27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kilichowang’oa vigogo NSSF

Mradi Kijichi
Mradi Kijichi

Na ARODIA PETER, DAR ES SALAAM

UBADHIRIFU wa fedha na ukiukwaji wa taratibu na sheria katika usimamizi wa miradi kadhaa ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), vimeelezwa kuwa miongoni mwa sababu za kusimamishwa kazi wakurugenzi sita na mameneja watano wa shirika hilo.

Vigogo hao walisimamishwa kazi juzi na Bodi ya Wadhamni ya NSSF inayoongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Samwel Wangwe, kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, ununuzi wa ardhi na ajira katika shirika hilo.

Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacoub Kidula, Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Chiku Matessa na  Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhra na Majanga, Said Shemliwa.

Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani, Pauline Mtunda na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Cresentius Magori.

Mameneja waliosimamishwa ni Meneja Utawala, Amina Abdallah, Meneja wa Uwekezaji, Abdallah Mseli na Meneja wa Miradi, John Msemo.

Wengine ni Mhasibu Mkuu, John Davis Kalanje, Meneja Kiongozi Mkoa wa Temeke, Wakili Chedrick Komba na Meneja Miradi, John Ndazi.

Inaelezwa kuwa baadhi ya ubadhirifu huo ulifanywa kupitia miradi ya usimamizi wa nyumba za kuuza zilizopo Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, unaokadiriwa kufikia Sh bilioni 137.7.

Katika ripoti ya mwaka ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2014/2015, imebainika kuwa ulikuwapo ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika miradi hiyo.

Taarifa hiyo ya CAG inaeleza katika ukurasa wa 165 na 166 kuwa Juni 30 mwaka 2015, Sh bilioni 79 za shirika hilo  zilitumika katika ujenzi wa nyumba hizo ambazo ziliamuriwa kuuzwa ndani.

Uamuzi huo ulitolewa badala ya kufuata maelekezo ya wasimamizi kwa kutumia benki au makampuni ya mikopo kama ilivyoelekezwa katika kanuni namba 13 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na mwongozo wa uwekezaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Katika maoni yake kuhusu mradi huo, ofisi ya CAG iliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa na wasimamizi wake.

“Kitendo chochote cha kutofuata maagizo kinatakiwa kuwasilishwa kwa maandishi kwa mdhibiti wa sekta na kukubaliana muda uliopangwa kwa ajili ya kufuatwa,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.

Ukiukwaji mwingine wa sheria na taratibu unaotajwa kufanywa na vigogo hao, ni ununuzi wa ardhi bila ushindani kutoka kwa muuzaji mmoja, kwa gharama ya Sh bilioni 15.16.

Taarifa hiyo ya CAG inaeleza kuwa NSSF ilipanga bajeti ya Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa kiwanja kupitia zabuni za ushindani.

“Hata hivyo, ilitumia chanzo kimoja katika ununuzi wa kiwanja kilichogharimu Sh bilioni 15.16. Nimegundua kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma haikujulishwa, kinyume cha kanuni namba 87 ya mwaka 2013 ya mamlaka hiyo inayohitaji kuwasilishwa taarifa za mkataba wa tuzo kwake, ndani ya siku saba kuhusu mchakato wa ununuzi endapo chanzo kimoja kilitumika,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.

CAG aliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia mpango wake wa bajeti na kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013, kuhakikisha ununuzi unafanyika katika ushindani ili kupata huduma kwa bei nafuu.

Kutokana na hali hiyo, katika ripoti hiyo ya ukaguzi, CAG alieleza namna NSSF lilivyoingia ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estate kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Bulders Limited.

Katika mkataba huo, Azimio Housing Estate inatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni ambapo kwa hatua ya awamu itaaanza na ekari 300.

“Katika ubia huu, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii linamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estate inamiliki asilimia 55. Jumla ya gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 653.3.44.

“Ukaguzi wa hatimiliki umeonyesha kuwa Azimio Housing Estate inamiliki viwanja viwili, kiwanja chenye hatimiliki namba 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye hatimiliki namba 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11 ambavyo vyote vinapatikana katika eneo la Rasi Dege,” ilieleza taarifa ya CAG.

Pamoja na hali hiyo, CAG alisema kuwa hajaweza kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio iliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji hali ambayo NSSF ililipa asilimia 20 ya fedha kama mtaji ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kupotea.

Licha ya kuibuliwa kwa hili, CAG alieleza kuwa Menejimenti ya NSSF ina udhaifu katika mifumo ya kifedha na kiuhasibu. Kwamba wana mfumo mkuu wa usimamizi wa rasilimali ambao unaweza kuunganishwa na mfumo wa usimamizi wa fedha ambao unakosa moduli ya uhasibu kwa ajili ya kuhifadhi taarifa za kifedha.

 

DENI LA BIL 723.22

Katika taarifa hiyo ya CAG, inaelezwa kuwa NSSF iliikopesha Serikali katika miradi yake mbalimbali, lakini hata hivyo imekuwa hailipi madeni yake kwa muda mrefu.

Kwamba hali hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa limbikizo la riba na adhabu hadi kufikia asilimia 39 ya salio la Sh bilioni 729.22 kufikia Juni 2014.

 

WAFANYAKAZI NA MADENI

Shirika hilo lina utaratibu wa ndani wa kutoa mikopo kwa wafanyakazi wake, na ukaguzi umeonyesha kiasi cha Sh milioni 827.98 bado kinadaiwa kwa wafanyakazi ambao si waajiriwa tena wa NSSF.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na kumteua kuwa balozi ingawa hadi sasa hajapangiwa nchi ya kwenda.

Vilevile, mwanzoni mwa Machi mwaka huu, mrithi wa Dk. Dau, Dk. Carine Wangwe ambaye aliteuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, uteuzi wake ulitenguliwa na Ofisi ya Rais Ikulu katika kile kilichoelezwa kuwa ulikiuka taratibu.

 

KUHOJIWA TAKUKURU

Wakati huohuo, taarifa zilizoifikia MTANZANIA jana, zilisema vigogo hao wameanza kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu suala hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yuko nje ya ofisi na akashauri atafutwe msemaji wa taasisi hiyo, Mussa Misalaba.

Hata hivyo, Misalaba alipoulizwa, alisema hana taarifa na jambo hilo kwa sababu hakuwa ofisini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles