RAMADHAN HASSAN-DODOMA
SERIKALI imesema kila mwananchi anatakiwa kumiliki laini moja kwa mtandao mmoja wa simu, ili kuondoa utitiri wa laini zisizokuwa na tija.
Kampuni za simu zimeagizwa kusajili kwa kutumia alama za vidole na zoezi hilo litaanza Mei Mosi, mwaka huu.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema).
Katika swali lake, mbunge huyo alisema waziri huyo alinukuliwa kwenye vyombo vya habari Mei mosi, mwaka huu kutakuwa na usajili mpya wa laini za simu wa kutumia alama za vidole na kwamba hakutakuwa na ruhusa ya kumiliki laini mbili hadi ruhusa maalumu ya maandishi.
“Kuna maeneo mengine laini hazipatikani kuna mengine Vodacom ipo, Airtel haipo sasa hamwoni kama mtawasumbua wananchi?,” alihoji.
Akijibu swali hilo, Nditiye alisema kilichozungumzwa ni kwamba anatamani kila Mtanzania awe na laini moja ya simu kwa mtandao mmoja na akihitaji laini nyingine aseme.
“Tunaepuka utitiri wa laini nyingi nyie ni mashahidi mnaombwa hela kila siku tuma kwa namba hii mara hii hayo ni malalamiko yasiyo na tija kwa Watanzania,”alisema.
Alisema kilichozungumzwa ni kuwa na laini moja kwa mtandao mmoja.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti maalumu, Anna Gidarya (Chadema), alihoji serikali itapeleka lini huduma ya mawasiliano kwenye baadhi ya vijiji vya Jimbo la Babati ambavyo kwa muda mrefu havina huduma hiyo.
Akijibu swali hilo, Nditiye alisema serikali inaendelea kuratibu utekelezaji wa jitihada muhimu za kuwezesha maeneo yote nchini kufikiwa na huduma za mawasiliano sawasawa na maelekezo ya sera ya Taifa ya Tehama ya mwaka 2016.
“Kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote serikali itaviainisha vijiji vya Yorotonik, Endagwe, Hoshan na Endakiso kwa kuangalia ukubwa wa eneo, idadi ya wakazi wake pamoja na kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya rusuku kwa ajili ya kufikisha huduma hiyo,” alisema
Alisema baada ya tathmini kukamilika vijiji hivyo vitajumuishwa katika orodha ya miradi itakayoingia katika zabuni zinazotarajiwa kutangazwa katika mwaka wa fedha 2019/20.