Kili Stars kuiliza Uganda

0
1032

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

TIMU ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, inatarajia kushuka dimbani leo kuvaana na Uganda katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Chalenji, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda, akitamba kuwaliza wapinzani wao hao.

Mchezo huo wa michuano hiyo ya nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), utapigwa kwenye Uwanja wa KCCA, jijini Kampala.

Kabla ya Kili Stars kucheza na Uganda, Kenya watakipiga na Eritrea katika mchezo mwingine wa hatua hiyo kusaka timu zitakazotinga fainali.

Kili Stars ilitinga nusu fainali baada ya kutoka suluhu na Sudan katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi, huku Uganda ikiingia hatua hiyo kwa kuifunga Eritrea mabao 4-1.

Kwa upande wao, Kenya waliingia hatua hiyo kwa kuichapa Zanzibar bao 1-0, wakati Eritrea walitoka suluhu na Djibouti.

Mechi kati ya Kilimanjaro Stars na Uganda, inatarajiwa kuwa na upinzani wa aina yake kutokana na rekodi ya timu hizo zinapokutana kwa siku za hivi karibuni.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana, ilikuwa ni katika mchezo wa kuwania tiketi ya Afcon ambapo Tanzania iliichapa Uganda mabao 3-0 na kufuzu michuano hiyo iliyopigwa nchini Misri mwaka huu.

Kwa maana hiyo, Uganda leo watashuka dimbani wakiwa na azma mbili, kwanza kupata ushindi ili kutinga fainali ya Chalenji, lakini pia kulipiza kisasi, huku Tanzania wakitaka kuendelea ubabe wao.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alisema vijana wake wapo tayari kwa vita wakiamini lazima watashinda na kutinga fainali.

“Tunashukuru tumeweza kuingia hatua hii na sasa tunaenda kupambana kwa kuingia na mfumo mwingine utakaotupa matokeo,” alisema.

Alisema kuwa wachezaji wake wanaendelea vizuri na wamemuahidi kupambana kufa au kupona ili kupata ushindi ili kutinga fainali na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here