26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete: Watumishi wa Umma jiepusheni na mikopo kausha damu

Na Lusungu Helela, Simiyu

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Ridhiwani Kikwete (Mb) amewatahadharisha Watumishi wa Umma kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kwa jina la “Kausha Damu” huku akisisitiza kuwa mikopo ya aina hiyo imekuwa ikidhalilisha na kutweza utu wa watumishi katika jamii.

Sehemu ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza na wilayani humo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Kikwete ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Busega mkoani Simiyu katika kuhitimisha ziara yake aliyoianza mapema wiki hii mkoani Mara.

Amesema mikopo hiyo imewafanya baadhi ya watumishi wa umma kuathirika kisaikolojia na kushindwa kufika katika vituo vya kazi na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi. 

Amefafanua kuwa mikopo hiyo ambayo huchukuliwa kwenye Taasisi za Kifedha  zisizotambulika imekuwa na riba kubwa ambayo huwapelekea watumishi wengi kushindwa kuwasilisha marejesho na hivyo kupelekea kuuzwa kwa nyumba au vitu vya thamani  wanavyo vimiliki.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Kikwete amewataka Watumishi kuanza kutumia Mfumo mpya wa kieletroniki wa kukopa (e-loans) ulioanza kutumika kuanzia Septemba 1, 2023 ambao unamuwezesha Mtumishi wa Umma kuomba mkopo pasipo kufika kwenye Taasisi ya Kifedha au Tawi la Benki.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akiwa  na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega mara baada ya kukagua zahanati iliyotekelezewa na mradi wa TASAF.

Amesema mfumo huo umeanzishwa na Ofisi ya Rais – UTUMISHI na Utawala Bora ili kumsaidia Mtumishi wa Umma kupata mikopo katika Taasisi za Kifedha zinazotambulika na Mwajiri ili kumuepusha Mtumishi  kukopa sehemu ambazo humpeleka Mtumishi   kunyang’anywa kadi ya Benki.

Aidha, Kikwete amewataka watumishi hao kujenga nidhamu ya matumizi ya pesa wanazopata kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya baadaye baada ya kustaafu.

Amewasihi kujiwekea malengo ya kujiandaa kustaafu kuanzia leo ili wasije kuwa wateja wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Kuendeleza Jamii (TASAF).

“Hakikisheni hata hela mnazozikopa mnafanya uwekezaji wa kimkakati kwa ajili ya kujitegemea kiuchumi katika siku za mbeleni,” amesisitiza Kikwete.

Katika ziara hiyo Kikwete mbali ya kuzungumza na watumishi wa umma katika mikoa ya Mara na Simiyu pia  amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF pamoja na kuzungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles