Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo ameitaka jamii kuendelea kuwalinda watoto bila kuwabagua na kuhakikisha wanapatiwa haki zote wanazostahili.
Tumike alikuwa akizungumza kwa niaba ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Bonyokwa.
“Mtoto halelewi na mtu mmoja, mwalimu au mzazi peke yake, analelewa na watu wote. Mtu anaweza kuona mtoto ananyanyaswa anakaa kimya…mtoto wa mwenzio ni wa kwako kila mmoja awe balozi wa kumtetea mtoto,” amesema Tumike.
Amesema pia katika jitihada za kuendelea kulinda haki za watoto wana mpango wa kujenga uzio katika Shule ya Sekondari Bonyokwa ili watoto wasome vizuri kusiwe na ushawishi.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bonyokwa, Shabani Maliyatabu, amewataka wazazi na walezi kuyatumia maadhimisho hayo kwa kujitathmini kama wamekuwa chanzo cha kutengeneza watoto bora au kuwaharibu.
“Migogoro ndani ya familia inaharibu watoto wetu, siku ya leo tukafanye tathmini kama ni mzazi, mlezi nyumbani kwako unakuwa chanzo cha kutengeneza mtoto wa kesho aliye bora na mwema ama unatengeneza atakayekuwa tatizo…ukipata majawabu nenda kafanye marekebisho.
“Ukimpenda mtoto ukimfanyia yaliyo mema naye atakwenda kuifanyia mema jamii,” amesema Maliyatabu.
Katika risala ya watoto iliyosomwa na Veronica Thomas, wameomba watoto walindwe dhidi ya ukatili wa kimwili, kiuchumi na kihisia.
Amesema bado kuna changamoto ya vitendo vya ukatili kwa watoto kama vile ukeketaji, kingono, utumikishwaji katika kazi nyingi majumbani, kutelekezwa na kukosa mahitaji yao ya msingi kutokana na migogoro ya wazazi.
“Tuna wajibu wa kutetea haki zetu kwa kuwa wajasiri wa kuzidai, tuzidai kupitia utaratibu uliowekwa na serikali bila kuwakosea wakubwa,” amesema Veronica.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Bonyokwa, Regina Ng’ongolo, amesema watoto wana haki ya kusikilizwa na kuwataka wazazi kuhakikisha watoto wanapata haki zote wanazostahili ili waweze kukua na kufikia malengo yao.
“Sisi kata ya Bonyokwa tunalinda haki za mtoto tuna dawati la mtoto ambalo liko chini ya afisa ustawi wa jamii, kesi zote kuhusu ukatili wa kijinsia kwa watoto zinaletwa pale zinapatiwa suluhisho na wahusika wanafikishwa katika vyombo vya kisheria,” amesema Regina.
Siku ya Mtoto wa Afrika ilianza kuadhimishwa mwaka 1991 ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto waliouawa kikatili Juni 16, 1976 huko Soweto Afrika Kusini.