23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kili Stars ya kwanza robo fainali

thumb_IMG_2055_1024*Zanzibar yaangukia pua, mzimu wa Algeria wamwandama Mudathir

NA MWANDISHI WETU

TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imekuwa timu ya kwanza kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea kutimua vumbi nchini Ethiopia, baada ya jana kuichapa Rwanda ‘Amavubi’ mabao 2-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Awassa.

Wakati Kili Stars ikikenua kwa ushindi, wawakilishi wengine wa Tanzania, Zanzibar Heroes waliendelea kuwa wateja kwenye michuano hiyo baada ya kupokea kipigo kikali cha mabao 4-0 dhidi ya Uganda ‘The Cranes’.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Kili Stars baada ya mchezo wa awali kuirarua Somalia mabao 4-0 na sasa ndio vinara wa Kundi A wakiwa na pointi sita wakifuatiwa na Rwanda mwenye tatu.

Shukrani za pekee ziende kwa kiungo, Said Ndemla na winga Simon Msuva, walioifungia Kili Stars mabao hayo muhimu mbele ya Rwanda iliyokuwa ikiongozwa na nahodha wake, Haruna Niyonzima, anayekipiga tmu ya Yanga.

Timu zote mbili zilianza mchezo huo kwa kupelekeana mashambulizi makali na dakika ya 17, mshambuliaji Jacques Tuyisenge, almanusura aiandikie Rwanda bao kwa njia ya mkwaju wa adhabu ndogo, lakini shuti alilopiga lilitoka sentimita chache ya lango la Kili Stars.

Dakika saba baadaye Kili Stars ilijipatia bao safi lililofungwa na Ndemla kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo, uliomshinda kipa Olivier Kwizera.

Faulo hiyo ilitokana na madhambi aliyofanya kiungo wa Rwanda, Jean Mugiraneza ‘Migi’ kwa nahodha wa Kili Stars, John Bocco, nje kidogo ya eneo la 18.

Kili Stars ilijitahidi kulinda bao hilo hadi mpira huo ulipoenda mapumziko, lakini mambo yalibadilika kipindi cha pili kwa Rwanda kuja juu na kumiliki sehemu kubwa ya mchezo, hasa baada ya kiungo Himid Mao kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Mkude.

Wakati Rwanda ikijitahidi kupata bao la kusawazisha, ilijikuta ikipigwa bao la pili dakika ya 74 lililofungwa na Msuva, akitumia vema uzembe wa kipa Kwizera aliyeukosa mpira alioutokea, uliomkuta mfungaji na kufunga vema lango likiwa wazi.

Rwanda ilizidi kupeleka mashambulizi langoni mwa Kili Stars na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 85 lililofungwa na Jacques Tuyisenge.

Kama Kili Stars itaambulia sare au ushindi dhidi ya wenyeji Ethiopia kwenye mchezo wake wa mwisho wa Kundi A Jumamosi hii, itamaliza kinara wa kundi hilo na kwenye robo fainali itakutana na timu mshindwa bora namba tatu.

Mabao ya Uganda dhidi ya Zanzibar yalifungwa na kiungo Farouk Miya, aliyefunga mawili huku Erisa Ssekisambu akipiga la tatu na Denis Okot akipiga la nne.

Lakini Zanzibar imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na kadi nyekundu mbili walizozipata kwenye mchezo huo, wakipewa kipa Mwadini Ally na kiungo Mudathir Yahya.

Zanzibar ni kama imetanguliza mguu mmoja nje kutoka kwenye michuano hiyo, kufuatia kipigo hicho cha pili mfululizo kufuatia cha awali cha bao 1-0 dhidi ya Burundi na sasa inasubiria kukamilisha ratiba kwa kucheza na Kenya keshokutwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles