ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
MICHUANO ya Chalenji ya nchi za Afrika Mashariki (Cecafa) kwa timu za taifa za wanawake, ilianza kutimua vumbi Jumamosi iliyopita Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam, ikishirikisha timu nane za ukanda huo.
Katika michuano hiyo, Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Queens’ ipo Kundi A pamoja na ndugu zao Zanzibar, Burundi na Sudan Kusini.
Kundi B zimo Ethiopia, Kenya, Uganda na Djibouti.
Tayari Kilimanjaro Queens imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kushinda michezo yake miwili, ikianza kuirarua Sudan Kusini mabao 9-0, kabla ya kuifumua Burundi mabao 4-0.
Timu hiyo imebakiza mchezo mmoja wa hatua ya makundi dhidi ya Zanzibar.
Kutinga nusu fainali ya michuano hiyo, kunaifanya Kilimanjaro Queens kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.
Katika kuonyesha kwamba haikubahatisha kutwaa taji hilo mwaka jana nchini Rwanda, Kilimanjaro inayonolewa na kocha Bakari Shime maarufu ‘Mchawi mweusi, si kwamba inashinda tu, bali inaonyesha kandanda safi.
Mechi ya Tanzania dhidi ya Sudan ilivunja rekodi ya mabao iliyokuwa imewekwa mapema mchana na Burundi iliyoichakaza Zanzibar kwa kuichapa mabao 5-0, mchezo uliochezwa kuanzia saa nane mchana.
Mbali na rekodi ya mabao iliyowekwa na kikosi cha Kilimanjaro Queens ambayo ni bingwa mtetezi, pia wachezaji wake waliotea mara 23 huku Sudan Kusini ikifanya hivyo mara mbili pekee.
Katika mchezo huo, Mwanahamis Omary alipoteza nafasi tatu za wazi kipindi cha kwanza kutokana na kile kilichoonekana kuwa na presha ya mchezo.
Kwa ujumla Kilimanjaro iliizidi kwa kila kitu Sudan Kusini kwani katika mchezo huo ilitengeneza nafasi za kufunga zaidi ya 15 wakati wapinzani wao wakifanya hivyo mara tatu.
Kilimanjaro pia ilivuna kona tisa,wakati Sudan Kusini hawakufanikiwa kutengeneza hata moja.
MTANZANIA limezungumza na wachambuzi mbalimbali wa soka nchini juu ya matokeo ya Kilimanjaro Queens na mtazamo wao katika kupigania kutetea taji la Cecafa ili kuandika rekodi ya kutwa kwa mara ya tatu mfululizo.
“Ukiangalia katika ukanda wa Cecafa, Tanzania tuna ligi bora ya wanawake, pongezi ziende kwa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWF) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kuhakikisha mpira wa wanawake unachukua nafasi nchini.
“Ubora wa ligi ya wanawake unatosha kuiwezesha Tanzania Bara kulibakisha kombe nyumbani, jambo zuri ni kwamba wachezaji wa Kilimanjaro Queens wanafahamu Watanzania tumeshajiandaa kushangilia ubingwa, nina uhakika wanapambana kutimiza ndoto zetu,”anasema Ally Mayay mchambuzi na mwanasoka nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars.
Kwa upande wake mchambuzi wa soka nchini, Alex Kashasha anasema:
“Wachezaji wetu wana uwezo wa kuifunga timu yoyote watakayokutana nayo, upinzani pekee ninaoutarajia kuuina watakapokutana na Kenya ambao nao hatujapishana sana ubora wa ligi.
“Lakini hilo sio tatizo kama watajipanga vizuri, ukizingatia wanakocha mwenye mbinu nyingi na za haraka, baada ya kuwaona wapinzani wao, sina hofu na wanangu kama waliweza kuchukua ubingwa ugenini hakuna kitakachowashinda nyumbani mbele ya baba na mama zao wanaoaacha shughuli na kwenda uwanjani kuwapa sapoti.”
Shime afunguka
“ Kwanza
namshukuru Mungu kwa kuanza mechi ya kwanza na ushindi mkubwa, niwapongeze
wachezaji kwa kufanya kile tulichokubaliana kifanyike, siri ya mabao mengi tuliyoyapata
ni nidhamu na kujiamini katika kile wachezaji wanachokifanya.
“Vijana wanajituma na wanatambua kwamba ni mabingwa watetezi jambo
linalowapa morali ya kupambana, suala la kukosa nafasi lililojitokeza ni presha
tu ya mchezo hasa kutokana na kuwa mara yao ya kwanza kucheza mbele ya umati
mkubwa uliojitokeza lakini katika mechi yetu ya pili hili suala halitojitokeza
tena.”
Cecafa kwa Wanawake
Michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza inafanyika katika ardhi ya Tanzania , imeandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Cecafa ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa
ikiandaa michuano ya wanaume maarufu ‘Cecafa Senior Challenge Cup’ iliamua
kubuni michuano kwa upande wa wanawake kwa lengo la kuinua soka la wanawake
kwenye ukanda huo.
Mashindano ya wanawake yalianzishwa mwaka
1986, ambapo Zanzibar ilikuwa mwenyeji na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo.
Ilichukua miaka 30 michuano hiyo kufanyika tena, ambapo mwaka 2016, Uganda ilikuwa mwenyeji na Kilimanjaro Queens iliibuka mabingwa.
Mwaka 2018 ilifanyika nchini Rwanda Kilimanjaro ikaiibuka mabingwa kwa mara ya pili.