27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete, Sirro wafunguka kifo cha Mengi


AZIZA MASOUD – Dar es Salaam

RAIS mstaafu Jakaya Kikwete ameitaka jamii kuwa na utulivu na kuacha kuzusha uongo kuhusu kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, badala yake wasubiri  taarifa sahihi kutoka kwa ndugu na mtoto wa marehemu walioko Dubai.

Kauli ya Kikwete imekuja baada ya kuwapo kwa taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Mengi, huku wengine wakiwataja watu wake wa karibu kwamba wanafahamu undani wa kifo hicho wanachodai si cha kawaida.

Akizungumza nyumbani kwa Mengi, Kinondoni, Dar es Salaam jana alipokwenda kuhani msiba, Kikwete alisema kama watu wanampenda Mengi, wanapaswa kuacha kuandika vitu vinavyotungwa mitandaoni na katika baadhi ya vyombo vya habari ambavyo si sahihi.

“Familia inapaswa kumuenzi Mengi kwa kufanya mambo aliyokuwa akijivunia na sisi wengine tuendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki, tuache uongo, tuache kuingiza yasiyokuwepo tukaichanganya  jamii.

“Kama kweli tunampenda Mengi, haya ya uongo na kutungatunga tuachane nayo, tusubirie ukweli tutaupata, amefariki Dubai wakati mdogo wake akiwepo, mtoto wake akiwepo, kwahiyo hao ndio wana ukweli wenyewe, hao wengine mnaowasoma wote  tuwaache wanaweza kutuchanganya,” alisema Kikwete.

ALIVYOPOKEA KIFO

Akizungumzia jinsi alivyopokea kifo hicho, alisema alipata taarifa akiwa nchini Benin alikoenda kushiriki mkutano wa masuala ya malaria.

“Si rahisi kupata maneno mazuri ya kusema na kupata nguvu ya kuongea katika kipindi hiki cha simanzi, nilipata habari hii nikiwa Benin, nilipofika nikapata taarifa hiyo, kwa kweli ilinishtua sana, kitu ambacho sikutegemea, lakini ni kweli kifo siku zote hakina taarifa.

“Basi nilieleze tu hisia zangu kwa kupoteza rafiki, kupoteza kaka, kupoteza ndugu na kama taifa pia limepoteza mmoja wa raia wake na watu wake makini na mahiri.

“Taifa pia limepoteza mchapakazi kwa sababu ukiangalia historia kule alipoanzia hadi alipofikia sasa tunaona ni kiasi gani mtu akitumia juhudi na maarifa anaweza kufikia mafanikio ya kiasi gani,” alisema Kikwete.

Pia alisema kabla Mengi hajasafiri aliongea naye kupitia simu ya mkononi na walikubaliana kukutana baada ya wote kurudi safari.

Alisema walikuwa na utaratibu wa kukutana na Mengi mara kwa mara kama kaka na mdogo wake kwa mazungumzo mbalimbali.

“Mengi alikuwa mzalendo, mtu aliyeipenda sana nchi yake, alipenda maendeleo ya taifa letu. Pia alikuwa na huruma na moyo wa upendo. Alikuwa pale ambapo ana uwezo wa kusaidia hapendi kumuacha mwenzake awe anateseka na kwa bahati nzuri Mungu alimjalia utajiri mkubwa ambao ameutumia pia katika kusaidia na wengine waliokuwa na uhitaji,” alisema Kikwete.

Alisema kwa kuwa watu wa aina ya Mengi ni wachache duniani, hivyo kuondoka ni jambo la kusikitisha na kutia huzuni kwa kuwa walitamani waendelee kuwa naye, lakini Mungu amepitisha hukumu yake.

“Kwa sisi tunaoamini Mungu tunaamini kwamba kabla hujatoka kuja duniani  Mungu unaweka naye mkataba, kwamba  huko unapokwenda utakaa siku ngapi na siku ile ikifika unakuwa hauna la kufanya,  kwa sababu yoyote na kwa mazingira yoyote utaondoka duniani,” alisema Kikwete.

Alisema kwa sasa ni jukumu la jamii kuwatia moyo watoto wake na familia ili waweze kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu.

Kikwete alisema Mengi kaishi maisha yake na amefanya mengi yale aliyoyafanya yapaswa yadumishwe na wa kuyadumisha si watu wengine zaidi ya wanae.

“Watoto wana nafasi kubwa ya kuhakikisha kwamba baada ya mzee kuondoka bendera ya IPP inapepea, isipopepea tu lawama ni kwa wale aliowaachia.

“Jana (juzi) nilizungumza na Regina (mtoto wa Mengi), nimezungumza na mdogo wake Benjamin akiwa kule Dubai, lakini ndiyo hayo, sisi tuwaombee hawa sasa, Regina, ndugu zake na wengine wahakikishe tu kwamba yale ambayo mzee wao aliyasimamia na aliyoyaonea fahari yanaendelea kudumishwa na kupepea,  kufanya hivyo watakuwa wamemuenzi vya kutosha mzazi wao,” alisema Kikwete.

KAULI YA IGP

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alisema wameshafungua dokezo na kuanza kufuatilia taarifa zinazotolewa na watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Mengi.

“Tunafuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Mengi, hatuzipuuzii, tunafuatilia. Lakini kwa sasa kazi ni kuhakikisha msiba unamalizika kwa amani na utulivu,” alisema Sirro.

Alisema wamejipanga kuimarisha ulinzi siku ya kutoa heshima za mwisho ambayo anaamini kutakuwa na waombelezaji wengi ili watu wenye nia ovu wasipate nafasi ya kuharibu shughuli hiyo.

Pia alisema kifo cha Mengi ni pigo kwao kwa sababu alikuwa mdau muhimu na alilipenda jeshi tofauti na wafanyabiashara wengine.

“Licha ya kuwa na fedha, lakini alikuwa tofauti na matajiri wengine. Polisi imepoteza mdau mkubwa kwa sababu alilipenda jeshi, alikuwa mzalendo na ‘very humble’, alilipenda jeshi tofauti na wafanyabiashara wengine ambao wanaliona jeshi ni adui kutokana na mambo wanayoyafanya, ikiwemo kuvunja sheria,” alisema Sirro.

WAZIRI UMMY

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliyekuwa miongoni mwa waombolezaji, alisema Mengi ni mdau mkubwa wa sekta ya afya, hasa alipoonesha dhamira ya kuanzisha kiwanda cha dawa, hivyo pengo lake ni kubwa na halitazibika.

 “Nimefanya kazi kwa karibu na Mengi tangu nikiwa Naibu Waziri hadi sasa nikiwa waziri, ni mdau mkubwa wa sekta ya afya, tumepata pigo kubwa, hivyo pengo lake halitazibika,” alisema Ummy.

Alisema kama waziri atahakikisha anashirikiana na familia kukamilisha kiwanda cha dawa alichokianzisha ili kuongeza upatikanaji wa dawa nchini.

Mwili wa Mengi unatarajiwa kuwasili nchini kesho kutoka Dubai na kuzikwa Alhamisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles