27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kilimanjaro Queens tishio Cecafa

NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’, imeibuka na ushindi wa mabao 9-0 dhidi ya Sudan Kusini, katika mchezo wa kundi  A wa michuano ya Chalenji ya nchi za Afrika Mashariki na Kati(Cecafa), uliochezwa jana Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo mnono ni mwanzo mzuri kwa kikosi cha Kilimanjaro Stars ambacho ni bingwa mtetezi wa michuano hiyo. 

Mabao ya Kilimanjaro Queens yalifungwa na Mwanahamisi Omari, ambaye alipachika matatu(hat-trick), dakika za 17, 41 na 46 na mengine yakitupiwa wavuni na Donisia Minjia dakika ya 32, Stumai Abdalah dakika za 47 na 50 na Julitha Tamuwaji dakika za 52 na 71.

Mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja ulishuhudiwa Kilimanjaro Queens ikienda mapumziko ikiwa mbele  kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili, kilikuwa kizuri zaidi kwa upande wa Kilimanjaro Queens  kwani iliweza kuvuna mabao mengine saba. 

Kilimanjaro Queens ilitwaa ubingwa huo katika michuano hiyo iliyopita iliyofanyika nchini Uganda,  baada ya kuifunga Kenya.

Kama itafanikiwa kutwaa ubingwa katika michuano hii, itakuwa mara ya tatu mfululizo, baada ya kutwaa taji hilo kwa kuilaza pia Kenya zilipokutana fainali, ambapo Rwanda ilikuwa mwenyeji.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Kilimanjaro Queens, Bakar Shime alisema ameridhishwa na kiwango kilichoonesha na wachezaji wake na kusababisha ushindi huo mnono.

“Wachezaji wangu wamecheza vizuri, washambuliaji walikuwa na utulivu wa kutosha, sina shaka kama tutafanya vizuri pia katika mchezo ujao,”alisema.

Wakati huo huo, Timu ya Taifa ya Wanawake ya Zanzibar  ilizindua vibaya kampeni zake za michuano hiyo
baada ya kufungwa mabao 5-0 na Burundi, mchezo uliochezwa kuanzia saa nane mchana Uwanja wa Azam Complex.

Burundi ilianza kupachika bao dakika ya 24 kupitia kwa Sakina Saidi ambaye pia alifunga la pili dakika ya 35.

Sandrine Niyonkuru aliifungia Burundi bao la tatu dakika ya 55, huku lile la nne likipachikwa na Aziza Haji ambaye alijifunga wakati anaokoa hatari.

Aniela alihitimisha kalamu ya mabao ya Burundi kwa kuifungia bao la tano dakika ya 88.

Leo itakuwa zamu ya Kundi B, ambapo Kenya itapepetana na Ethiopia, mchezo  utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa nane mchana kabla ya Uganda kupimana ubavu na Djobout baadaye saa kumi jioni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles