26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

Kila mmoja kuishangilia Yanga leo

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KUTOKANA na taratibu za mchezo wa kiungwana ‘Fair Play’, leo kila mmoja atasimama kuwapigia makofi Mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Yanga SC watakapokabidhiwa mwali kwenye mchezo wao dhidi ya Azam utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini hapa kuanzia saa 11 jioni.

Yanga ilitangaza ubingwa mapema Jumatatu ya wiki iliyopita, walipoichapa Polisi Morogoro mabao 4-1 na kufikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Wakati Yanga ikitaka kushereherekea vema ubingwa huo leo kwa kupata ushindi, Azam wataingia dimbani kusaka pointi tatu muhimu ili kujihakikishia kushika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 48.

Matajiri hao wa Azam Complex wenye pointi 45 wapo kwenye vita kali na wapinzani wao Simba waliojikusanyia pointi 44, ambao nao wanawania nafasi ya pili ili kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Azam inahitaji pointi tatu tu katika mechi mbili ilizobakiza ya leo na ile ya Mgambo JKT, watakayocheza nayo Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na mabingwa hao wa msimu uliopita, waliotwaa taji bila kufungwa mchezo wowote.

Yanga itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa jumla ya mabao 2-1, huku Azam ikifungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa ligi uliofanyika Jumapili iliyopita.

Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, anatarajia kukosekana kwa upande wa Azam kutokana na kadi nyekundu ya kizembe aliyoipata kwa kumchezea vibaya beki wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Kocha Mkuu wa muda wa Azam, George Nsimbe ‘Best’ alilipasha MTANZANIA jana kuwa mechi dhidi ya Yanga ni ya kawaida sana kwao na wamejipanga kuibuka na ushindi.

“Bado tupo kwenye vita ya kuwania nafasi ya pili ili tuimalize lazima tushinde mechi ya kesho (leo), nimekiandaa kikosi changu kupambana na kupata matokeo tunayoyahitaji ili kutimiza malengo yetu,” alisema.

Mechi hiyo inatarajia kuchezeshwa na mwamuzi wa kati, Jacob Adongo kutoka Mara, akisaidiwa na washika vibendera, Fednand Chacha (Mwanza), Hellen Mduma (DSM), huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Hussein Kalindo (DSM) na Kamisaa wa mchezo huo ni Damian Mabena kutoka Tanga.

Katika kile kinachoelezwa ni kuipa nguvu Yanga kushinda mchezo huo, baadhi ya mashabiki wa Simba wanadaiwa wamepanga kuwashangilia watani zao wa jadi ili waifunge Azam.

Simba ina ukame mkubwa wa kushiriki michuano ya kimataifa, mara ya mwisho ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka juzi na kutolewa kwa jumla ya mabao 5-0 na Libolo ya Angola, ambapo ushindi wowote wa Azam leo utazidi kuwaongezea ukame huo.
Yanga na kombe lao

Kama ilivyopewa Azam kombe jipya msimu uliopita, Kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom Tanzania ambao ndio wadhamini wakuu wa ligi hiyo, leo itawafanyia jambo kama hilo Yanga.

Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, aliliambia gazeti hili jana kuwa pamoja na kuipa Yanga kombe jipya, pia wamepanga kuivalisha medali Azam kama itashinda mchezo huo na kutwaa nafasi ya pili.

“Tumefurahishwa sana na msimu huu wa ligi, umekuwa ni msimu wa mafanikio kutokana na ushindani wa timu zote na imedhihirisha ni kwa namna gani Vodacom tumepania kuifanya ligi hii kuwa ya kimataifa zaidi, kwani tumekuwa tukitoa zawadi za kila mwezi kwa wachezaji wanaofanya vizuri lengo ni kuwapa morali ya kufanya vizuri,” alisema.

Kampuni ya Vodacom pia itatumia mchezo huo kumkabidhi zawadi mchezaji bora wa mwezi Aprili, Mrisho Ngassa, pamoja na fedha taslimu Sh milioni moja.

Mgeni rasmi atakayeikabidhi Yanga kombe hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fennela Mukangara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles