, kilimo cha mpunga kwa nchi zinazoendelea kinakabiliwa na changamoto nyingi zinazokwamisha maendeleo ya uzalishaji wake na kubwa ikiwa ni kutegemea mvua kama chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga kwa wakulima wadogo.

Viwango vya mahitaji ya maji katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za mpunga na maeneo ya uzalishaji kutoka wilaya moja hadi nyingine.

Ni kwa jinsi hii mpunga hupandwa katika mazingira mbalimbali kwa kutegemea mahitaji yake ya maji.

Wataalamu wameshabainisha aina tatu kuu za mazingira yanayolimwa mpunga kulingana na upatikanaji wa maji na hali ya mwinuko wa nchi. Mazingira haya ni kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea mvua kwa asilimia 72, kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko (20%) na kilimo cha mpunga cha umwagiliaji (8%).

Maeneo yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania ni Morogoro maeneo ya Bonde la Kilombero/Ifakara, Dakawa, Malolo, Mbeya, Kyela, Mbarali, Shinyanga, Kahama, Mwanza, Magu, Geita na Sengerema, Bonde la Ruvu mkoani Pwani na Bonde la  Mto Rufiji  na mengineyo.

Asilimia 90 ya wakazi wa Wilaya ya Kilombero ni wakulima ambapo shughuli kuu ya uchumi ni kilimo cha mpunga, kama zao kuu la chakula na biashara.

Kutokana na faida kubwa inayotokana na zao hili, ni lazima kuliwekea msukumo na kipaumbele katika kukabili changamoto kubwa zinazokwamisha uzalishaji kwa kiwango cha juu kwa kuzingatia ubora unaostahili kimataifa.

Bado wakulima wengi wa zao hilo wanalima kilimo kisicho na tija cha  kizamani (kienyeji), hali inayowafanya kushindwa kuzalisha kwa wingi na kwa ubora, badala yake huvuna chini ya gunia saba kwa ekari moja ambapo kama wangefuata kanuni bora za kilimo cha mpunga wangeweza kuvuna gunia zaidi ya arobaini kwa ekari moja.

Wakulima  wanaweza kuzalisha kwa wingi zao hilo kama watafuata kanuni bora za kilimo na kukifanya kilimo hicho kuleta tija kwa kulima eneo dogo na kuvuna mavuno mengi zaidi.

Kwa sasa ni tofauti kwani wakulima wengi wanalima eneo kubwa na kushindwa kufuata kanuni bora za kilimo na kusababisha mavuno kuwa madogo, hafifu na wakati mwingine kukosa mavuno ya kutosheleza mahitaji ya chakula katika ngazi ya familia. Hali hiyo inatokana na kushambuliwa na wadudu, ndege na wanyama waharibifu wa mazao. Aidha, fikra duni kuwa kulima eneo kubwa ni kupata mavuno mengi, bado zinatawala na wakulima wachache wanaolima eneo dogo kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ni mfano mzuri kwa kuwa huvuna mavuno mengi na bora.

Akizungumzia kuhusu zao hilo, Mtafiti wa zao la mpunga   ambaye pia ni  mwanafunzi anayesomea  udakatari wa kilimo katika  Chuo Kikuu cha Bonn, Ujerumani Julius Kwesiga chini ya mradi wa Global E, unaotekelezwa katika maeneo chepechepe ya nchi za Afrika Mashariki, anabainisha kuwa bado wakulima wa zao la mpunga wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazokwamisha uzalishaji wenye tija wa zao hilo.

Kwesiga anasema kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa nchini Tanzania, utafiti wake aliofanya Tanzania katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, eneo la  Katindiuka na Kiyongwile amegundua aina tisa za kilimo cha mpunga.

Aidha, anasema kuwa  mkulima anaweza kuzalisha gunia 40 kwa ekari moja na kumfanya anufaike kupitia kilimo cha mpunga kuliko wanavyolima kwa sasa, kilimo kisichokuwa na tija na  kukifanya kilimo hicho kuwa ni cha biashara na kitakachomkomboa mkulima katika wimbi la umasikini.

Mtafiti Kwesiga anasema lengo la kufanya utafiti huo ni kupunguza utofauti wa mazao kutoka kwa mkulima anayevuna  gunia tano kwa ekari moja na  yule anayevuna gunia arobaini kwa ekari moja.

“Ili mkulima aweze kuvuna gunia 40 kwa ekari moja ni lazima alime na kuweka kingo za matuta katika shamba na hii inasaidia shamba kutunza unyevu na katika upandaji  apande sentimita ishirini kwa ishirini pamoja na kuweka   mbolea aina tatu tofauti za  Urea (Nitrogen) kilo 100, DAP (Phosporus)kilo 50 na MOP (Potasium) kilo 40 huku maji yakihitajika kwa wingi,” anafafanua Kwesiga.

Anaamini kuwa kilimo hicho  kinafaa kwa watu wenye pesa lakini pia aina ya pili ya  utafiti wa kilimo hicho ni kutoweka kingo za matuta kwenye shamba. Katika aina hii ya kilimo, mkulima anaweza kuvuna  chini ya gunia saba  kwa ekari moja na sababu  iliyopelekea  kutoa mavuno kidogo ni kutokana na kutowekwa kwa mbolea na  kutokuwa na unyevu wa kutosha kutokana na kutokuwa na kingo za matuta na katika kilimo hiki palizi hufanyika mara moja tu.

Aina ya tatu ya utafiti wake inabainisha kilimo cha kuweka kingo za matuta kwenye shamba, kuchabanga, kupiga udongo kulala kwa usawa ‘kupigalevel’ na kupanda na kufanya palizi  mara mbili na mavuno yake huanzia gunia kumi na mbili hadi kumi  na sita.

Kwa utafiti mwingine Kwesiga anasema mkulima anaweza kupata gunia 28 kama ataweka kingo za matuta, kuchabanga na kupanda, kuweka mbolea aina moja ya Urea (Nitrogen) mfuko mmoja wenye kilo 50.

Aina ya tano ya kilimo cha mpunga ni kwa  kutumia majani ya fiwi  ambapo katika kilimo hiki mkulima anapaswa kupanda fiwi kwenye shamba la mpunga na upandaji wake ni sentimeta 40 kwa 60 na  baada ya siku 45 shamba linakatuliwa pamoja na fiwi na baadaye mvua itakapoanza kunyesha mpunga unapandwa  kwa kumwaga  na mavuno yake ni gunia ishirini kwa ekari moja.

Aina ya sita  ya utafiti ni kutumia mbolea aina ya samadi ambapo katika utafiti huu mkulima anashauriwa kuweka samadi gunia 40 kabla ya kulima shamba na baadaye atakapokatua udongo utachanganyika na mbolea hiyo ambayo ina uwezo mzuri wa kurutubisha udongo na kustawisha mazao kwa muda mrefu  na mavuno yake hufikia gunia 20 kwa ekari moja.

Matokeo zaidi ya utafiti huo yanatokana na matumizi ya samadi na kuongeza upandaji wa mimea jamii ya mikunde. “Katika aina hii mkulima anapaswa kuvuna mpunga si kwa kufyeka bali kwa kukata mpunga ili majani ya mpunga yabaki shambani na baada ya kuvuna anatakiwa kupanda kunde kuanzia Juni hadi Januari,” anasema.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here